ILIPOISHIA…
WAKATI Jamal amekwishazama kwenye penzi la msichana aliyemwokoa asiliwe na Simba kwenye hifadhi ya American National Park; Catarina, ambaye hivi sasa ni mjamzito akitegemea kupata mtoto, anapata mgeni ofisini kwake ambaye amejitambulisha kwa jina la Kevin na kumsimulia Jamal lengo la safari yake hapo kwamba ni kumtafuta mchumba wake aitwaye Catarina, ambaye inaaminika alitupwa mbugani na wauaji ili afe kwa kuliwa na wanyama wakali.
Jamal ameshtuka, kwani msichana anayetafutwa ndiye aliyenaye ndani ya nyumba yake, maelezo ya Kevin badala ya kumfurahisha yanamtia hasira, anahema kwa nguvu na jasho jembamba linamtoka, huku akisubiri Kevin amalizie kuelezea historia yake ndipo ajue la kufanya.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…
KEVIN alipomaliza kusimulia, Jamal akaachia tabasamu kama vile alikuwa amefurahishwa sana na habari aliyokuwa ameisikia, kumbe maumivu aliyokuwa nayo moyoni mwake yalikuwa makubwa mno! Hakika ujio wa Kevin ulikuwa hatari kubwa katika maisha yake na Catarina ambaye kwa wakati huo hakuwa tu mpenzi, bali mke ambaye walikuwa pamoja wakisubiri kuhalalisha tu ndoa yao.
“Ooh! Kumbe ni wewe? Nilisoma habari za mtu huyo mtandaoni kwamba alikuwa marehemu na alizikwa kwao huko Afrika, sijui nchi gani vile?”
“Tanzania!”
“Ah! Ndiyo, Tanzania, sasa inakuwaje tena upo hai?”
“Sikufa, ule ulikuwa ni mchezo ambao mzee mmoja aitwaye Thomas Edmund aliamua kuufanya kwa ajili ya usalama wangu.”
“Kweli ni wewe?” Jamal aliuliza tena.
“Kabisa, naomba tu Meneja unisaidie kunitembeza ndani ya hifadhi mpaka nifanikiwe kupata mabaki yake kama kweli alikufa na kama yuko hai, basi nimchukue twende zetu Afrika tukafunge ndoa na kuendelea na maisha yetu, huo ndio ukweli!” Kevin aliendelea kujieleza bila kufahamu maneno aliyokuwa akiyatoa yalikuwa mkuki moyoni mwa Jamal.
Jamal aliinamisha kichwa chake akiwaza, hakuwa tayari kabisa kumwachia Catarina aondoke, tena ukizingatia wakati huo tayari alikuwa mjamzito wa mtoto wake wa kwanza! Halikuwa jambo rahisi hata kidogo kuruhusu Catarina na Kevin wakutane, mara kadhaa alishagundua kutokana na maongezi yake na Catarina kuwa sehemu fulani ya moyo wake ilikuwa bado iko kwa Kevin pamoja na kuwa naye, kilichothibitisha zaidi mawazo hayo ni ndoto za mara kwa mara za Catarina akiita jina Kevin.
“Ni heri angekuwa hana mimba yangu, ningeweza kufikiria kuwakutanisha, kwa sasa haiwezekani!” aliwaza Jamal akiwa kimya, tayari machozi yalikuwa yakipenya kwenye kona za macho yake na kutiririka kuelekea mashavuni hadi kidevuni.
“Pole! Inavyoonekana historia niliyokuelezea imekugusa sana!”
“Mno! Nimekuonea huruma, sasa itabidi nikupatie chumba kwenye hosteli yetu iliyoko hapo nje, utalala hapa mpaka siku ya kesho, nijipange kwa ajili ya safari ya kuelekea hifadhini, nimeamua kukusaidia ili umpate Catarina wako!”
“Ahsante sana, Mungu akubariki, sikutegemea kukutana na mtu mwema kama wewe!” alisema Kevin akinyanyuka na kumkumbatia Jamal aliyekuwa akijifuta machozi kwa kitambaa, moyo wake ulikuwa katika maumivu makali mno, hisia za kunyang’anywa Catarina zilikuwa zikimsumbua.
Kevin alichukuliwa na Jamal na kuongozwa hadi nje ya jengo la utawala wa hifadhi, wakazunguka nyuma ambako kulikuwa na hosteli za wageni, wafanyakazi wakampokea begi lake na kumwonyesha chumba kimoja kizuri kilichokuwa na kiyoyozi pamoja na sehemu ya kuongezea joto chumbani wakati wa baridi.
“Kitakufaa?” Jamal aliuliza.
“Kinafaa sana rafiki yangu, cha muhimu ni Catarina!”
“Hiyo kesho, jiandae tu kwa safari!”
“Niko tayari.” Kevin alijibu akionyesha furaha yake waziwazi.
Jioni ya siku hiyo Jamal alirejea nyumbani akiwa hana raha kabisa, hali iliyomshangaza sana Catarina aliyemzoea kama mtu mchangamfu aliyefanya nyumba ifae kuishi. Akamsogelea na kuketi kando yake akijaribu kumdadisi ni kitu gani kilikuwa kimetokea kazini kwake siku hiyo.
“Hapana tatizo kabisa, ila kesho nitalazimika kusafiri kidogo kwenda mbugani, kuna mtalii nitakwenda kumwonyesha sehemu fulani ambako wanyama hupatikana wakati wa usiku tu!”
“Hakuna shida, hilo ndilo limekufanya usiwe na amani?”
“Limechangia kwani sitaki kuwa mbali na wewe hasa katika kipindi hiki cha ujauzito wako.”
“Si utarudi?”
“Nitarudi lakini usiku.”
“Hakuna shida.”
Pamoja na mazungumzo hayo, Jamal hakupata usingizi usiku huo mpaka asubuhi alipoamka na kujiandaa kwa ajili ya kwenda ofisini, huko alifanya kazi zake vizuri mpaka jioni ndipo akaondoka kwenda hosteli kumpitia Kevin kwa ajili ya safari, alikuwa na kila kitu kwenye gari lake ikiwa ni pamoja na bunduki ya kujilindia aina ya SMG.
“Nimekupitia twende!” alisema baada ya kuingia chumbani kwa Kevin.
“Nashukuru sana, salama lakini?”
“Mimi sijambo kabisa!”
“Familia?”
“Mh naishi peke yangu!”
Kevin akapakia begi lake ndani ya gari, wote wakaingia, Jamal akiwa kwenye usukani na gari kuanza kuendeshwa kutoka kwenye lango la kuingilia ndani ya hifadhi na kuendeshwa kwa saa tatu, giza likiwa limeingia, mara kadhaa Kevin alimwambia Jamal asimamishe gari ili kama Catarina alitupwa maeneo hayo waweze kuyaona mabaki yake.
“Hapana, najua sehemu ambayo wanaweza kuwa wamemtupa!”
“Wapi?”
“Tulia nikupeleke mimi ndiyo mwenyeji wako.”
“Ahsante, twende.”
Safari ikazidi kuendelea, mpaka saa nne na nusu usiku ndipo gari likasimamishwa kando ya bwawa kubwa la maji, mbalamwezi ilikuwa ikipita angani na kusaidia kupunguza giza, hapa ndipo mahali ambako wanaweza kuwa wamekuja kumtupa, wahalifu wengi hutupa watu maeneo haya.”
“Sasa?”
“Chukua tochi hii hapa!”
“Nishuke?”
“Shuka tu uanze kumulika huku na kule, namalizia kuongea na simu moja hapa halafu nitaungana na wewe!”
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1