×

Mkuki moyoni mwangu – 53

BILIONEA Jackson Motown anafanikiwa kuwaondoa duniani watu ambao kama wangesimama mahakamani na kuthibitisha kwamba alibaka na baadaye kuua, hukumu yake ingekuwa ni kifo! Mtu pekee ambaye amebaki anayeamini ni hatari kwake ni Catarina ambaye FBI wamemficha mahali kusikojulikana akilindwa saa ishirini na nne.
Akiwa mahabusu kusubiri kesi yake, Jackson Motown anamtumia kijana wake wa kazi maarufu kwa jina la Dracula kuendeleza unyama wake, hivi sasa wanatafuta mahali alipo Catarina ili waweze kumuua akiwa huko huko.
Akiwa mafichoni Catarina amepatwa na tatizo la kisaikolojia sababu ya kumfikiria sana Kevin, hawezi kula chakula na muda mwingi analia! Wazazi wake mwisho wanafikia uamuzi wa kutafuta msaada wa kisaikolojia, wanawasiliana na FBI kuwaomba wawaunganishe na mtumishi wa Mungu atakayekuwa akija kumpa Catarina nasaha pamoja na maombi.
Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

ILITHIBITIKA kwa hali aliyokuwa nayo Catarina kwamba alihitaji msaada wa kisaikolojia, bingwa wa masuala ya saikolojia ndani ya FBI, Dk. Amran Kaima, aligundua kilichokuwa kikimsumbua Catarina na kufanya afya yake idhoofike lilikuwa ni tatizo liitwalo Post Traumatic Stress Disorder (PTSD) lililohitaji nasaha za haraka na wazazi wa Catarina walipendekeza apatikane mchungaji au kiongozi yeyote wa dini.

