Kutokana na maombi ya wasomaji wengi, kwamba wanachelewa kusubiri mkasa kwa wiki moja, sasa mkasa huu utakuwa ukitoka na siku ya Alhamisi kwenye Gazeti la Amani. Kwa hiyo ukisoma Alhamisi ijayo, kesho yake utausoma kwenye gazeti hili.
“Mimi kwa jina naitwa Juma Ally lakini wengi hupenda kuniita Jumaa au Tolu. Jina la Tolu nilipewa kutokana na huu urefu wangu. Nimefanya kazi ya ubaharia kwa miaka 22. Tangu mwaka 1985 mpaka 2007 nilipoamua kuacha mwenyewe nikiwa na miaka 61 kama sikosei,” anasimulia Tolu ambaye kwa umri wake wa miaka 71 sasa naweza kumwita mzee Tolu.
Anaendelea: Wakati naanza kazi hiyo mwaka 1985 nilikuwa na miaka 39, wengi waliniambia si kazi nzuri kwa vile muda mwingi nitakuwa kwenye maji. Lakini pia waliniambia kwamba, baharini kuna mambo mengimengi ya ajabu na tena ni ya kutisha.
Baba yangu mkubwa, sasa ni marehemu aliniambia kisa kimoja kwamba, aliwahi kusikia kuwa, baharini ndiko kwenye makazi au makao makuu ya majini. Majini ninayosema mimi namaanisha vile viumbe.
Kwa hiyo, akasema kufanya kazi ya ubaharia ni kujikaribisha na viumbe hao ambapo wengi wanajua kwa kuwasikia tu lakini waliyokumbana nao ni wachache, kama mimi hapa mzee Tolu.
Moyo wangu ulishaamua kwa vile kazi yenyewe alinitafutia bwana mmoja anaitwa Mohammed Omar. Alikuwa Mwarabu. Kwa sasa hivi ni marehemu. Alikuwa akiishi Zanzibar baadaye akaenda Oman ambako mauti yalimkuta huko.
Meli yangu ya kwanza kufanyia kazi iliitwa Cape na nilianzia Mombasa nchini Kenya. Kwenye meli hiyo tulikuwa wafanyakazi kama 12, wakiwemo na Wazungu.
Wiki moja baada ya kuanza kazi, siku hiyo nakumbuka ilikuwa saa tano usiku, tulikuwa tunatoka Sri Lanka kwenda kisiwa kimoja kinaitwa Sumatra ambacho ni sehemu ya Indonesia, majini tulikumbana na tukio la kwanza mpaka nikatamani kurudi au kushuka niache meli iendelee na safari kama ingekuwa ni barabarani.
Tulifika mahali fulani tukakuta mbele yetu kuna Wazungu wamesimama juu ya maji. Nahodha alipambana sana ili kuzuia kuwakuta lakini kadiri meli ilivyokuwa ikiwakaribia walionekana kuwa mbele lakini hawatembei.
Mfanyakazi mwenzangu mmoja anaitwa Nurdin, akaniambia nisiogope kwa vile matukio kama yale baharini ni ya kawaida sana. Lakini mimi nilishindwa, nikachukuliwa na kupelekwa kwenye chumba cha staff ambacho kilikuwa kikitumika endapo kuna dharura ya mfanyakazi kuugua ghafla.
Nilipokuwa kwenye chumba hicho, nilijisikia kuangalia nje kwa kutumia dirisha lakini nikiwa na hofu kwamba naweza kuwaona wale Wazungu. Kweli bwana, nilipoangalia tu, niliwaona wakiwa nje ya meli na walikuwa wakiniangalia huku mmoja akiachia tabasamu.
Nilitoka kwenye chumba hicho mbio na kurudi kwa wenzangu ambapo niliwaambia kuhusu wale Wazungu. Nurdin ambaye ndiye aliyetokea kuwa rafiki yangu mkubwa, akanikumbusha tena kuacha kuondoa hofu kuhusu viumbe wale:
“Bwana Mohammed, ukiwa hivyo utashindwa hii kazi. Wenzako tumeona mengi sana hilo ni dogo tu. Kuna wakati mwingine wanaingia mpaka ndani ya meli na kutufanyia vituko, lakini mpaka leo bado tunafanya kazi.”
Nilijipa moyo lakini wasiwasi bado ulikuwepo kwani sasa walikuwa bado wanaonekana kwa mbele na pembeni na ilionekana meli inakwenda kuwagonga.
Je, unajua kilichoendelea? Usikose kusoma Alhamisi kwenye Gazeti la Amani.