
Zakia Onesmo
STORI: GLADNESS MALLYA,
Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: NYUMA ya lile tukio la mwanamke mjane aliyetambulika kwa jina la Zakia Onesmo kulazimika kulala nje kwa kufungiwa mlango na ndugu wa mumewe, mapya yameibuka ambapo ndugu wa mume wamedai mama huyo anajitakia na si kwamba ana shida.
Zakia aliripotiwa na gazeti hili wiki iliyopita akieleza kuwa ndugu wa marehemu mumewe wakiongozwa na mtoto mkubwa wa marehemu kwa mama mwingine, Yusuf Mandai wamemfungia mlango wa nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu mumewe, Kasimu Mandai maeneo ya Azimio, Tandika jijini Dar baada ya msiba kumalizika.
Akimzungumzia mama huyo, mtoto mkubwa wa marehemu, Yusuf, alisema kama ndugu wanalaani kitendo alichokifanya mama huyo kwani hakuwa na sababu ya kulala nje wakati tayari amepewa nyumba yake ya urithi iliyopo Kongowe jijini Dar.
“Baada ya mazishi ndugu wote tulikusanyika na yeye (Zakia) akiwepo, tukakubaliana kwa kuwa marehemu baba aliacha nyumba tatu, ya Mlandizi warithi walikuwa ni mke mkubwa wa marehemu na baadhi ya ndugu wengine.
“Nyumba ya Kongowe akapewa yeye mke mdogo (Zakia) na mwanaye Nuru Kasimu Mandai na ya tatu ni ya Tandika ambayo nilipewa mimi na baadhi ya ndugu zangu, ndugu wote tukakubaliana, tukaweka sahihi.
“Tunashangaa kumuona tena mama Zakia akiitaka nyumba ya Tandika wakati kiutaratibu za mirathi si yake kwani baba aliandika kabisa. Kifupi ana matatizo, maana hata maneno aliyoyasema kuwa aliondoka kwenda kwao na kumuacha marehemu baba akiwa mzima ni uongo mtupu.
“Alimuacha baba akiwa mgonjwa. Ni kama alishamtelekeza kwani zaidi ya mwaka mzima hakuwa akiwasiliana na baba kwa chochote, Muda wote huo sisi tulikuwa tunamuuguza mzee hadi alipofariki. Ana uchu wa mali lakini sisi tunamshauri kama ana malalamiko zaidi aende mahakamani lakini si kusingizia hana pa kulala wakati nyumba anayo,” alisema Yusuf.