ILIPOISHIA…
MAHAKAMA imemwachia huru Jackson Motown na wenzake wote aliokuwa amekamatwa nao kwa kesi ya mauaji na kubaka, baada ya ushahidi kukosekana ili kuwatia hatiani! Kwanini mashahidi wamekosekana? Jackson Motown akimtumia muuaji wake Dracula aliwaua watu wote ambao wangeweza kusimama mahakamani kutoa ushahidi dhidi yake.
Hakutaka kabisa abakie mtu yeyote aliyekuwa anafahamu siri ya mambo yaliyotendeka, ndiyo maana walipofika nyumbani na Dracula walikunywa pombe nyingi na kusherehekea ushindi lakini baadaye alimtaka waongozane pamoja ili akampe malipo yake, wakaingia ndani ya boti na kwenda umbali mrefu katikati ya Bahari ya Atlantic, huko Jackson Motown alichomoa bastola na kumwamuru Dracula asimame na kunyoosha mikono juu.
Bila huruma alimmiminia risasi, akaanguka chini akivuja damu nyingi na kutulia, alichokifanya Jackson Motown ni kumfunga Dracula kamba kiunoni ambayo aliiunganisha na chuma kizito, akamzamisha majini pamoja na chuma hicho! Akatabasamu akijua Dracula asingeonekana tena.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…
BOTI ndogo ya Jackson Motown aina ya Honda 2200 ilikatisha maji kwa kasi ya ajabu, yeye akiwa ametulia ndani yake, moyo umejaa furaha, akiamini sasa alikuwa mtu huru kusingekuwa na yeyote wa kumtia hatiani kwa makosa aliyoyatenda! Dhambi yake ya kumbaka Catarina ilikuwa imeondoka na roho za watu wengi lakini hakusikitika.
“I had no option but killing him!”(Sikuwa na njia nyingine ya kufanya isipokuwa kumuua!) aliwaza alipomfikiria Dracula.
Watu wengine aliowahofia ni Dragon na wenzake watatu, lakini hao kwa hali waliyokuwa nayo, wakiwa hawana uwezo wa kuona, tena wakimtegemea yeye kwa maisha yao yote yaliyobaki duniani, alijipa moyo na kuamini wasingefungua midomo yao kuzungumza chochote cha kumtia hatiani na kama wangefanya hivyo wao pia wangekuwa miongoni mwa washtakiwa.
Dakika thelathini na tano baadaye boti yake ilikuwa ikigota ufukweni kando ya jumba lake la kifahari, akashuka na kutembea taratibu hadi ufukweni kisha kuelekea ndani ambako aliendelea kunywa pombe kali mpaka asubuhi, mfanyakazi wake wa ndani alipoingia ndipo akaondoka kwenye baa iliyokuwemo ndani ya nyumba yake na kuelekea chumbani ambako alijitupa kitandani na kulala.
Alipozinduka saa tisa alasiri, aliingia bafuni na kuoga kisha kuvaa nguo safi na kuelekea chumba cha chakula ambako alikuta kila kitu kikiwa tayari, akala mfanyakazi wake akiwa pembeni bila kuongea naye lolote! Baadaye aliketi sebuleni na kuanza kufuatilia vyombo vya habari, kuanzia CNN, BBC, Sky News na Fox News, kote aliongelewa vizuri kama mtu aliyeteseka mahabusu kwa makosa ambayo hakuyafanya, kifupi alionekana shujaa.
Jioni ya siku hiyo rafiki zake na wafanyakazi wa kampuni zake walianza kumtembelea kwa lengo la kumpa pole, hakuna aliyeulizia juu ya Dracula, tangu siku hiyo na kuendelea ilikuwa ni sherehe mfululizo na mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari! Kuelezea mambo yaliyompata na alivyojisikia baada ya kuachiwa huru.
“Nimewasamehe wote waliofanya nikaingia mahabusu, najua ni maadui zangu wa kibiashara, namshukuru Mungu niko hai!” alisema katika moja ya mahojiano, karibu kila mtu aliyemwona akihojiwa alimwonea huruma kwa jinsi alivyofanikiwa kujenga picha ya mtu asiyekuwa na hatia mbele za macho ya watu.
Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani pia walimtumia salamu za pole na pongezi, hakuna mtu hata mmoja aliyefanikiwa kuelewa kilichofanyika nyuma ya pazia mpaka Jackson Motown kuonekana hana hatia.
***
Juhudi za kuwatafuta Catarina na Padri Coronel Garsia zilikuwa bado zikiendelea, hawakujulikana walikokwenda baada ya ajali mbaya ya gari kugongana na Katapila! Polisi na FBI waliamini kabisa hicho ndicho kilichokuwa kimetokea, haikuwa ajali ya kupangwa, ilitengenezwa vizuri katika namna ambayo mtu yeyote asingeweza kuhisi, watendaji hawakuacha alama yoyote nyuma.
Shida pekee ilikuwa ni mahali walipokuwepo watu hao wawili, wazazi wa Catarina walikuwa wakilia kila siku, kama ilivyokuwa kwa wazazi wa Kevin! Wote sasa walikuwa wamepoteza watoto wao kama kweli Catarina pia alikuwa amekufa au kuuawa kisha mwili wake kutupwa au kufukiwa mahali fulani.
