×

The Angle of Darkness -61

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.

Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.

Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Baadaye Mashango anafariki dunia baada ya kugongwa na gari na Brianna anachukuliwa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka. Wanatengeneza tukio feki la ujambazi ili ionekane wamevamiwa na Arianna kutekwa na majambazi.

Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya bila mtu yeyote kujua kwamba bado yupo hai, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake. Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Dakika kadhaa baadaye, gari walilopanda lilipaki kwenye hoteli kubwa ya Moven Pick Nairobi, wakateremka na Diego akawaongoza mpaka kwenye bustani nzuri zilizokuwa nje ya hoteli hiyo, wakakaa huku akiwa makini kumtazama yule msichana ambaye muda wote alikuwa akishangaashangaa kila kitu.
“Nataka mniambie binti yangu amefanya nini mpaka mumtafute kwa nguvu namna hii kama mkora!” alisema mke wa Njoroge, Diego akawa anamshangaa kwa nini amuite yule msichana binti yake wakati aliamini hamfahamu.

Mazungumzo yaliendelea lakini yalitawaliwa na hali ya kutoelewana, huyu anazungumza hivi huyu anazungumza kile, ikawa vurumai. Ilibidi Diego aombe kuzungumza na msichana huyo pembeni wakiwa wawili tu.

“Arianna! Hebu niambie ukweli, kwa nini umeamua kunigeuka? Kwa nini umetoroka peke yako na kunipa kazi ya kukutafuta kiasi hiki? Kwa nini umevunja ahadi yetu?”
“Hee! We kaka vipi? Nimeshakwambia kwamba siitwi Arianna wala sielewi chochote unachozungumza.”
“Wewe siyo Arianna kivipi? Una matatizo gani kwani?”

“Mimi naitwa Brianna, sina matatizo yoyote nawashangaa nyie mnaonilazimisha mambo ambayo siyafahamu.”
“Hebu nitazame usoni Arianna, nitazame!” alisema Diego huku akiwa amemkazia macho msichana huyo, akamgeukia na kumtazama, wakawa wanatazamana huku Brianna naye akiwa amemkazia macho Diego.

“Umepatwa na nini mpaka unalikana mpaka jina lako? Arianna kwa nini unanifanyia hivyo?”
“Mimi siyo Arianna, mbona hunielewi? Kama unaendelea kuning’ang’aniza nitaondoka sasa hivi,” alisema msichana huyo huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

“Au umepatwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu? Hebu angalia hizi picha kama unaweza kuikumbuka hata moja,” alisema Diego huku akitoa simu yake na kuanza kumuonesha msichana huyo picha mbalimbali, zikiwemo walizopiga pamoja na nyingine za Msuya na wanaye.
“Siwajui hata mmoja, hata wewe sikujui, sijawahi kukuona hata mara moja maishani mwangu zaidi ya leo.”

“Unaweza kunipa historia yako kwa kifupi?”
“Ndiyo, nilizaliwa hapahapa Mathare, baba yangu simjui lakini mama yangu alifariki nikiwa bado msichana mdogo, nikachukuliwa na familia ya Njoroge ambao ndiyo wamenilea mpaka leo.”
“Umewahi kuishi Tanzania?”

“Sijawahi, nimekwambia nimezaliwa hapahapa na kukulia hapahapa.”
“Mama yako alikuwa anaitwa nani?”
“Mashango.”
“Jina lake la pili?”
“Silijui.”

“Ilikuwaje mpaka akafariki dunia?”
“Aligongwa na gari.”
“Ooh! Maskini, pole sana.”
“Sasa hivi unajishughulisha na nini?”

“Namsaidia mama kuuza genge.”
“Ok, sasa usimwambie mtu yeyote hiki tulichokizungumza hapa. Naomba niongee na mama yako kwanza halafu nitakwambia nini cha kufanya. Mtu akikuita jila la Arianna usiitike wala usikatae, unyamaze tu, sawa?”

