ILIPOISHIA…
Jamal hajakata tamaa bado anaendelea kuomba msamaha kila siku, akijaribu kumshawishi Catarina kwa zawadi mbalimbali na maneno matamu lakini msimamo wa msichana huyo bado unaonekana kuwa palepale, Jamal aliondoka kazini asubuhi na kurejea nyumbani na mara zote alimkuta Catarina akilia.
Hali ndani ya nyumba yao ilikuwa imebadilika kabisa, furaha na upendo uliokuwa umejengeka kati yao ulishapotea kabisa, chuki ya Catarina ikionekana wazi kwa Jamal kwa sababu tu ya kubaini ukweli kwamba mwanaume huyo pamoja na kumpenda kupindukia hakuwa binadamu wa kawaida, alimuona katili na mtu asiyekuwa na huruma hata kidogo.
Siku chache baadaye Jamal anarejea kutoka kazini na kuingia ndani ambako anamkuta mkewe hayupo, anakimbilia chumbani nako pia hamkuti jambo linalochanganya ubongo wake anatoka nje ni huko katika zungukazunguka yake anamwona Catarina akiwa ameketi kwenye moja ya msingi pembezoni mwa nyumba yao, anamsogelea kisha kuanza kuongea naye.
Ni katika mazungumzo hayo ndiyo Catarina anamweleza Jamal ukweli kwamba amefikiria kwa muda na kuamua kumsamehe kwani hata kama angefikiria miaka elfu moja bado Kevin asingerejea anakwenda mbele zaidi na kumweleza kwamba pamoja na msamaha huo si rahisi kumtoa Kevin moyoni mwake. Furaha ya ajabu inamjaa Jamal haamini anachokisikia anamkumbatia mkewe na kuanza kummiminia mabusu mfululizo akiahidi kulitunza na kulilinda penzi lao hadi mwisho.
SONGA NAYO…
Kitendo cha Catarina kutoa msamaha kwa Jamal ni kama vile kilikuwa kimechipusha upya penzi lao, muda wote Jamal alikuwa akitabasamu, kwa ilivyoonekana ndani ya mtima wake alikuwa akiteseka kupindukia, yote hii ilitokana na kumpenda Catarina, hakuwa tayari kumpoteza, alitaka awe naye mpaka kifo hiyo ndiyo ilikuwa dhamira aliyojiwekea.
“Mungu amesikia maombi yangu, amejibu nilivyokuwa nikitegemea, ni kweli nilimuua Kevin yote hii ni kwa sababu ya penzi nilililonalo juu ya Catarina, naamini huyu ni mwanamke wa maisha yangu…” aliwaza Jamal huku akimwangalia Catarina aliyekuwa amejilaza juu ya kitanda.
“Jamal! Jamal! Hebu rudi hapa upesi, unawaza nini tena? Si nimeshakusamehe au huamini.”
“Naamini mpenzi, moyo wangu ulikuwa na simanzi siko tayari kukupoteza ninakupenda mno Catarina wangu.”
“Sogea karibu yangu!” aliongea Catarina huku akimvuta Jamal karibu yake na sekunde chache baadaye wote walikuwa katika ulimwengu mwingine, kilichosikika ndani ya chumba wakati huo hakiwezi kuandikika gazetini!
“Nakupenda Jamal! Wewe na Kevin mmefanikiwa kuteka moyo wangu kwa sababu moja kubwa!”
“Ipi hiyo mpenzi?”
“Mmeokoa maisha yangu!”
“Ahsante, ninakupenda pia si wewe tu bali mtoto wetu mtarajiwa.” Alijibu Jamal huku akinyanyuka kitandani na kuketi kitako.
Hakuna siku iliyokuwa ya furaha kama hiyo kwa Jamal, hakika alijiona mshindi, kufanikiwa kumrejesha Catarina katika himaya yake, kwake ulikuwa ni zaidi ya mtihani, akauahidi moyo wake kutimiza yale yote ambayo alikusudia ili tu kuhakikiksha Catarina hapati shida ya aina yoyote na ikiwezekana kumsahaulisha kabisa jina la Kevin.
Penzi ndani ya nyumba lilikuwa limezaliwa upya, Jamal akionyesha upendo wa hali ya juu na Catarina pia vivyo hivyo, pamoja na ujauzito wake kuwa mkubwa bado hakuacha kumtimizia mpenzi mambo yote aliyoyahitaji.