“I know an Orthodox Priest in town who is very good at councelling people, he did help my sister who had almost the same condition!” (Namjua Padri mmoja wa dhehebu la Orthodox ambaye ni mzuri sana kwa masuala ya nasaha, alimsaidia dada yangu aliyekuwa na tatizo linalofanana kabisa na hili!)
“Are you sure?” (Una uhakika?)
“Yes boss!” (Ndiyo mkuu!) alijibu Clarence Nicolaus, mmoja wa vijana walioshiriki katika zoezi la kumlinda Catarina mahali alikofichwa.
“Then bring him next week on Monday!” (Basi mlete wiki ijayo Jumatatu!)
“I will do that boss, without miss!”(Nitafanya hilo mkuu, bila kukosa!)
Baada ya mazungumzo hayo Clarence Nicolaus aliondoka ndani ya chumba cha mikutano akionekana mwenye furaha, kama vile alifurahi sana Catarina kupona tatizo lililokuwa likimsumbua. Nje ya ofisi ndani ya gari lake alichukua simu na kubonyeza namba fulani, ilipopokelewa alianza kuongea.
“Yes Major, can I speak to the boss?”(Ndiyo Meja, naweza kuongea na bosi?)
“Hold on! The prison superintendent is here, call in the next twenty minutes!” (Subiri kidogo! Mkuu wa gereza yuko hapa, piga baada ya dakika ishirini!)
Dakika ishirini baadaye alipiga tena namba hiyohiyo, Meja akapokea na kumuunganisha na Jackson Motown, akamweleza kila kitu walichoongea juu ya mchungaji na mtu wa kumpatia Catarina ushauri na kumtaka afanye kila kinachowezekana kumtafuta mtu anayeweza kujiweka kama mchungaji wa Dhehebu la Orthodox, kuanzia mavazi mpaka muonekano wa ndevu.
“I am sure, Dracula will handle that!” (Nina uhakika, Dracula atalishughulikia jambo hilo!) Jackson Motown alijibu na kukata simu kisha kumkabidhi Meja Peter Johnson.
***
Kesi ya Jackson Motown na wenzake ilikuwa ikitajwa tena mahakamani, idadi kubwa ya watu ilifurika kufuatilia, vyombo vya habari vyote vilikuwepo, watu wakitaka kufahamu nini ingekuwa hatima kwa mtu tajiri mwenye ushawishi kama yeye nchini Marekani.
Waliposimamishwa kizimbani walikana mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili kwa mara nyingine tena, upande wa mashitaka ukaieleza mahakama kwamba bado upelelezi ulikuwa haujakamilika. Ilikuwa ni kazi ngumu sana kupata ushahidi na vielelezo vya kutosha kumtia Jackson Motown hatiani, alishawaua watu wote ambao wangeweza kusimama mahakamani kutoa ushahidi dhidi yake isipokuwa watu wawili tu ambao ni Catarina na Mariana.
Aliporejeshwa mahabusu siku hiyo alimwita Meja Peter Johnson na kumwomba simu yake, akabonyeza namba ya Dracula, ilipopokelewa alitoa maagizo ya watu hao wawili kuhakikisha nao wanaondoka duniani kwani uwepo wao ulikuwa unatishia uhai wake.
“Mariana ni kazi rahisi, yuko Miami, tutaifanya kazi ya kuwaondoa wote duniani siku moja, kabla kesi hii haijatajwa tena!”
“Fanyeni hivyo haraka bila kukosa, hawa watu ni hatari mno kwangu, nataka kesi hii iishe niingie tena barabarani na njia pekee ya kuimaliza ni kuondoa ushahidi wote unaoweza kuthibitisha kwamba nilibaka na kuua!”
“Sawa mkuu!”
“Nakuamini!”
“Endelea kuniamini!”
Simu ikakatwa na kukabidhiwa Meja Peter Johnson ambaye aliondoka taratibu eneo hilo bila mtu yeyote kugundua kwani ilikuwa ni marufuku kwa mtu aliyekuwa mahabusu kuongea na simu, kiasi kikubwa sana cha fedha kilikuwa kimetumika kumfanya askari huyo kuwa kibaraka wa Jackson Motown.
***
Siku ya Jumatatu asubuhi, majira ya saa mbili na dakika kumi na tano, gari ndogo aina ya Morris, muundo wa kizamani kabisa iliegeshwa mbele ya jengo la FBI, ndani yake akashuka mzee mwenye ndevu nyingi zenye mvi, miwani ya duara kama aliyotumia marehemu Mahatma Ghandhi, mkononi mwake alikuwa ameshikilia kitabu cheusi ambacho kwa kukitazama kutokea mbali kilionekana ni Biblia.
Shingoni mwake alivalia mkufu mkubwa na mrefu wenye msalaba ulioning’inia kifuani, huku kiunoni akiwa amejifunga mshipi wa rangi nyeupe ulioifunga vizuri kanzu yake nyeusi iliyoshuka hadi miguuni na kuvificha viatu vyake! Akafunga mlango wa gari taratibu kama vile mikono yake haikuwa na nguvu kisha kuanza kutembea kwa mwendo wa taratibu akizifuata ngazi za kuingia ndani ya jengo la FBI.
“Praise the Lord, priest!”(Padri, tumsifu Bwana) mlinzi mmoja wa kike aliyekuwa mbele ya jengo alimsalimia, hapakuwa na ubishi wowote, kwa kumwangalia mzee huyo wa makamo mtu yeyote angekiri alikuwa ni Mtumishi wa Mungu wa dhehebu lenye misimamo la Orthodox!
“Am…eee…n!” aliitikia mzee huyo.
“What can I do for you?”(Nikusaidie nini?)
“I am here to visit the councelling department!”(Niko hapa kuwatembelea watu wa idara ya ushauri nasaha!)
“Ooh! Let me escort you, can I help you to carry your bag sir?”(Ooh! Acha nikusindikize, naweza kukusaidia kubeba begi lako?)”
“Thank you! But I can do it myself!”(Ahsante! Lakini naweza kubeba mwenyewe!) aliongea mzee huyo akitabasamu.
Mlinzi akamwongoza moja kwa moja hadi kwenye lifti ambako waliingia ndani na kubonyeza namba mbili, huko ndiko kitengo cha ushauri nasaha ndani ya FBI kilipokuwa, mtumishi huyo wa Mungu akapokelewa vizuri na kuingizwa kwenye chumba cha mikutano, dakika kumi baadaye watu watatu wakaingia kwa ajili ya mahojiano.
“We are sorry that Clarence Nicolaus did not come to pick you, he is assigned to something else!”(Samahani sana Clarence Nicolaus hakuja kukuchukua, amepewa kazi nyingine!)
“It’s okay, my name is father Coronel Garsia, a councelling specialist, Clarence told me that I can help the FBI with my expertise!” (Hakuna shida, naitwa Padri Coronel Garsia, mtaalamu wa ushauri nasaha, Clarence aliniambia naweza kusaidia FBI na utalaam wangu!)
“Yes, we have a client who needs Psychotherapy!” (Ndiyo, tunaye mteja anayehitaji tiba ya kiakili!)
“I am ready!” (Niko tayari!)
“Thank you so much, we will be leaving in the next half an hour to where she is!” (Ahsante sana, tutaondoka hapa kwenda mahali alipo nusu saa ijayo!)
Wote wakaondoka na kumwacha Padri Coronel akiwa peke yake, moyoni mwake alikuwa na furaha, si kwa sababu alikuwa anakwenda kumsaidia Catarina, bali sababu alikuwa anakwenda kugundua mahali alipofichwa, jambo ambalo lingerahisisha kuuawa kwa Catarina.
Pembeni akaona kuna kioo, mara moja akanyanyuka na kukisogelea kisha kuanza kujiangalia mwenyewe ndani ya kioo hicho, tabasamu likambana kwa jinsi alivyokuwa anafanana na mapadri wa Kanisa la Orthodox! Aliposikia hatua za watu wakitembea kuelekea kwenye chumba alichokuwa, haraka alirejea kwenye kiti na kuketi.
“Mpaka waje kugundua kwamba mimi ni Dracula, Yesu atakuwa amesharejea na kuondoka!” aliwaza moyoni mwake, mlango ukafunguliwa.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia Siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave a Comment