Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.
Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Baadaye Mashango anafariki dunia baada ya kugongwa na gari na Brianna anachukuliwa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge.Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka. Wanatengeneza tukio feki la ujambazi ili ionekane wamevamiwa na Arianna kutekwa na majambazi.
Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya bila mtu yeyote kujua kwamba bado yupo hai, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna na Diego anashiriki kuandaa mpango wa kumuaminisha Msuya kwamba huyo ndiye Arianna na tayari amefika nyumbani kwa Msuya lakini matendo yake yanazua maswali mengi kwa mumewe.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Macho ya Msuya yakatua kwenye kifua cha msichana huyo, akaona kitu ambacho kilimshtua sana moyo wake, mapigo ya moyo yakawa yanamuenda mbio mithili ya fisi aliyeona mfupa, akameza funda la mate.
“Arianna!”
“Abee!”
“Nakupenda sana mke wangu, licha ya matatizo yaliyokupata lakini naona kama umezidi kuwa mrembo, nakupenda sana,” alisema Msuya kwa hisia na kabla msichana huyo hajajibu chochote, tayari alikuwa amemkumbatia kimahaba huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida.
Kama ilivyokuwa mwanzo, msichana huyo alimtoa kifuani kwake na kurudi nyuma huku akionesha kutokuwa sawa kihisia.
“Ooh! Samahani mke wangu, ujue nakuwa najisahau kila mara, samahani,” alisema Msuya na kwenda kukaa pembeni, akawa anamuongelesha mwanamke huyo mambo mbalimbali lakini hakuwa akimchangamkia kama ilivyokuwa kawaida yake, akaendelea kuamini kwamba msichana huyo amepatwa na matatizo makubwa ya kisaikolojia ndiyo maana alikuwa kwenye hali hiyo.
Kwa Brianna, huo ulikuwa wakati mgumu sana kwenye maisha yake. Ni kweli alichoshwa na maisha ya ufukara aliyokuwa anaishi na familia ya mzee Njoroge iliyomlea lakini alipata kazi kubwa kuigiza maisha ambayo hayakuwa yake.
Kila alichokuwa anakifanya, alikuwa anajua kwamba anakosea kwani afadhali kama angekuwa anamjua huyo Arianna na angalau angemuona jinsi alivyo na mambo aliyokuwa anayafanya. Kila kitu kilikuwa usiku wa giza kwake, akawa anamuomba Mungu wake amvushe kwenye kipindi hicho kigumu alichokuwa anapitia.
Mtihani mwingine kwake, ilikuwa ni kuhusu kukutana kimwili na Msuya. Katika maisha yake hakuwa anamjua mwanaume kwa hiyo kama angemruhusu, Msuya ndiyo angekuwa wa kwanza lakini mbaya zaidi, lazima angemgundua kwamba hakuwa Arianna kwa sababu kama ni mkewe, lazima walikuwa wakishiriki tendo la ndoa.
Uamuzi alioamua kuuchukua, ni kuendelea kumkwepa Msuya mpaka mwisho, hakujua nini itakuwa hatima yake atakapoujua ukweli. Upande mwingine wa nafsi yake ulikuwa ukimsuta kwa kukubali kirahisi kutimiza matakwa ya Diego, hata hivyo alipofikiria kwamba familia ya Njoroge tayari ilikuwa imeondokana na shida na ufukara ulioitesa kwa kipindi kirefu, aliamua kupiga moyo konde.
“Liwalo na liwe!” alijisemea Arianna moyoni huku akishusha pumzi ndefu. Muda mfupi baadaye, chakula kilikuwa tayari, Msuya akawataka wafanyakazi wake wapeleke chakula chake na mkewe chumbani kwani alihitaji muda zaidi wa kuwa wawili.
Muda mfupi baadaye, chakula kilipelekwa chumbani ambapo Msuya alimkaribisha mkewe, wakakaa kwenye meza ndogo iliyokuwa chumbani na kuanza kula. Tofauti na alivyotegemea kwamba msichana huyo angekifurahia sana chakula hicho kwa sababu huwa anakipenda, walipoanza kula, alishangaa akila kama ndiyo mara yake ya kwanza kula.
“Vipi mbona unakula kwa kusuasua tofauti na siku zote? Halafu mbona huweki pilipili nyingi kama kawaida yako?” alihoji Msuya lakini Brianna akakosa cha kujibu zaidi ya kusingizia kwamba hakuwa akijisikia vizuri.
