Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale akina Bite na Monica walipoamka baada ya kusikia Dorcas akilia na kumkuta mama yao akimuadhibu, walipomuuliza aliwaambia alikuwa jeuri sana. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na mkasa huu unaoelekea tamati.
Wakati akinizushia uongo huo nilifanikiwa kuvaa sketi yangu na kuzidi kumuomba msamaha mama japo sikuwa na kosa, lengo langu lilikuwa anisamehe ili aache kunishambulia.
“Bahati yako umelitambua kosa lako, ukirudia tena nitakufukuza hapa nyumbani kwangu,” mama aliniambia.
Nafsi yake iliporidhika, alimwambia Bite aende akachukue fedha anikabidhi ili niende sokoni nikanunue mboga na viungo.
“Muone kwanza, hebu kamalizie chai yako ila usirudie tena upuuzi wako wa kuamua kunywa chai bila kupewa maelezo na wenye nyumba,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.
Nikiwa sina amani, licha ya kujongea pale mezani nilishindwa kunywa chai nikabaki nimejiinamia na kumkumbuka marehemu mama.
“Hivi kama mama na baba yangu wangekuwepo sidhani kama ningepitia mateso haya, hivi ni lini nitaishi kwa amani kama watu wengine, lini nami nitakuwa na furaha hapa duniani?” niliwaza.
Wakati nawaza hivyo, mama aliniambia kama sikuhitaji kunywa chai niende sokoni nikanunue mboga kisha nipike ili wasijechelewa kula.
Niliinuka na kuelekea chumbani kwa lengo la kubadili siketi na kujiweka sawa, nilipoingia niliwakuta Monica na Bite wakiwa wameketi kitandani ndipo Bite akaniambia nisimfanyie ujeuri mama yao.
“Dorcas, unaona huo ujeuri wako umesababisha mama akuchape makofi na kama hutajirekebisha anaweza hata kukufukuza hapa nyumbani,” Dorcas anasema Bite alimwambia bila kujua sababu ya mama yao kumchapa.
Aliponiambia hivyo, sikumjibu chochote, nilibadili nguo nikaenda jikoni nilikochukuwa kikapu na kuelekea sokoni.
Niliporejea nikatakata nyama na kuiinjika jikoni, wakati huo akina Bite walikuwa wanajiandaa ili waende mjini. Walipokunywa chai waliacha vyombo walivyonywea mezani kisha wakaondoka.
Kwa kuwa niliwazoea, nilivikusanya na kwenda kuviosha huku nikiwa nina msongo wa mawazo. Kufuatia hali hiyo nilisahau kama nilikuwa nimeinjika nyama.
Aliyenishtua alikuwa Barton aliyenifuata na kuniambia nyama ilikuwa ikiungua nikatoka mbio kwenda jikoni na kukuta sehemu kubwa ikiwa imeungua na harufu ikiwa imetanda jiko zima.
Nilichofanya ni kuipua lakini kabla sijafanya chochote mama aliyesikia harufu ya nyama kuungua aliingia, kama alivyofanya asubuhi alijishika kiunoni na kuniuliza nilikuwa nimefanya nini!
Kwa hofu nilishindwa kumjibu ndipo akaniuliza nilifanya nini nikamwomba msamaha kwa kuunguza nyama kwa bahati mbaya, akatoka mle jikoni. Moja kwa moja nilijua anakwenda kufuata fimbo.
Kabla hata sijachukua hatua ya kutoka nje aliingia akiwa amefura kwa hasira, kabla hajaanza kunitandika nilipiga magoti na kumwomba msamaha kwamba nyama iliungua kwa bahati mbaya hakunielewa, alinitandika bakora ya mgongoni.
Baada ya kunitandika, alinyanyua tena fimbo ili anichape begani nikakinga mkono, hapo nikawa nimemuongeza hasira akaniambia kumbe nilikuwa najua kukinga fimbo yake!
Alipotoa kauli hiyo alinizaba kibao cha nguvu upande wa kushoto nilipojishika kufuatia maumivu niliyopata alinizaba tena kibao upande wa kulia, nikasikia masikio yakivuma.
Mama aliniambia hapendi kuishi na mtu jeuri akaitupa fimbo chini, akaniambia nitafute fedha zangu nikanunue nyama nyingine. Kwa kuwa sikuwa na fedha niliomuomba msamaha, akanisonya.
“Kumbe unajua kuunguza tu wakati huna hata hela mjinga wewe, hivi huko ulikotoka ulikuwa unakula nyama?” mama alinikebehi.
Wakati akinikehi hivyo, bado masikio yalikuwa yakivuma, alichokifanya alimtuma Bite akanunue nyama.
Siku hiyo nilikosa raha kutokana na maumivu ya kipigo, nilipokula nilishindwa kufanya kazi yoyote nikaingia chumbani kulala. Kufuatia kipigo kutoka kwa mama, nilipoteza uwezo wa kusikia vizuri, kutokana na makofi aliyonipiga masikioni. Nilipomwambia mama akanieleza nimuondolee upuuzi wangu na kusema kama sikusikia vizuri yeye afanyeje!
Je, kilifuatia nini? Usikose sehemu ya mwisho wiki ijayo.
Maoni tumia namba hiyo juu.