ILIPOISHIA:
Akawa anazunguka huku na kule kama anayetafuta kitu fulani pale nje kwetu, ghafla nikaona mlango ukifunguliwa, baba akatoka kwa kasi na kuwapita watu wote, akasogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amesimama, wakawa wanatazamana.
SASA ENDELEA…
“Ni nani aliyekupa mamlaka ya kuingia kwenye miji ya watu na kutapeli ukijifanya unawatoa watu uchawi?”
“Wewe ni nani wa kunihoji maswali hayo? Wewe ni mchawi na wanakijiji wenzako wamekuchoka hapa kijijini. Hii safari ya ujio wangu ni kwa ajili yako, lazima nikunyooshe.”
“Wewe bado ni mwepesi sana kwangu, huna ubavu wa kushindana na mimi. Isitoshe mimi siyo mlozi kama wewe, mimi ni mtaalamu, tena gwiji,” alisema baba kwa sauti ambayo niliisikia vizuri kisha baada ya hapo akageuka na kurudi ndani, nikamuona yule mganga akivuta na kutoa pumzi ndefundefu kama anayejiandaa kufanya tukio moja kubwa sana.
Alipoingia ndani na kufunga mlango, huku nje yule mganga aliendelea kuzunguka huku na kule, wasaidizi wake wakawa wanampigia manyanga na kumuimbia nyimbo ambazo walizielewa wenyewe.
“Inatakiwa tumkamate kwa nguvu na kumtoa nje, anaonesha ni jeuri sana,” alisema mganga huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wote wakawa wanatingisha vichwa kuonesha kukubaliana na alichokuwa anakisema.
Nilijikuta nikitetemeka sana pale nilipokuwa nimejibanza, nikajua arobaini za baba zilikuwa zimewadia. Japokuwa bado sikuwa na majibu kamili kichwani mwangu kama baba ni mganga au mchawi, bado sikukubaliana na kitendo alichokuwa anataka kufanyiwa kwa sababu ulikuwa ni udhalilishaji wa hali ya juu.
Wakati kundi la wanaume wakijiandaa kuingia ndani kwa nguvu na kuvunja mlango, nilimuona baba akitoka kwa kujiamini, kifua akiwa amekitanguliza mbele na kusimama tena mbele ya mganga, wale watu wote wakamzunguka kisharishari.
“Mnataka kutumia nguvu kunikamata? Hivi mna akili timamu nyie? Haya mwenye ubavu anyooshe mkono wake na kunigusa,” alisema baba kwa hasira. Nilibaki namshangaa baba kwani sikujua amepata wapi ujasiri wa kiasi kile. Kauli hiyo iliwashtua hata wale watu waliokuwa wanataka kumkamata, nikaona wote wakirudi nyuma lakini mganga aliendelea kusisitiza kwamba ni lazima wamkamate kwa nguvu.
Watu wote walipojaribu kufanya hivyo, tulishtuka kuona kimbunga kikubwa ambacho hata sikujua kimetokea wapi, kikianza kuvuma kwa nguvu pale baba alipokuwa amesimama, vumbi jingi na takataka za kila aina zikawa zinarushwa huku na kule, kufumba na kufumbua, baba hakuwepo tena eneo hilo.
Wale watu wote, akiwemo na mganga mwenyewe, walibaki wamepigwa na butwaa, kila mmoja akawa anajifuta vumbi. Sikuwahi kushuhudia kimbunga kikubwa kikitokea, tena usiku kama ule, nikabaki na maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Ametukimbia! Ametukimbia!” alisema yule mganga kwa sauti ya juu, huku na yeye akionesha dhahiri kuwa na taharuki kubwa ndani ya moyo wake.
“Siwezi kuwakimbia kwa sababu hakuna wa kunitisha hata mmoja kati yenu,” ilisikika sauti ya baba kisha nikashangaa kumuona akitokea gizani nakurudi tena pale alipokuwa amesimama awali, nikaona watu wote wakianza kurudi nyuma kwa hofu kubwa kwa sababu walishajua baba anaweza kufanya chochote muda wowote.
“Nataka hili liwe funzo kwako na kwa watu wengine wenye akili kama zako,” alisema baba kwa kujiamini huku akiendelea kumsogelea yule mganga, akafanya ishara kama ananyonga kitu kwa nguvu, kufumba na kufumbua mganga yule alidondoka chini na kuanza kutapatapa kama anataka kukata roho.
Kuona hivyo, watu wote waliokuwa wameandamana na mganga huyo, walitimua mbio, kila mmoja kuelekea njia yake na muda mfupi baadaye, wote walikuwa wametokomea gizani, ikabidi nitoke pale nilipokuwa nimejibanza huku na mimi nikiwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
“Hebu beba huko miguuni tuutoe huu mzoga hapa,” alisema baba, akimaanisha tumtoe yule mganga.
Huku nikitetemeka nilisogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu, tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.
Hahahahah mganga kaingia pabaya duh
huyu mzee noma sana.