×

Ndoa na Shetani-18

ILIPOISHIA:

Nilijiuliza kijiwe mbona kimedorora hivyo, lakini walinipa moyo na kunieleza  muda wa kukata tamaa bado, kibaridi cha Nairobi nacho kilikuwa kikichonyota. Majira ya saa nne kasoro wateja wenye magari walianza kutokea kuonesha wengine walikuwa bado wamo maofisini.  Kama kawaida yangu sikuwa mtu wa kupigana vibega  na watu kukimbilia wanaume nilijiamini mwanaume mpenda vizuri lazima angenichagua hata kama nikisimama mbali.

SASA ENDELEA…

Wakati watu wakipigana vibega na mimi kusimama, Sipe alipata nafasi ya kupata bwana ambaye aliingia ndani ya gari lake na gari lilikwenda kusimama mbele kidogo ilionekana mteja alitaka huduma ya haraka. Baada ya dakika ishirini alirudi.

“Vipi Sipe?” Doi alimuuliza.

“Ilikuwa huduma ya chapuchapu si unajua kwa kazi hiyo huwa sicheleweshi.”

“Nakujua.”

Tukiwa katikati ya mazungumzo, ilisimama gari nyingine, kama kawaida walikimbilia lakini mimi sikunyanyua mguu wangu kitu kilichomuudhi Doi na kuniambia.

“Konso shoga yangu changamka hapa siyo Bongo, pia kijiwe hujakizoea lazima uchangamkie tenda siku za mwanzo,” Doi alinishtua.

“Sawa,” nilimjibu huku nikiwa bado nimesimama.

Bahati nzuri kukimbilia kule Doi ilikuwa bahati yake alipata mteja wa kuondoka naye. Nilibakia na shoga zangu wengine ambao ndiyo walikuwa wenyeji wangu. Tulibakia mimi na Bahati ambao tulikuwa hatujapata wateja, majira ya saa nne lilikuja gari moja la kifahari na kusimama karibu na tulipokuwa tumesimama, kama kawaida sikwenda wasichana wote walikimbilia kulizunguka lile gari.

Wenzangu walinishika mkono na kunisogeza kwenye gari. Nilijisogeza hadi karibu na gari ambalo tangu lisimame lilikuwa halijashusha vioo, tuliposogea lilishusha taratibu kisha sauti ilitoka ndani ya gari na kusema:

“Ninyi watatu ingieni.”

Kila mmoja alijinadi yeye lakini msemaji alimaanisha sisi watatu, tuliingia kwenye gari. Ulifungwa mlango na kuondoka bila kusema neno nikajiuliza mbona tumeondoka hakuna maelewano. Niliwaona wenzangu wametulia na mimi nikatulia ili nione mwisho wake.

Gari lilikwenda huku ukimya ukitawala mpaka kwenye jumba moja la kifahari maeneo ya Karen. Baada ya gari kuingia kwenye geti na kwenda kusimama mbele ya jumba lile tulifunguliwa mlango na kuelezwa tuteremke ilionesha wenzangu ni wenyeji wa tukio lile nami niliwafuata.

Baada ya kuteremka tuliingia ndani hadi sebuleni ambako tulikaribishwa kwenye sofa.

“Karibuni warembo.”

“Asante.”

“Mnatumia kinywaji gani?”

Wenzangu walikuwa wa kwanza kusema kuonesha si wageni maeneo yale:

“Tusker Lite.”

Mimi nilichelewa kusema kwa vile sikuelewa tumekwenda kufanya biashara au kufanya nini japokuwa wale walikuwa wateja.

“Mrembo mbona husemi?” aliniuliza kaka mmoja aliyekuwa amependeza na mikufu ya dhahabu shingoni na sikio moja alikuwa amevaa hereni.

Na mimi hiyohiyo,” niliamini haikuwa na tofauti na bia niliyoizoea nyumbani Tanzania ya Castle Lite.

“Ooh! Bahati huyu mgeni?” aliulizwa Bahati na mkaka mmoja kuonesha ni wateja wao wa muda mrefu.

“Ndiyo.”

“Ametokea wapi?”

“Tizedi.”

“Yuko na shepu nzuri sana.”

Mara alitokea mwanaume mmoja aliyekuwa amevalia kaptura iliyovuka magoti, juu alikuwa kifua wazi na kuonesha michoro ya tatuu mkononi alikuwa na glasi iliyokuwa na pombe ndani.

Itaendelea katika Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave a Comment