Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet anayetokea familia ya kimaskini na Anna anayetokea familia ya kitajiri. Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana na kuahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo yake moja kushindwa kufanya kazi.
Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, baadaye wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet kutokana na umaskini wake wakidhani hana hadhi ya kumuoa Anna.
Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.
Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India na Jafet anafuatwa Tanzania baada ya hali ya mgonjwa kuwa mbaya.
Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.
Wanafunga safari ya kurejea Tanzania na hatimaye wanawasili jijini Mwanza kisha siku inayofuatia wanaelekea kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa wazazi. Hilo wanalikamilisha na mwisho wanasafiri mpaka jijini Dar es Salaam kufuatilia uhamisho wa Jafet chuoni ambapo kijana huyo anamuandikia ujumbe mzito mpenzi wake wa chuoni hapo, Suleikha.
Hata hivyo, anakosa ujasiri wa kumpa ujumbe huo na kuishia kubabaika.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
Alipoingia kwenye teksi, baba yake Anna alimwambia dereva awashe gari, taratibu wakaondoka eneo hilo huku Suleikha na yule rafiki yake wakiwapungia mkono mpaka walipopotea kwenye upeo wa macho yao.
“Usilie Jafet! Jikaze, wewe ni mwanaume, sote tumepitia huko,” alisema baba yake Anna huku akimpigapiga Jafet mgongoni, kitendo kilichosababisha azidi kulia kwa uchungu. Alijikuta akiwa katika wakati mgumu mno kihisia, hakujua afanye nini kwa wakati huo.
“Kwani kikubwa kinachokusumbua ni nini? Hebu dereva simamisha kwanza gari kisha utupishe,” alisema baba yake Anna, dereva ambaye tayari alikuwa ameingia kwenye Barabara ya Umoja wa Mataifa alitii alichoambiwa, akapunguza mwendo na kutafuta sehemu nzuri ya kuegesha gari, pembezoni kabisa mwa barabara.
“Najisikia vibaya kumuumiza Suleikha. Alikuwa pembeni yangu katika kipindi nilichokuwa nahitaji msaada, akanisaidia kuniponesha majeraha makubwa kwenye moyo wangu, leo na mimi narudia kumuumiza vilevile kama mimi nilivyoumia, isitoshe hajawahi kunifanyia jambo lolote baya, najisikia vibaya sana,” alisema Jafet huku machozi na makamasi vikimtoka kwa wingi.
“Kuna kingine kinachokusumbua kichwa chako?”
“Hapana, kubwa ni hilo, najihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wangu.”
“Hebu kuwa muwazi kwangu, unampenda nani kati ya Suleikha na Anna? Niambie ukweli na wala usiogope chochote kwa sababu nataka kukusaidia.”
“Nampenda sana Anna na yeye ndiyo chaguo la moyo wangu.”
“Basi kama ni kweli unachokisema, hili suala la Suleikha niachie mimi, nitatafuta muda wa kuja kuzungumza naye na naamini atakuelewa. Kwa sasa usimwambie kitu kingine chochote zaidi ya kumueleza kwamba una matatizo nyumbani kama ulivyomwambia,” alisema baba yake Anna, kauli ambayo ilimpa nguvu Jafet, akafuta machozi na kamasi na kushusha pumzi ndefu.
“Kama kuna jambo jingine linalokusumbua tafadhali niambie na wala usisite kuniambia chochote muda wowote, nataka uwe salama kwa sababu naamini wewe ukiwa salama, mwanangu naye atakuwa salama,” alisisitiza baba yake Anna, Jafet akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.
Wakamuita dereva teksi ambaye aliingia ndani ya gari na safari ya kuelekea hotelini walikofikia ikaanza. Njia nzima baba yake Anna alikuwa akimpigisha Jafet stori za hapa na pale ili kumpoteza mawazo, kazi ambayo kwa kiwango fulani ilifanikiwa kwani mpaka wanafika hotelini, Jafet alikuwa akiongea na kucheka kiasi kwamba haikuwa rahisi kwa Anna kujua nini kilichotokea.
