Shoga yangu, ni siku nyingine tena ya Jumanne ambapo tunakutana katika kilinge chetu hiki tunachokitumia kuelimishana na kukosoana kuhusiana na mambo yetu ya chumbani zaidi.
Wiki iliyopita nilizungumza nawe kuhusiana na mke wa mtu kupenda ofa za kilevi kutoka kwa vijana maarufu kwa jina la wasela, nawashukuru walionipigia simu na kunitumia SMS kwamba ilikuwa mada nzuri.
Leo shoga yangu nitazungumza nawe kuhusu tabia ya mwanamke aliyeolewa kumnyima chakula cha usiku mumewe kwa sababu kipato chake kidogo.Nimeamua kutiririka na mada hii kwa sababu nimeshuhudia ndoa kadhaa zilizovunjika kisa kikiwa wanawake kuwafanyia hivyo waume zao.
Ukiacha hao,wapo waliowakimbia na wanaowakimbia waume zao kwa kuwa hawana uwezo na kwenda kwa wanaume wenye nazo.Shoga, hakuna kitu kibaya kama mwanamke kumkimbia mumewe ambaye hana fedha kwani anayetoa ridhiki ni Mwenyezi Mungu na huileta kwa wakati wake.
Kinachoumiza zaidi ni pale mwanamke anapoamua kumnyima au kumpa mumewe chakula cha usiku kwa masharti ya kwamba siku atakayorejea nyumbani na fedha ya kutosha ndiyo atakula chakula cha usiku.
Shoga yangu, huo ni unyanyasaji ambao hakuna mwanaume anayeweza kuuvumilia zaidi ya kumtimua mkewe kisha kutafuta mke mwingine.
Jambo la hekima, ikiwa kipato cha mumeo ni kidogo kaeni chini mjadiliane namna ya kufanya ili kipato chenu kiongezeke siyo kumnyanyasa mwenzio kwa kumnyima unyumba kwani atakuacha kisha akibarikiwa kupata pesa itakuwa aibu yako.