“Catarina!” Aliita Jamal siku moja.
“Bee mpenzi!”
“Nataka nikutafutie mtu wa kukusaidia sasa, hali yako hairuhusu tena kufanya kazi.”
“Kwa nini?”
“Si kwa ubaya, napenda kukuona unapumzika.”
“Lakini sijachoka, bado nina nguvu za kutosha.”
“Una hakika.”
“Asilimia mia moja.”
“Haya, ila mimi naona umechoka na unahitaji msaada.”
“Utanisaidia wewe mpenzi au na wewe umechoka?”Aliuliza Catarina huku akiachia tabasamu.
“La hasha, siwezi kuchoka kwako, ninakupenda mno, ninakuonea huruma tu.”
Hali ndani ya nyumba ilishatulia kabisa, furaha na mapenzi yakiendelea vizuri, Jamal akitimiza wajibu wake vivyo hivyo Catarina, kama ilivyokuwa ada, Jamal hakuacha kurejea nyumbani mara tatu kwa siku ili tu kumjulia hali mke wake mpenzi.
Daktari wa Catarina naye akifika kila mara kuangalia maendeleo ya mteja wake pamoja na mtoto aliyekuwa tumboni, mara zote alipompima Catarina alitoa majibu ya ujauzito kuendelea vizuri na hakukuwa na tatizo lolote lile lililogundulika.
“Daktari nitakulipa fedha yoyote utakayo ili mradi tu uhakikishe mke wangu anajifungua salama bila matatizo, sitaki kumpoteza yeye wala mtoto.”
“Hakuna shida, kila kitu kinakwenda sawa kabisa, wote wawili wako salama.”
“Jambo moja ningependa kufahamu ni jinsi gani atajifungua.”
“Kama mambo yatakwenda vizuri atajifungulia hapa hapa nyumbani nami nitakuwepo kumsaidia lakini ikitokea akahitaji upasuaji basi ni lazima apelekwe hospitali sijui unasemaje?”
“Hakuna shida, ila ningependa ajifungue hapa nyumbani kwa njia ya kawaida, lipo jambo ambalo nahitaji kulificha pengine kwa usalama wake na mtoto.”
“Usijali, kila kitu kitakuwa sawa kabisa.” Alijibu daktari.
Hakuna kitu kilichoumiza akili ya Jamal kama siku ambayo mke wake alitarajiwa kujifungua, alitamani siku hiyo ifike haraka ili hatimaye kukamilisha zoezi moja tu ambalo lingekuwa limebaki; Ndoa na baada ya hapo waishi maisha ya raha mustarehe kwani hakukuwa tena na kizuizi kingine mbele yao ambacho kilikuwepo kwani tayari Kevin alishakufa kwa kuliwa na wanyama wakali katika hifadhi ya mbuga ya American National Park.
Mwezi wa saba katikati Catarina alikuwa amechoka kabisa hali iliyolazimu Jamal kuomba ruhusa kazini ili kupata muda wa kushinda na mkewe nyumbani.
“Mke wangu mimi nadhani niombe likizo kidogo ili nibaki na wewe hapa.”
“Kwa sababu gani?”
“Umechoka sasa au unasemaje?”
“Hapana binafsi napenda ufanye kazi ili upate fedha si unajua mtoto atakayezaliwa atahitaji matunzo muhimu.”
“Najua ila nikikuangalia hata kupika tena huwezi, umechoka.”
“Wasiwasi wako tu sina tatizo lolote na kama lingekuwepo daktari wetu angesha-kuambia Jamal au humwamini?”
“Namuamini kwa asilimia mia ila basi tu nataka kufanya hivyo unakuwa mpweke sana hapa nyumbani kwa hali yako unatakiwa upate mtu wa kuongea naye.”
“Unataka nisiwe mpweke?”
“Kabisa.”
“Leo nataka nikuambia jambo ambalo nina hakika litaniondolea upweke, uko tayari?”
“Niko tayari jambo gani hilo mpenzi wangu?” alijibu Jamal huku macho yake yakishuhudia hatua za Catarina kumwelekea mahali alipokuwa ameketi.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1
Nini anaoneshwa teena?