×

Mama Samia Kuongoza Tamasha la Pamoja Tunafanikisha

Na Daria Erasto

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza Tamasha la “Pamoja Tunafanikisha” katika kusherehekea maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani itakayofanyika Jumamosi ya Machi 5, ukumbi wa King Solomon, Namanga, Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo ambao ndio waandaji wa tamasha hilo alisema mama Samia pamoja na wadau wengine wa masuala ya wanawake watakutana siku hiyo ili kusheherekea mafanikio ya mwanamke pamoja na kuziangalia changamoto zinazomzunguka na kuzibadili kuwa fursa.

“Kwa kweli tamasha hili litakuwa la aina yake ikizingatiwa hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuwa na makamu wa rais mwanamke tangu kupatikana kwa uhuru, hii itatoa fursa kwa wanawake kuamini kuwa tunaweza kutimiza ndoto zetu kwenye safari ya mafanikio”

Agnes alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inalenga katika kuwaleta pamoja wanawake na wanaume na  kutoa ahadi zao za kuwa mabalozi wa kuharakisha harakati za usawa wa kijinsia katika maeneo  yanayowazunguka.

Alisema ahadi hiyo inasisitiza kuwa kila mmoja ni kiongozi katika eneo lake, hivyo ana budi kuchangia nguvu zake na kuleta msukumo wa upatikanaji wa usawa wa kijinsia.

Agnes alisema tamasha hilo ambalo litafanyika Jumamosi ya Machi 5, kuanzia saa 10 jioni, ukumbi wa King Solomon, Namanga, Dar es Salaam litakuwa jukwaaa muhimu kwa wanawake na wanaume kukutana na kufurahia mafanikio ya wanawake pia kuhamasishana harakati za maendeleo ya wanawake.

Aliongeza kuwa tamasha hilo litakuwa jukwaa la kukutanisha wanawake kutoka fani na kada  tofauti ili kutengeneza mtandao ambao utakuwa chachu muhimu kwa ustawi wao.

Aliongeza kuwa tamasha litaenda sambamba   na watoa mada kutoka nyanja mbalimbali kama vile uchumi na fedha, ujasiliamali na masuala ya afya maonyesho ya biashara ya bidhaa za ubinifu kutoka kwa wanawake, chakula cha usiku na  burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa hapa nchini akiwemo Elias Barnaba na bendi yake ya Clasicc, mkogwe wa muziki wa taarab Mama Patricia Hillary na Misoji Mikwabi ambao wataongozwa na mchekeshaji maarufu MC Pilipili.

Leave a Comment