Wanafunzi wengi nchini hutokea kwenye kaya zenye kipato cha kawaida, kwa mujibu wa takwimu mbalimbali inatajwa kuwa asilimia 70 ya familia za wanafunzi nchini ni za wazazi wakulima na wafanyabishara ndogondogo, kundi ambalo hutafsiriwa kama wananchi wa hali ya kawaida.
Ni suala lililo wazi kabisa kuwa wanafunzi kwenye familia hizi kwa nyakati tofauti hushindwa kufikia mahitaji ya ziada kama vile; kusoma shule zenye ufundishaji mzuri, kupata vifaa vya kisasa vya kujisomea kama vile kompyuta na wengine wakishinda kabisa kufikia mahitaji muhimu kama; chakula, malazi, mavazi na hata huduma za afya pindi wanapoumwa.
mambo hayo yote huweza kusababisha mwanafunzi kufeli au kupata ufaulu mdogo ukilinganisha na yule anayetokea familia yenye kipato kikubwa.
Wanafunzi wanaotokea kaya zenye kipato cha kawaida, mara nyingine hujikuta wakipaswa kugawanya muda wa kusoma na muda wa kufanya shughuli za kujiingizia kipato au kujikimu wenyewe suala ambalo huwafanya washindwe kuhudhuria masomo yao ipasavyo.
Hivyo basi wanafunzi wengi wanapopitia hali hii hukata tamaa na kuacha masomo yao na hatimaye kufeli masomo na baadaye kuishi maisha magumu.
Jambo ambalo wanafunzi wanapaswa kufahamu ni kwamba pamoja na ugumu wa hali ya maisha unaowakuta, hawatakiwi kufanya hicho kama kisingizio cha wao kutofikia malengo yao kitaaluma.
Mifano ipo hai kuwa wanafunzi wengi wanaotokea familia maskini wapo wanaofaulu vizuri pamoja na changamoto za kimaisha wanazozipitia.
Siri ya ufaulu huo unatokana na ukweli kwamba wanafunzi hao wengi huchukia umaskini wa familia zao na kuamua kupambana kupitia elimu hadi tone la mwisho na hatimaye kujikuta wakifaulu na mwishowe kubadili maisha yao kwa ujumla.
Ushauri kwa wanafunzi wote ni kwamba, wanapaswa kugeuza changamoto za kimaisha kuwa ari ya kusoma kwa bidii na kusonga mbele kwani matunda yake ni makubwa hapo baadaye.