×

Huoni haya kujisevia mume wa shoga yako?

Asalam alaikum wapenzi wasomaji wa safu hii, naamini mko salama, kwa wenye matatizo poleni, kwa walioachika nawashangaa kwa nini uachike wakati wewe mwanamke kama mwingine? Mlioachika mlichukue hilo.

Leo nimekuja na mada ya kuwasema akina mama wanaojirahisisha kwa wanaume wa marafiki zao, hivi inakuwaje unajisevia mume wa rafiki yako wakati ukijua maana ya urafiki? Au hamjui maana ya urafiki wanawake wenzangu? Rafiki anaweza kuwa zaidi ya ndugu uliyezaliwa naye tumbo moja.

Kuna msomaji wangu amenitumia ujumbe mfupi akinieleza kuwa anahisi mumewe anatoka na rafiki yake kipenzi, nikamuuliza kwa nini unamhisi na huna uaminifu kwao? Akaniambia kuwa sababu kuu ni mambo wanayoongea kuyakuta kwa mumewe kitendo ambacho kinamshangaza.

“Siku moja kuna kitu nilimshirikisha ambacho hakuna mtu aliyekuwa akikijua ni mimi na yeye, lakini cha kushangaza nilikikuta kwa mume wangu tena siku hiyo alinipa kipigo cha maana, lakini nilipombana alitoa habari hizo wapi alikataa kuniambia, moja kwa moja nikajua ni rafiki yangu na unadhani walianzia wapi mpaka akamwambia itakuwa ni mapenzi tu!”
Msomaji huyo tuliongea mengi lakini kwa haya niliyokupa hapa ndiyo chanzo cha kuandika mada hii, mwanamke mwenzangu nikufunze kabla ya kumchukua mume wa shoga yako, unatakiwa kwanza kumfikiria mwenzako na ndoa yake, kumbuka kila unalomtendea mwenzako huwa linarudi kwa njia nyingine.

Wengi huingia na tamaa ya lile penzi na mahaba anayopewa na mwenzake huku wakati mwingine huingia tamaa ya mali au fedha alizonazo jamaa, hivi unapoamua kufanya kwa sababu ya tamaa, huoni kuwa mwisho wako ni mbaya?
Kwanza unatakiwa kujiuliza, huyu ninayeingilia penzi lake amevumilia mangapi kisha na mimi nijiingize lakini pia umejiuliza zile pesa zinazokupa tamaa anazipata wapi au unaamua kwa sababu ya pesa tu, je kama anaiba na mkewe anajua toka siku nyingi wamekubaliana kufichiana siri.. hapa ndiyo unaambiwa kabla ya kuamua kutenda jambo fikiria kwanza.

Mwanamke unayeamua kumchukua mume wa shoga yako, nakuona kama mwanga unayeweza kumfanyia lolote mwenzako kwa sababu mwanzo wa kumtenda hayo ndiyo mwanzo wa kutafutana ubaya.
Ni kweli utakuwa umekosa mwanaume wa kutembea naye mpaka utoke na shemeji yako? Kwa nini usivumilie, kweli wapo wanaume wanaoshawishi lakini kwa nini usijikaze? Na ili ufanikiwe huyo shemejio muone kama kaka yako.
Hivi hujiulizi rafiki yako akigundua atakuchukuliaje? Kama utashindwa kujiuliza na kuamua kutoka na shemeji yako hapo ndipo nathubutu kukuita mwanga unayeweza kufanya lolote ili ukae kwenye imaya ya mwenzako

Leave a Comment