×

Vigogo Watatu Watumbuliwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

1Mkurugenzi wa Elimu wa wizara hiyo, Profesa Eustella Bilalusesa.

Na Daniel Mbega

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, imewavua madaraka Wakufunzi Wakazi (Resident Tutors) watatu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kutokana na kukiuka sheria na kupotosha katika kuchagua wanafunzi wanaostahili kujiunga na elimu ya sekondari katika vituo vinavyosimamiwa na taasisi hiyo.

Uamuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Elimu wa wizara hiyo, Profesa Eustella Bhilalusesa, ambaye amemuagiza Mkurugenzi wa Elimu ya Watu Wazima, Fidelis Mafuniko, kuwavua madaraka mara moja wakufunzi hao.

“Ninamuagiza Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (ambaye ninaye hapa) kuwavua maraka Wakufunzi Wakazi wafuatao ambao wamekiuka utaratibu – Wotugu Muganda wa Dar es Salaam, Senorina Kateule wa Dodoma na Steward Ndandu anayesimamia mikoa ya Mwanza na Geita,” alisema.

Kutimuliwa kwa vigogo hao kumetokana na malalamiko yaliyojitokeza katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Geita kutokana na utaratibu wa kuchagua wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza.

Kwa mujibu wa Profesa Bhilalusesa, wakufunzi hao wakazi walikuwa wakichagua wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza katika vituo vya TEWW kupitia halmashauri na mikoa, jambo ambalo halikuwa sahihi.

Kwa hiyo amemtaka mkurugenzi wa TEWW kusitisha mara moja utaratibu wa kuchagua wanafunzi kupitia Halmashauri na mikoa bila ridhaa ya wazazi na walezi kwa sababu tayari suala hilo limeleta mkanganyiko.

Alisema wanafunzi katika vituo hivyo wanapaswa kujiunga kwa hiari kama ilivyo katika shule nyingine zisizo za serikali na kuwataka Wakufunzi Wakazi kutangaza nafasi hizo kwa wanaohitaji ili wajiunge kwa hiari.

“Mkurugenzi wa Taasi ya Elimu ya Watu Wazima atoe elimu kwa umma kuhusu utaratibu sahihi wa kujiunga na Programu ya Elimu ya Sekondari Huria (PESH),” aliongeza.

Awali, Profesa Bhilalusesa alisema, malalamiko yaliyojitokeza mwaka huu hasa kufuatia uamuzi wa serikali kwa kutoa elimu bure kwa shule zote za serikali hadi kidato cha nne ndio uliofichua madudu hayo yaliyokuwa yakifanywa na wakufunzi wakazi.

Alisema kwamba, wakufunzi hao wakazi katika baadhi ya mikoa wamekuwa wakitangaza kuwa wanafunzi hao wamechanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kama wanafunzi wa chaguo la pili katika shule za sekondari za serikali, jambo ambalo siyo kweli na kinyume cha utaratibu.

“Mwaka huu wazazi wamechanganyikiwa zaidi baada ya watoto wao kwenda kwenye vituo husika na kutakiwa kulipa gharama wakati wanajua kwamba elimu ni bure, sasa katika vituo hivi vya TEWW wazazi na walezi wanachangia gharama.

“Kwa kawaida, uchaguzi wa pili hufanywa kwa wanafunzi ambao wamefaulu Mtihani wa Taifa wa Eliumu ya Msingi kwa kupata alama za ufaulu kuanzia 100 hadi 250 lakini hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa nafasi, lakini pale nafasi zinapopatikana wanafunzi hawa huchaguliwa kujaza nafasi hizo,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Sheria namba 12 ya mwaka 1975 kifungu 4 (b), (k), na (q), TEWW inaweza kuendesha mafunzo ya elimu ya sekondari kwa vijana na watu wazima walio nje ya mfumo rasmi wa shule, utaratibu ambao ni wa hiari na wahusika wenyewe ndio huomba kama ilivyo kwa shule zisizo za serikali.

Leave a Comment