Mtandao wa waganga kuunganisha watu Freemason - Global Publishers

Imewekwa na on February 1st, 2016 , 10:07:21am

Mtandao wa waganga kuunganisha watu Freemason

2 (2) (1) Kiongozi Mkuu wa Freemason Ukanda wa Afrika Mashariki, Sir Andy Chande.

Stori: Chande Abdallah na Gabriel Ng’osha, WIKIENDA
DAR ES SALAAM: Ama kweli Bongo lazima utumie ubongo! Wakati watu wakisaka utajiri kwa njia ya hata ushirikina na ile ya kuamini unapatikana Taasisi ya Freemason, nyuma ya dhana hiyo kuna kundi kubwa la waganga wa kienyeji ‘sangoma’ ambao wanajifanya Freemason wakidai kutoa utajiri huku wakiishia kutapeli watu.

Hivi karibuni, Kitengo cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kilipokea malalamiko ya watu waliotapeliwa na waganga hao kwa nyakati tofauti.
Waathirika hao walisema sifa kubwa ya sangoma hao ni kutaka watumiwe fedha kwa njia ya simu kisha hutokomea na wanapopigiwa huwa hawapokei.

SIKIA HII
“Jamani watu wanatakiwa kushtuka kwani nyuma ya kuunganishwa Freemason kuna utapeli mzito ambao wajinga ndiyo waliwao. Huu utapeli unafanywa na baadhi ya waganga wa kienyeji.

“Wamesambaza mabango yenye namba zao za simu, wanapopigiwa jambo la kwanza huwa wanataka ulipe kwa njia ya simu na ukituma umeliwa.
“Mimi nimelizwa shilingi elfu ishirini (20,000) na sina utajiri wowote,” alisema mmoja wa waliokuwa wateja wa waganga hao.

IMG_2890OFM YACHUNGUZA
Baada ya taarifa hizo, kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers kilizunguka Jiji la Dar na kushuhudia matangazo mengi ya waganga hao yakiwa yamebandikwa kwenye maeneo mbalimbali.

Sehemu zilizobainika na OFM kuwa na matangazo hayo ambayo mengi yamepigiliwa kwenye nguzo za umeme ni Barabara ya Mandela (maeneo ya Tazara), Barabara ya Morogoro kuanzia Shekilango hadi Ubungo-Mataa, Makaburi ya Ufi, Barabara ya Kawawa (maeneo ya Magomeni-Mataa), Sinza Makaburini, Buguruni na Mbagala Rangi-Tatu kwenye Barabara ya Kilwa.

OFM YATEGA MTEGO
Kama kawaida, OFM ilichimba ukweli wa madai ya utapeli kupitia Freemason hao feki kwa kuchukua moja ya namba za simu zilizopo kwenye matangazo hayo na kuipiga huku mpigaji akiigiza lafudhi ya ‘kishamba’. Majibizano yakawa hivi:

IMG_2892OFM: Haloo, naongea na Freemason?
Freemason Feki: Ndiyo, wewe nani na uko wapi?
OFM: Naitwa Side Chumbageni, mwenyeji wa Tanga, nipo hapa Sinza nimekuja kumtembelea kaka
yangu.

Freemason Feki: Unataka kujiunga na Freemason? Masharti utayaweza?
OFM: Nitayaweza, nipo tayari kumtoa kafara hata mwanangu ilimradi niwe tajiri, nisaidie kaka yangu.

Freemason Feki: Oke, nitumie majina yako matatu kwenye meseji halafu nitakupa namba nyingine unitumie shilingi elfu ishirini ila usiipige namba hiyo. Kama upo siriasi kweli tuma pesa hiyo ndani ya dakika kumi.

OFM: Samahani, pesa hiyo ni ya nini?
Freemason Feki: (kimya kwanza) pesa hiyo ni ya kuangalia nyota yako ili tujue unapaswa kupewa utajiri wa shilingi ngapi, tuma sasa hivi.
OFM: Sawa, natuma sasa hivi maana nina shida kaka. Lakini tunaweza tukaonana? Elfu ishirini siyo kitu, nipo tayari nitoe hata laki tatu mambo yangu yawe mazuri.

IMG-20160119-WA0018Mganga feki.

Freemason Feki: Oke, basi njoo maeneo ya Shekilango, lakini uwe peke yako na hiyo pesa.
OFM YATINGA
Baada ya mazungumzo hayo, makamanda wa OFM walifika eneo waliloelekezwa na kugawana maeneo huku wakiwa na vifaa vya kazi tayari kwa kumnasa mganga huyo feki.

Dakika chache baadaye mtu mmoja aliyekuwa bize na simu alipita mbele ya Kamanda wa OFM kisha kurudi huku simu yake ikiwa sikioni kama vile anatafuta kitu.
Kamanda wa OFM alipojaribu kuipiga namba ya Freemason Feki, simu ya jamaa huyo iliita na alipoipokea kikosi kizima cha OFM kilimuweka mtu kati.

JAMAA AFYATUKA
Hata hivyo, njemba huyo alibaini kuwa, yupo ndani ya mtego, hivyo alitimua mbio mpaka kuwashinda OFM. Alivuka Barabara ya Morogoro bila kujali magari yaliyokuwa yakienda kasi, akaelekea barabara ya kwenda kwenye Makaburi ya Ufi.

IMG_2884APIGIWA SIMU, AWAKA
Baada ya tukio hilo, OFM walimpigia tena simu ambapo aliwaka ile mbaya:
“Ninyi jamaa vipi? Kwa hiyo mlitaka kunikamata? Hayo siyo mambo, kila mtu anatafuta kwa mtindo wake, kwani Freemason nipo mimi peke yangu?” (akakata simu).

KAULI YA SERIKALI YA MTAA
Baada ya kujionea hayo, OFM ilipiga hodi kwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo-Riverside, Sarah Enea ili kumsikia anasemaje kuhusu watu hao:

“Baada ya serikali kutoa amri ya kuondolewa kwa matangazo ya waganga mitaani, tulijua tutapata ahueni lakini ndiyo kwanza yamezidi. Hii ni kazi ya halmashauri zetu.
“Mbaya zaidi hawa watu sisi wajumbe hatuwatambui, hata serikali za mitaa hazitambui kazi zao. Huo ni utapeli tu. Itabidi niende tena Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni ili kazi ya kuyatoa mabango ifanyike na kuwakamata wahusika.”

SIR CHANDE ALISHAFAFANUA
Kwa mujibu wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Freemason Ukanda wa Afrika Mashariki, Sir Andy Chande, watu wanapaswa kuelewa kuwa katika jamii hiyo kubwa duniani, hakuna utajiri unaogawiwa kama wengi wanavyoambiwa. Faida za kuwa Freemason ni kuongeza idadi ya marafiki na kukuza knowledge (ufahamu). Hakuna zaidi ya hapo.

Imeandikwa na Chande Abdallah na Gabriel Ng’osha.

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana