×

Jumanne MheroNgoma: Mvumbuzi wa Tanzanite-2

tanzanittmann_87929

Baada ya kuibiwa jiwe lake hilo la Tanzanite, akili ya Ngoma ilifanya kazi haraka na akaamua kwenda kupata leseni ya umiliki wa eneo ambako aliyapata madini yale.

Akapewa viwanja nane kwenye eneo lile la Lalouo ambako alilipia kiasi cha Sh. 15 kwa kila kimoja. Akaweka alama zote muhimu na kuamini kwamba lile ni eneo lake halali kisheria na mara wakati utakapofika, ataanza kuchimba madini hayo.

“Februari mwaka 1968, nikaenda kutembelea kwenye eneo lile. Nikamkuta kijana mmoja akiwa anachimba madini hayo kwenye eneo langu. Alikuwa ameyajaza kwenye ndoo.
“Nikamwambia kwa nini amechimba madini hayo kwenye eneo langu? Akanijibu kwamba lile si eneo langu bali ni la mtu mmoja aitwaye De Souza . Nikamwonesha alama zangu zote nilizoweka pamoja na nyaraka nilizokuwa nazo.
“Nilipoenda kushitaki polisi kuhusu huyu mtu anayeitwa De Souza, nikaambiwa ataitwa na atafika Jumatatu. Bila ya taarifa, kumbe huyo bwana akaja Jumamosi na akazungumza na polisi mapema.

“Mkuu wa polisi kwenye eneo letu alikuwa akifahamika kwa jina la Kitenge akaniita polisi na akaniambia ameamua kumpa De Souza vitalu (viwanja) vinne kati ya nane nilivyokuwa navimiliki.
“Sasa mimi nikabaki nimeshangaa, inakuaje mtu anapewa vitalu vyangu. Lakini afande Kitenge akasema ama nikubali hivyo au nitanyang’anywa vyote. Nikakasirika sana na nikasusa kabisa. Sikurudi tena kule kwenye machimbo. Nikaenda kufanya biashara zangu,” anasema mzee Ngoma.
Mzee Ngoma anamtaja De Souza kabila la Goa, mzaliwa wa India alikuja nchini Tanganyika mwaka 1933 akiwa na umri wa miaka 20.

Taarifa katika mitandao mbalimbali duniani inamtaja yeye kama mvumbuzi wa Tanzanite. Kwamba Julai 1967, kundi la Wamasai, lilimpeleka Goa huyo kwenye eneo ambako aligundua madini hayo.
Kwenye mtandao unaoheshimika zaidi duniani wa Wikipedia unamtaja, Emmanuel Merishiek Mollel, unadai ndiye aliyempa De Souza madini hayo na yeye akayapeleka kwa wataalam ambao waliyabaini kwamba ni Tanzanite.
Historia inapindishwa kusudi ili mzee Ngoma akose hadhi na heshima anayostahili!
Mwaka 1984, serikali ilimtaja rasmi mzee Ngoma kama mvumbuzi wa madini hayo ikampa zawadi ya ngao,  cheti na fedha taslim Sh. 50,000. Pia hayati mzee Rashid Kawawa alimzawadia Sh 50,000!
Alipoulizwa na mwandishi mmoja anataka nini kutoka serikalini anajibu; “Sihitaji mambo makubwa sana. Ninachohitaji ni kuishi maisha yanayofanana na Tanzanite. Nataka mtu akiniona mimi aone Tanzanite,” anasema. Ni ombi ambalo linanisisimua, Serikali ya Magufuli imuangalie kwa jicho la tatu mzee huyu.

Mzee Jumanne Mhero Ngoma, alizaliwa mwaka 1939 katika Kijiji cha Marwa, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Wazazi wake walikuwa wafugaji wa ng’ombe na mbuzi hivyo waliishi maisha ya kuhamahama ili kupata malisho bora ya mifugo kama ilivyo hulka na tabia za wafugaji.
Wakati akiendelea na shule ya msingi,  mwaka 1952 wazazi wake walihama kutoka Hedaru na kwenda kuishi Mererani, Arusha. Mzee Ngoma, aliweza kusafiri na wazazi wake hadi Mererani akaendelea na masomo yake katika shule iliyokuwa ikiitwa Town School, Arusha mjini, ambako ilibidi akae na mjomba wake, Ruben Mkali aliyekuwa akiishi Arusha wakati huo.

Mwaka 1965, alifunga ndoa na Bi Fatma Mauya na kupata watoto nane.
Mzee Jumanne Ngoma alijiunga na kozi fupi ya madini iliyokuwa ikitolewa na Wizara ya Madini wakati huo, katika ofisi ya madini Morogoro, Juni 1, 1966 alipata leseni ya utafiti wa madini baada ya kuhitimu mafunzo hayo kisha alirejea nyumbani kwake Makanya.
Serikali inapaswa kuwaenzi watu kama akina mzee Ngoma kwani simulizi zao zitafanya watu wajenge akili ya kuhoji kila wanachokiona na watachochea watu wawe wagunduzi.

Leave a Comment