Japokuwa kilikuwa ni chakula kizuri sana, kwa Brianna kilikuwa kigeni kabisa.
Alishazoea kula vyakula vya kuchemsha na mboga chukuchuku lakini siku hiyo, kila kitu kilikuwa ni cha kurosti, kikiwa na viungo vingi ambavyo hakuwahi hata kuviona. Kadiri alivyokuwa anazidi kula, ndivyo alivyokuwa anazidi kunogewa na chakula hicho.
Ikafika mahali, akawa anakula kwa uroho na kumfanya Msuya azidi kumshangaa ingawa moyoni alifurahi kuona anakula. Aliendelea kula mpaka akamaliza chakula chote, akawa anadai maji ya kunywa ambapo Msuya aliinuka na kwenda kumletea, akanywa kwa wingi.
“Nimefurahi sana mke wangu umekula,” alisema Msuya, akamuita mfanyakazi atoe vyombo ambapo naye alishangaa kwani haikuwa kawaida ya Arianna kula chakula chote na kumaliza, akatazamana na Msuya na wote wakatabasamu.
Baada ya kumaliza kutoa vyombo na kusafisha, mfanyakazi huyo alitoka na kuwaacha wawili hao chumbani, Msuya akawa anaendelea kumsemesha mambo mbalimbali lakini msichana huyo alikuwa mbali kimawazo, mara akapitiwa na usingizi akiwa palepale alipokuwa amekaa wakati akila.
Msuya aliinuka na kuandaa kitanda vizuri, akaenda kumuinua akiwa hajielewi kwa usingizi na kwenda kumlaza kitandani, akamfunika vizuri kisha na yeye akaenda kuoga na kurudi kulala. Kama alivyozoea kwa mkewe, Msuya alimkumbatia msichana huyo na kuendelea kumshukuru Mungu wake kwa kumnusuru. Baadaye na yeye alipitiwa na usingizi kutokana na uchovu wa pilikapilika za kutwa nzima.
Brianna ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzinduka alfajiri na kujikuta akiwa amelala huku amekumbatiwa na Msuya, harakaharaka akajitoa kwenye mikono yake na kukimbilia bafuni, akapeleka mkono kwenye ‘ikulu’ yake kwani hakujua Msuya amemfanya nini baada ya kupitiwa na usingizi.
Alipogundua kwamba alikuwa salama, alishusha pumzi ndefu na kurudi chumbani, akamkuta Msuya akiwa amekaa kitandani.
“Vipi? Mbona umekurupuka kiasi hicho?”
“Nimeota ndoto mbaya,” alijibu Brianna kwa kifupi, Msuya akamtaka arudi kitandani waendelee kulala lakini alikataa na kusema kuwa tayari kumeshapambazuka anataka kuanza kufanya usafi.
Kauli hiyo ilimshangaza zaidi Msuya kwani haikuwa kawaida ya Arianna kuwahi kuamka kiasi hicho, akiwa bado anaendelea kujiuliza, msichana huyo alianza kupiga deki chumbani humo, jambo ambalo pia halikuwa kawaida kwa Arianna.
“Mke wangu, hebu njoo kwanza, mbona kama sikueleweelewi!” alisema Msuya huku naye akiamka.
“Ngoja kwanza nifanye usafi nitakuja tuongee,” alisema msichana huyo huku akiendelea na kazi. Alisafisha chumba chote, akahamia upande wa choo na bafu ambako nako alifanya usafi wa nguvu. Alipomaliza alihamia kwenye ngazi, akasafisha na kushuka hadi kwenye sebule kubwa. Akafanya usafi kila sehemu na kuhakikisha kila kitu kinakaa mahali pake.
Mpaka wafanyakazi wa Msuya wanaamka kwa ajili ya kufanya usafi kama kawaida yao, Brianna alikuwa amemaliza karibu kila sehemu, nao wakabaki wamepigwa na butwaa kwani haikuwa kawaida ya bosi wao huyo kuwa mchapakazi kiasi hicho.
Wakawa wanaangaliana, wakiwa hawana majibu. Kwa muda wote huo, Msuya alikuwa makini kuendelea kumfuatilia mkewe kila alichokuwa anakifanya.
Akabaki na mshangao mkubwa kwani huyo hakuwa Arianna anayemjua yeye, akawa anajiuliza moyo wa uchapakazi na usafi wa kiwango hicho ameupata wapi? Hakuwa na majibu zaidi ya kuzidi kumpenda.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1