Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za Teknolojia, Benedict Ndomba (kulia) akisoma taarifa mbele ya wanahabari (hawapo pichani), kushoto ni Ofisa Habari Mwandamizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Jonas Kamaleki.
Viongozi hao wakisikiliza maswali kutoka kwa wanahabari (hawapo pichani).
SERIKALI leo imetoa mwongozo wa matumizi sahihi ya mfumo wa teknolojia yaani ‘TEHAMA’ na kuandaa viwango na miongozo mbalimbali inayotoa maelekezo na uafafanuzi wa taratibu zinazotakiwa ili kuwa na matumizi sahihi na salama ya teknolojia ya Habari na mawasiliano katika hatua za kupanga, kupata, kubuni, kununua, kusimamia na kuendesha mifumo mbalimbali ya Tehama serikalini.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Msimamizi wa Huduma za Tehama, Benedict Ndomba, amesema miongozo na viwango hivyo vinalenga kuziwezesha taasisi za umma kujenga mifumo inayoendana na mahitaji halisi ya taasisi husika na kuepuka mifumo inayojengwa kwa shinikizo la wafanyabishara, wafadhili au kwa matakwa ya mtu binafsi.
Aidha, Ndomba alibainisha taratibu za kusanifu,kutengeneza na kuendesha mifumo inayowasiliana na kubadilishana taarifa miongoni mwa taasisi hizo ili kuboresha utoaji wa maamuzi na huduma kwa wananchi wanaoishi mijini na vijijini kwa haraka na gharama nafuu huku ufanisi ukiwa mkubwa.
Alisema serikali itakuwa na uwezo wa kuepuka urudufu wa mifumo na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji na kuwa na mifumo endelevu na yenye gharama halisi na inayofuata viwango vya usalama katika kulinda taarifa za serikali.
Alifafanua kuwa wakala wa serikali anashauri taasisi zote za umma ikiwa ni pamoja na wizara mbalimbali, idara zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, wakala wa serikali/mamlaka, bodi, tume, mabaraza, mifuko, mashirika ya umma na mamlaka za serikali za mitaa kufuata miongozo na viwango vilivyotolewa katika uanzishaji na usimamizi wa mifumo ya Tehama serikalini.
Ndomba aliongeza kuwa viwango na miongozo hiyo hupatikana katika tovuti ya Wakala ya Serikali kupitia www.ega.go.tz huku akieleza wafanyabiashara wanaojihusisha na miradi au utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA serikalini wanashauriwa kufuata miongozo na viwango ili kujua mahitaji halisi ya selikali na kuweza kujenga mifumo ya teknolojia endelevu na inayoleta tija kwa umma.
Na Denis Mtima/Gpl.