×

Miaka 15 Ateseka na Mguu

Mgonjwa mguu mwanza (1) Msichana Debora Nekodemu.

Stori: Idd Mumba,  UWAZI

Mwanza: Msichana Debora Nekodemu 25, (pichani) mkazi wa Kijiji cha Nyambiti, Kata ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, amepoteza mwelekeo wa maisha yake, ikiwemo kutimiza ndoto yake ya kusoma kuishia njiani kutokana na ugonjwa wa ajabu unaomtesa kwa takriban miaka 15 sasa.

Mguu waanza kuvimba

Msichana huyo alianza kuugua tangu akiwa na umri wa miaka kumi, akisema mguu wake ulianza kuvimba kidogokidogo na kuongezeka kadiri siku zilivyosonga mbele hadi kushindwa kwenda shule au kufanya shughuli zingine kama awali.

Apelekwa Bugando, akosa huduma

Ili kunusuru maisha ya msichana huyo, wasamaria wema  walimpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza ili kufanyiwa vipimo ambavyo vingesaidia kupata matibabu ya ugonjwa wake lakini pamoja na kufanyiwa vipimo ikiwemo X-ray,  madaktari hawakugundua chanzo cha uvimbe huo.

Mgonjwa mguu mwanza (3)Baada ya madaktari kushindwa kupata kiini cha uvimbe huo, waliwaruhusu kurudi nyumbani.

“Niliporudi nyumbani hali ilizidi kuwa mbaya, ikabidi nirudi tena Bugando kupata vipimo kwa mara ya pili, lakini majibu yalitoka kama yale ya kwanza, nilijiuliza mambo mengi sana lakini bila majibu, nikakata tamaa ya kupata matibabu maana sina msaada wowote hadi leo.

“Bibi aliyekuwa ananilea alifariki dunia baada ya mama yangu pia kufariki, simjui baba yangu kwani aliondoka nyumbani miaka mingi kabla hata mama hajafariki, kwa sasa naishi kwa shangazi ambaye hana uwezo wa kunihudumia wala kugharamia matibabu.”

Anaishi kwa kuombaomba mitaani

Katika mahojiano na mwandishi wa habari hii wiki iliyopita nje ya Hoteli ya Mwanza, Debora alisema baada ya mama na bibi yake kufariki, amekuwa akiishi maisha ya kuombaomba mitaani ili kupata fedha kwa ajili ya kununulia chakula pamoja na fedha ya kodi ya chumba anachoishi na shangazi yake.

Aomba msaada kwa Watanzania

“Ninachowaomba Watanzania wenzangu mnisaidie hata angalau nipate matibabu ama kunijengea nyumba ili niweze kuishi kwa amani, kwani katika nyumba za kupanga napata shida sana, wananinyanyasa na kunitenga kutokana na hali yangu ilivyo,” alisema.

Kwa yeyote aliyeguswa na hali ya Debora na anahitaji kutoa msaada awasiliane naye kwa simu namba 0768420924.

Leave a Comment