Hawakukata tamaa, waliwashinikiza FBI kwa kutumia Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani angalau wachunguze ukweli wa ajali iliyotokea na mahali mtoto wao alipokuwa, hata kama alikuwa amekufa! Kilichowashangaza hapakuwa na juhudi zozote zilizoonyeshwa na FBI wala polisi ambao walidai tu kuwa ajali hiyo ilikuwa ni ya kawaida, Catarina na Padri Coronel walikuwa wanatafutwa na kama wangepatikana taarifa ingetolewa.
“But you are not doing enough!” (Lakini hamfanyi vya kutosha!) baba yake na Catarina alisema.
“May be you should tell us what is enough!” (Labda utuambie tufanye nini ndiyo itatosha!)
“You know your job!”(Mnajua kazi yenu!)
“Go home and rest, we will let you know the outcome of your daughter’s where about!” (Nenda nyumbani kapumzike, tutakujulisha yatakayoendelea juu ya mahali bintiyo alipo!) Afisa mmoja wa FBI aliwaeleza wakiwa ofisini kwake na kuwaomba wampishe afanye kazi nyingine.
Waliondoka wakiwa wamevunjika moyo kabisa na kwenda kutulia kwenye nyumba waliyokuwa wamepewa na FBI, wiki moja baadaye wakiangalia taarifa ya habari, walishangaa kuona Serikali ya Marekani ilikuwa imekata rufaa katika kesi ya Jackson Motown na tayari yeye na wenzake wote walikuwa wamekamatwa na kuwekwa mahabusu baada ya ushahidi muhimu wa kesi hiyo kupatikana.
“Whaat?”(Niniii?) mama yake Catarina aliuliza.
“This is a miracle”!(Huu ni muujiza!) mume wake akajibu.
“I don’t know what has happened!”(Sijui kilichotokea!) baba yake Kevin aliongea.
“Ijumaa ijayo kesi itaanza kusikilizwa tena mbele ya majaji wanne!”
“Lazima tuhudhurie!”
“Jackson Motown atakuwa anahusika kwa namna fulani na kifo cha Catarina pamoja na Kevin!”
“Hivyo ndivyo ilivyo, ila amekuwa akijaribu kutumia ushawishi alionao kupindisha sheria!”
“Mungu yuko upande wetu!”
Siku nne zilizokuwa mbele yao zilionekana kama miaka minne ili kuifikia hiyo siku ya Ijumaa, lakini kuondoka kwa sekunde moja hadi nyingine kwenye dakika sitini ndani ya saa tisini na sita, hatimaye siku ya Ijumaa ikawadia, walikuwa watu wa kwanza kufika mahakamani ambako walishuhudia majira ya saa mbili kamili asubuhi Jackson Motown akiletwa ndani ya gari la polisi na kushushwa akiwa na wenzake wanne waliotembea wakiwa wameshikiliwa sababu walikuwa ni vipofu.
Wakaingizwa kwenye chumba maalum na baadaye mahakama ilipokuwa tayari waliingizwa kwenye chumba cha kuendeshea kesi, wazazi wa Catarina pamoja na wale wa Kevin walikuwa katikati ya watu wasiopungua mia moja ndani ya chumba hicho, wafuatiliaji wengi wa kesi hiyo walikuwa nje ambako ziliwekwa spika maalum za kuwawezesha kusikia kilichokuwa kikiendelea ndani.
Upande wa mashtaka ndiyo uliopewa nafasi ya kuelezea sababu ya kukata rufaa haraka, watu wote wakiwa kimya, majaji wakiandika maelezo yote kwenye kompyuta zao! Ilimshangaza kila mtu aliyesikia taarifa kwamba mashahidi wawili muhimu walikuwa wamepatikana na walikuwa tayari kusimama katikati ya mahakama hiyo kutoa ushahidi dhidi ya Jackson Motown na wenzake.
“Mashahidi wapo tayari?” Jaji Johnson Macline aliuliza.
“Wapo.”
“Wanaweza kuingia mahakamani mmoja baada ya mwingine tuwasikilize?”
“Ndiyo.”
“Fanyeni hivyo.”
Mlango ukafunguliwa na shahidi wa kwanza akaingia, kilichosikika kutoka katikati ya watu waliokuwa ndani ya mahakama ni sauti ya watu wakipiga kelele kwa nguvu kiasi cha kusababisha mtafaruku na polisi wakalazimika kusogea mahali kelele ilipokuwa ikitokea.
“Mwananguuu! Mbona tulishamzika? Ametoka wapi tena? Ama huu ni mzimu? Keviiiin!” mwanamke alisikika akilia na kusema maneno hayo ambayo hakuna mtu aliyeyaelewa.
“Mamaaa!” shahidi akatoa maneno hayo na kuanza kukimbia akimwelekea mwanamke aliyekuwa akilia, wakakumbatiana na kuanguka sakafuni, jaji alishindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea na kuamuru mahakama iende kwenye mapumziko ya muda wa dakika ishirini kabla ya kuendelea tena.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1
Hadithi iko patamu sana asanteni kwa kutupa raha