×

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-17

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Nancy na Aisha wakakutana macho, wakakumbukana. Nancy alishangaa sana kumkuta Aisha nyumbani kwa Neema wakati kule baa aliingia na Bony wakiwa wameshikana mikono…
JIACHIE MWENYEWE…

“Mh! Ina maana…” aliwaza moyoni Nancy lakini alishindwa kumalizia kutokana na mshangao mkubwa alioupata…
“Za leo anti?” alisalimia Nancy kwa uso wenye furaha ya kujilazimisha…
“Salama, za kwako?” alijibu Aisha naye kwa sauti iliyojaa wasiwasi na uso uliochangamka kinafiki…
“Kwani mnafahamiana?” aliuliza Neema baada ya kuona kuchangamkiana kwa wawili hao.
Si Nancy wala Aisha aliyekubali kwamba wanafahamiana. Zaidi sana walibaki kimya wote…
“Nancy njoo tule shoga yangu,” Neema alikaribisha baada ya kutopata jibu.

Lakini moyoni, Neema alitatizwa sana na kitendo cha kutopata jibu la maana kwa Aisha na Nancy.
Walikaa meza moja kwa ajili ya chakula, Neema alipokaa, mumewe, Bony alimuweka kulia kwake. Kushoto kwake alikaa Nancy, Aisha alisimama akisubiri kuwanawisha maji…
“Karibu mgeni,” Aisha alianza kusema akiwa ameshika jagi lenye maji ya moto na beseni la kuogea…
“Asante sana,” alishukuru Nancy akikinga mikono ili amwagiwe maji…
“Lady’s first,” Neema alisema ili kuondoa ukimya uliopo. Wote wakacheka, lakini Bony alicheka kicheko cha maumivu. Maumivu kwa maana ya kwamba, kila alipowaangalia wanawake hao, alijisikia vibaya kwamba, wawili anabanjuka nao. Neema mkewe na Aisha halafu Nancy naye yuko njiani…
“Da! Mimi kweli kiboko…yaani wote hawa wake zangu!” alijisemea moyoni Bony huku dhamira ikimuuma.

Wakati wa mlo, Neema ndiye aliyeanza kuchangamsha wenzake…
“Nancy, huyu mrembo hapa anaitwa Aisha. Mumewe anaitwa Mudy, yuko masomoni Uingereza. Sasa kwa sababu ndoa yao changa, ni wenyewe tu, ndiyo tuko naye hapa…”
“Aha! Sawa, nashukuru kukufahamu,” alisema Nancy huku akimwangalia Aisha mwenyewe kwa macho ya kejeli…
“Aisha, huyu ni matroni wa harusi yangu, anaitwa Nancy. Alipoteza namba zangu za simu lakini bahati nzuri jana alikutana na mista sijui wapi huko, akampa,” Neema alizidi kutambulisha…
“Sawa, na mimi nashukuru kukufahamu mrembo,” alisema Aisha huku akiangalia pembeni tofauti na Nancy ambaye alisema na kumkazia macho.

Ukimya ulitawala kwa sababu kila mmoja kati ya Nancy, Bony na Aisha alikuwa unaujua ukweli na Aisha alijua anacheza na hatari kwani Nancy akifunguka tu amekwisha. Mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda kwa kasi ya ajabu. Alihisi kushiba chakula kile…
“Mwenzetu mbona kasi ya kula ndogo?”Neema alimuuliza Aisha…
“Kawaida tu,” alijibu Aisha…
“Hata mimi nahisi hivyo,” alisema Nancy ambaye moyoni alijua kwa nini Aisha hakuwa sawasawa.
***
Nancy alipumzika kwenye kochi kubwa baada ya kula wakati Aisha alikuwa chumbani kwake, Bony naye aliingia kupumzika kidogo chumbani kwake, sebuleni Neema alikuwepo akimpa sapoti mgeni wake, Nancy…
“Hivi Neema…huyu msichana wewe unamwamini?” aliuliza Nancy…
“Kwa nini nisimwamini Nancy…? Au we umeona kitu chochote tofauti?”
“Ah! Mimi namwona kama hajatulia vile? Kusema kweli kwa mimi siwezi kukubali niishi naye nyumba moja na mume wangu labda niwe singo…”
“Nancy mbona hana tatizo?”
“Hana tatizo? We unadhani akiwa nalo utajua? Mfano, namba ya shemeji Bony si anayo?”
“Anayo ndiyo…”
“We unaamini nini hapo? Je, wakipigiana simu wakakutana mbele kwa mbele huko we utajua?” alisema Nancy…
“Yaani hilo Nancy sitarajii kama linaweza kutokea. Anajua familia zetu zilivyo na ukaribu na kama akiwa na mawazo hayo basi ni mwanamke mmoja hatari sana kuliko wale wenye hatari za waziwazi…”
“Ndiyo nakupasha sasa upashike, si msichana mzuri kwako, mimi najua kuliko wewe.”
Neema kama aliingiwa na mawazo tofauti…
“Nancy,” aliita…
“Niambie shoga yangu…”
“Kwani we unajua nini kuhusu Aisha? Maana hata mliposalimiana niliwauliza kama mnajuana, nahisi mlichangamkiana. Naamini wewe na Aisha mnajuana tangu siku nyingine.”
Kabla Nancy hajajibu, Bony alitokea na kukaa hapo sebuleni, wakakata mazungumzo yao hapo. Na simu ya Neema iliita…
“Haloo…eee…haya nakuja,” Neema alisema na kukata simu…
“Darling, yule fundi anasema kamaliza lile gauni na kesho anakwenda Tanga. Ngoja niende mara moja…Nancy nakuja baada ya dakika ishirini,” Neema alimwambia mumewe na Nancy, akasimama na kwenda kuchukua sendozi, akatoka.
Ile anafunga mlango tu, Nancy akamdaka Bony…
“Shemeji mi sikubali…”
Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, Ijumaa ijayo.

Leave a Comment