“Sijakuelewa, kwa nini nifanye hivyo? Na kuna nini kinachoendelea? Mbona sielewi?”
“Subiri nizungumze na mama yako kwanza halafu nitakufafanulia kila kitu, naomba uwe na amani kwenye moyo wako,” alisema Diego kwa sauti ya chini na kumrudisha msichana huyo mpaka pale walipokuwa wamekaa awali.

Akampa ishara mama wa msichana huyo kwamba wazungumze pembeni, akainuka harakaharaka na kumfuata Diego kwani naye alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea.
“Samahani kwa usumbufu mama, mimi naitwa Diego kutoka Tanzania, eti ni kweli huyu msichana haitwi Arianna? Na wewe umefahamiana naye vipi?” alihoji Diego huku akiwa makini kumtazama mwanamke huyo usoni kubaini kama ambacho angemjibu ni kweli au la!

Mke wa Njoroge alimueleza kila kitu kuhusu msichana huyo, Diego alipokuwa akijaribu kufananisha maelezo ya wote wawili, aligundua kwamba alichokuwa anaelezwa kilikuwa na ukweli kwa asilimia zote.
“Sasa nini kimetokea? Inawezekanaje watu wafanane kiasi hiki? Hebu angalia mwenyewe,” alisema Diego huku akitoa simu yake na kumuonesha mwanamke huyo picha ya Arianna.

“Mungu wangu, mbona wamefanana kiasi hiki? Yaani ni zaidi ya mapacha, kumbe ndiyo maana watu wamemchanganya na binti yangu!” alisema mke wa Njoroge, wakaendelea kuzungumza ambapo Diego alimueleza kila kitu kilichotokea upande wa pili, wakawa wanajadiliana nini cha kufanya.
Kama ilivyokuwa kawaida ya Diego, alikuwa mjanja sana kwenye masuala yanayohusu pesa, akaanza kumshawishi mwanamke huyo akubaliane naye ili kwa pamoja wamtengeneze Arianna feki, kwamba Brianna ajifanye ndiyo Arianna ili akaishi kifahari na Msuya nchini Tanzania.

“Mh! Hilo suala haliwezekani kijana, kwa nini tushiriki kwenye dhambi hii ya uongo wakati ukweli tunaujua? Isitoshe mume wangu ni mtu wa dini, hawezi kuridhia hili suala,” alisema mke wa Njoroge, Diego akaamua kutumia ushawishi wa fedha ili kumlainisha mwanamke huyo ambaye baadaye alimwambia ni bora amkutanishe na mumewe ili wazungumze naye.

“Kwani Brianna umeshaongea naye kuhusu hilo suala?”
“Hapana, sijamwambia chochote nilitaka tuelewane na nyie wazazi kwanza mengine yatafuata.”
Ilibidi warudi mpaka pale walipokuwa wamekaa awali na kumueleza yule mwanaume aliyekuwa wa kwanza kumtambua msichana huyo kwamba huyo hakuwa Arianna wanayemtafuta bali mtu mwingine ambaye wamefanana naye.

“Haiwezekani, mnataka kunitapeli, nipeni zawadi yangu,” alisema mwanaume huyo, ikabidi mke wa Njoroge na Diego waanze kumfafanulia kwa kina, kwa shingo upande akakubali kuondoka hasa baada ya kupewa fedha na Diego kwa ajili ya usumbufu.

Alipoondoka, waliongozana mpaka nyumbani kwa Njoroge ambapo mazungumzo mazito yalianza kufanyika. Haikuwa rahisi kwa familia hiyo kukubaliana na kilichokuwa kinazungumzwa na Diego lakini alipoingizia suala la kiwango cha fedha ambacho wangekipata, ukichanganya na maisha ya dhiki waliyokuwa wanaishi, Njoroge na mkewe walijikuta wakibaki njia panda.

“Kwa hiyo wewe ulikuwa unasemaje baba?”
“Kama tumekubaliana, nampigia simu Msuya na kumwambia tumempata Arianna, mambo mengine yote niachieni mimi.”

“Na wewe Brianna unasemaje?”
Je, nini kitafuatia? Brianna atakubali? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

2 Comments

Leave a Comment