ILI kulinusuru penzi lake na Catarina, Jamal anampeleka Kevin porini na kumwacha huko akiamini kwamba lazima angeliwa na wanyama wakali, anarejea nyumbani kwake alfajiri na kuingia ndani ambako anamkuta mkewe Catarina ameketi akimsubiri, wanasalimiana na baada ya salamu anavua nguo zake chafu kisha kuingia bafuni ambako alioga kwa dakika kumi tu na kutoka, akajifuta maji kwa taulo kisha kujitupa kitandani, nusu saa tu baadaye alikuwa akikoroma! Saa mbili kamili, Catarina alichungulia kupitia dirishani analiona gari likiwa katika hali ya uchafu kupindukia anaamua kutoka nje na kuliosha, hakuogopa sana sababu angekuwa ndani ya ngome ya nyumba yao, watu wasingemwona.
Wakati analiosha gari hilo kwa kutumia mpira wa maji, macho yake yalitua ndani ya gari kiti cha nyuma na kuliona begi ambalo tangu aishi na Jamal hakuwahi kuliona, akaufungua mlango na kulisogeza karibu yake, moyo ukamtuma kufungua ndani ili aone kulikuwa na nini, macho yake yakakutana na nguo lakini pia kulikuwa na kitabu cha kuandika kumbukumbu, ambacho Waingereza hukiita Diary.
Alikichukua kitabu hicho na kukisoma juu yake, kiliandikwa; Kitabu cha Kutunzia kumbukumbu ambamo matukio muhimu katika kumtafuta mpenzi wangu Catarina hutunzwa! Moyo wake ukalipuka, mapigo kadhaa yakarukwa, jasho jingi likamtoka, akatamani kufungua ndani asome kilichoandikwa.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…
NGUVU za miguu zilimwishia, hakuweza kusimama tena, moyo wake ulikuwa umejaa uchungu baada ya kugundua Kevin alikuwa amekutana na Jamal na hisia zake zilimtuma kuamini baada ya mazungumzo yao akimwongelea yeye Catarina, jinsi alivyompenda, Jamal alikasirika, akahisi angenyang’anywa mwanamke aliyempenda na mama wa mtoto wake, hivyo akaamu kumuua.
“Safari yake ilikuwa ya ghafla mno na alionekana kabisa amevurugikiwa kichwani, inawezekana sababu ya yote haya alikuwa ni Kevin, masikini, atakuwa amemuua bila hatia, nampenda Kevin, ingawa pia nampenda Jamal! Watu hawa wote ni muhimu katika maisha yangu, waliniokoa.” Catarina aliwaza akielekea kwenye msingi wa nyumba ambako aliketi na kuanza kukifungua kitabu cha kutunzia kumbukumbu cha Kevin.
Kwenye ukurasa wa kwanza tu alikutana na maneno; Maisha yangu hatayakuwa sawa tena, mpaka siku nitakapompata Catarina, nampenda Catarina, nisipompata ni bora kufa, nitamtafuta popote duniani mpaka nimpate! Ulikuwa ni mwandiko wa Kevin.
Kumbukumbu zake zote zilimrejesha nchini Tanzania, maisha aliyoishi na wazazi wake, mateso aliyoyapata kwa ugonjwa wa saratani ya damu ambao Kevin ndiye aliyemwokoa, jinsi walivyopendana na kuahidiana kuoana! Akajilaumu kwa uamuzi wake wa kufuata mambo ya uanamitindo ambayo hatimaye yalikuja kuvuruga hatima yake.
Machozi yalikuwa yakimbubujika, alikuwa hataki kabisa kuamini kama kweli Jamal, mwanaume mpole, mnyenyekevu, anayejua kupenda na kudekeza mwanamke alikuwa amekutana na Kevin na kuamua kwenda porini kumuua! Ilikuwa ni lazima alifahamu jambo hilo kabla hajaanza kuhukumu.
“Pengine walisafiri wote bila Jamal kufahamu kuwa huyo Kevin ndiye amewahi kuwa mchumba wangu, wamerejea wote na begi la Kevin akaamua kuliachana ndani ya gari, hebu ngoja kwanza nisome kilichoandikwa humu ndani…” alijisemea na kuendelea kufunua;
… nimekutana na msichana aitwaye Mariana, huyu amenipeleka nyumbani kwake.
…ametokea kuwa rafiki yangu mkubwa, ameahidi kunisaidia kukutana na Jackson Motown,
…Nimetekwa,
…Nimewamwagia tindikali wote na kufanikiwa kutoroka,
…nipo ndani ya nyumba ya Thomas Edmund,
…Nyumba imelipuliwa,
…nimekwenda kufichwa nyumbani kwa mke wa Thomas Edmund,
…Kesi inaanza mahakamani, Jackson Motown na wenzake wanashtakiwa,
…Natoa ushahidi,
…Kaibuka mtu aitwaye Dracula na kumpiga risasi Motown mahakamani, yeye pia kapigwa,
…Amepona na ametoa ushahidi,
…Amesema hawakumuua Catarina,
…Walimtupa kwenye hifadhi ya American National Park ili aliwe na wanyama wakali,
…Dracula, Dragon na wenzake wamehukumiwa kifo kwa kudungwa sindano ya sumu,
…Ni shangwe, sasa naanza kazi ya kumtafuta Catarina.