“Vipi mmefanikiwa?”
“
Kila kitu kimekamilika, hapa kilichobakia ni kupanda pipa kuelekea Marekani tu,” alisema Jafet, wote wakacheka na kugongesheana mikono.
Usiku huo walilala hotelini hapo huku mara kwa mara baba yake Jafet akiwa makini kuhakikisha wawili hao hawavukiani mipaka kwani kulikuwa na kila dalili kwamba wakiachwa wenyewe, wanaweza kufanya mambo ambayo ni kinyume na mila na desturi za Kitanzania.
Kesho yake asubuhi waliondoka kwa ndege ya kwanza kurejea jijini Mwanza kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusafiri kuelekea nchini Marekani. Saa tatu za asubuhi, tayari ndege waliyokuwa wamepanda, mali ya Shirika la Precision Air ilikuwa imeshatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Jafet, Anna na baba yake wakateremka ambapo nje ya uwanja, walimkuta dereva wa familia hiyo akiwasubiri, akawachukua ndani ya gari la kifahari la mzee huyo na kuwapeleka mpaka Capri Point, nyumbani kwao.
Ili kumkwepa Suleikha, Jafet aliamua kubadilisha laini ya simu aliyokuwa anatumia lakini kabla ya kufanya hivyo, alimtumia ujumbe Suleikha na kumueleza kwamba alikuwa akikaribia kufika kijijini kwao, Rwamgasa na kumwambia kwamba kwa sababu mtandao wa simu ulikuwa ukisumbua kijijini hapo, akimkosa hewani asishangae.
Hakukuwa na muda wa kupoteza tena, maandalizi yaliendelea kufanyika huku kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, si Jafet wala Anna, kila mmoja alikuwa anatamani muda usonge mbele haraka na waondoke pamoja, kwenda sehemu ambayo hakuna mtu ambaye angewasumbua.
Siku tatu baadaye, maandalizi yote yalikuwa tayari yameshakamilika. Baba yake Anna, Jafet na Anna wakasindikizwa na wanafamilia mpaka uwanja wa ndege ambapo walisafiri tena mpaka jijini Dar es Salaam ambako walifanya utaratibu na kupata nafasi kwenye ndege kubwa ya KLM.
Saa tisa za jioni, tayari wote walikuwa ndani ya ndege, Jafet akiwa na shauku kubwa ya kufika Marekani kwani katika maisha yake yote, hakuwahi kufika zaidi ya safari ya India. Pembeni yake alikuwa amekaa Anna ambaye muda wote alikuwa amemganda kama ruba.
Hatimaye safari hiyo ndefu ilianza, ndege ikapaa na kuiacha ardhi ya Tanzania na kuanza kupasua mawingu kwa kasi kubwa kuelekea nchini Marekani. Kituo cha kwanza kilikuwa ni jijini Doha, Qatar ambapo ndege hiyo ilitua na kufanyiwa marekebisho madogo ikiwa ni pamoja na kuongezwa mafuta.
Safari ikaendelea na baada ya saa nyingi angani, hatimaye sauti laini ya mhudumu wa ndege, ilisikika ikiwataarifu abiria wote kufunga mikanda wakati ndege ikijiandaa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK jijini New York, Marekani.
“Whaoo! Huku ndiyo duniani sasa, cheki kulivyo kuzuri,” alisema Jafet, kauli iliyowafanya Anna na baba yake wamcheke kwani kwao haikuwa mara ya kwanza kufika nchini humo.
“Inabidi ujikaze basi mpenzi wangu usishangae sana, utaniaibisha mkeo,” alisema Anna, kauli iliyozidi kuwafanya wote wacheke kwa furaha. Dakika kadhaa baadaye, tayari walikuwa wameshakamilisha taratibu zote za usalama uwanjani hapo na kutoka hadi nje.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/