…Nimeamua kwenda kwenye hifadhi, nitazunguka hifadhi yote nikitafuta mifupa yake,
…Nimekutana na kijana mpole, Jamal, meneja wa hifadhi hii nimemweleza kila kitu juu ya mpenzi wangu na ameahidi kunizungusha mbugani nimtafute, ni mtu mwema!
…Leo jioni siku ya Jumamosi ananipeleka mbugani,
…Tuko ndani ya gari tunaelekea huko, naamini Catarina wangu yupo hai, kama amekufa basi niipate hata mifupa yake tu, itatosha kuutuliza moyo wangu.
Hayo ndiyo maneno ya mwisho ambayo Kevin aliandika kwenye kitabu hicho na kuthibitisha kabisa wasiwasi ambao Catarina alikuwa nao moyoni mwake, kwamba Jamal alikutana na Kevin na kumweleza lengo la safari yake, sababu ya mapenzi ambayo Jamal alikuwa nayo kwake hakuwa tayari wakutane hivyo akaamua kwenda kumuua katika ya hifadhi ili tu wasikutane.
Mashavu yake yote yalikuwa yamelowa machozi, hasira dhidi ya Jamal ghafla ilikuwa imempanda, akanyanyuka na kuanza kutembea kuingia ndani moja kwa moja hadi chumbani na kuanza kumtingisha Jamal kwa nguvu zake zote ili aamke! Mwili wake wote ulikuwa ukitetemeka.
“Amka! Amkaaaa! Amka Jamal!”
“Vipi tena mpenzi umekuwaje?”
“Nataka uniambie ulikompeleka Kevin.”
“Kevin?”
“Ndiyo, unabisha nini, angalia hiki kitabu au nikuletee kabisa na begi lake?” aliuliza Catarina akitembea kuelekea nje ambako alilibeba begi na kurudi ndani, akalibwaga mbele ya Jamal.
“Yuko wapi?” aliuliza tena.
“Tulia kwanza!”
“Siwezi kutulia, nataka nijue mahali alipo!”
“Unanipenda Catarina?”
“Ndiyo nakupenda, lakini niambie mahali aliko Kevin, si kwamba nitaondoka, nitabaki na wewe milele lakini nionyeshe mahali alipo, nampenda si kama mpenzi, bali kama mtu aliyeokoa maisha yangu nilipougua saratani ya damu, bila Kevin, amini usiamini, ningekuwa marehemu, umempeleka wapi?”
“Tulia nitakuambia!”
“Niambie sasa hivi!”
Jamal alishuka kitandani na kupiga magoti mbele ya Catarina, akilia kama mtoto mdogo, huku akisimulia mkasa mzima wa namna alivyokutana na Kevin ofisini kwake, akajitolea kumsaidia ingawa lengo lake halikuwa kufanya hivyo, bali alitaka kumwondoa duniani ili awaache wawili na mtoto wao atakayezaliwa waishi vizuri kwa raha mustarehe.
“Kwa hiyo umemuua?”
“Ndiyo.”
“Mamaaaaa! Mamaaaaa! Kevin wangu!” alilia kwa nguvu Catarina, wala hakuogopa tena watu kugundua alikuwa ndani ya nyumba hiyo na hatimaye kuhatarisha maisha yake.
“Tafadhali nyamaza, naomba unisamehe, nilifanya hivyo kulilinda penzi letu!”
“Ndiyo uue mtu?”
“Sikumuua!”
“Umefanya nini?”
“Nimemwacha porini aliwe na wanyama wakali.”
“Mungu wa Mbinguni, aliyeniokoa mimi kwa kukutuma wewe porini uje kuniokoa ndiye atakayemwokoa Kevin, amen!” alisema Catarina.
“Amen.” Jamal akaitikia.
Wakakumbatiana na kuendelea kulia kwa muda mrefu, Catarina akimlilia Kevin na Jamal akimbembeleza Catarina anyamaze lakini kwa kulia pia! Kwa saa mbili walikuwa katika hali hiyo, Catarina akimlaumu Jamal kwa kitendo chake cha kutoa uhai wa mtu asiye na hatia.
“Umekosea, umeniumiza, nilikuwa tayari kuishi na wewe maisha yangu yote, lakini kwa sababu umeua, upendo wangu umepungua, sina uhakika tena kama nitaweza kuishi na wewe siku zote za maisha yangu!”
“Nisamehe!”
Je, nini kitaendelea? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.