Ilipoishia Jumamosi:
Mambo yote yalipokamilika, nilipanda ndege ya safari namba BA46 siku ya Julai 3 ambayo iliondoka Dar es Salaam saa 2:30 asubuhi na kuwasili London kunako saa 10:40.
Sasa endelea…
Kilichonishangaza ni kwamba tukiwa njiani vyakula vilikuwa ni vitu vichache vya moto, mikate iliyochanganywa na nyama (sandwiches) na biskuti; hiyo ni bila kusahau kwamba tulikuwa daraja la kwanza.
Hali hiyo ilikuwa ya kusikitisha. Iwapo hali hiyo kwetu ilikuwa hivyo, je ilikuwaje katika wasafiri wa daraja la kawaida? Hili lilinitokea wakati ni muda mrefu ulikuwa umepita tangu nisafiri kwa shirika la BA mara ya mwisho.
Tulipowasili, mhudumu mmoja wa kike aliwauliza maofisa wa shirika hilo waliokuwa wamesimama nje ya ndege hiyo iwapo kulikuwa na mtu aliyepangwa kunichukua katika kitu cha magurudumu. Baadaye alitokea mtu mzima ambaye alinisaidia kuelekea kwenye kiti cha magurudumu.
Alikisukuma kiti hicho hadi katika sehemu aliyokuwa ameegesha moja ya vitoroli vya umeme ambamo tuliketi. Alirejea haraka kwenye ndege kwenda kumchukua mtu mwingine aliyekuwa mgonjwa kama mimi. Baada ya dakika kumi alirejea akiwa na mwanamke mzee mwenye asili ya Asia.
Alitupeleka kwenye sehemu ya kupokelea mizigo ambako nilimkuta Mwambata wa Jeshi (DA) la Tanzania wa Ubalozi wa Tanzania, Kanali Dominic Mrope, aliyekuwa akinisubiri. Aliichukua mizigo yetu, akaiweka katika toroli na kuelekea katika sehemu ya uhamiaji. Tulipita bila matatizo katika idara ya forodha na tulipotoka nje tulimkuta mwanetu, Bisala akitusubiri.
Tulielekea London Kaskazini na tukafikia katika Premier Hotel ambayo ilikuwa ndiyo pawe makao yetu kwa wiki tatu zilizofuata. Tulikaa hapo kwa siku mbili wakati Mwambata wa Jeshi alipokuwa akipitia ratiba yetu; kisha alinipigia simu alinifahamisha kwamba Dk. Sheaves wa London Clinic alikuwa tayari kuniona siku iliyofuata ambayo ilikuwa Julai 5. Mwambata alimtuma dereva wake kuja kutuchukua. Nilibeba karatasi zote za rufaa, za eksirei, picha za ‘Ultrasound’ na za MRI.
Daktari huyo aliisoma barua na kuzipitia picha husika akaniambia kwamba zilikuwa zinaonesha kila kitu lakini angefanya uchunguzi wake ili awe na uhakika kabla ya kutoa dawa yoyote. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kuchunguza damu ili kupata picha kamili ya jinsi ini, figo, na kadhalika vilivyokuwa vikifanya kazi.
Kisha alinielekeza kwa daktari mwingine, ambaye jina siwezi kulikumbuka ili nikachunguzwe kutokana na kupumua kwa shida. Nilipewa jaribio la kuchunguza mapigo ya moyo ambapo niliambiwa nitembee katika mashine maalum ya kuendeshwa kwa miguu ili kujua moyo unavyofanya kazi. Pia nilifanyiwa vipimo vya ‘Ultrasound’ na MRI siku ileile.
Niliporejea kwa Dk. Sheaves tarehe 8 Ijumaa, alinielekeza kwa Dk. Rogers ili nifanyiwe uchunguzi wa njia ya mmeng’enyo wa chakula kwa kutumia chombo maalum chenye mwanga na kamera (endoscope) kinachomwezesha daktari kuona kilichomo katika njia hiyo kupitia kwenye kiwambo cha televisheni ya rangi. Kipimo hicho kitaalam huitwa ‘endoscopy’.
Ilibidi pia nifanyiwe uchunguzi wa njia ya hewa kwa kutumia chombo kiitwacho ‘bronchoscope’ ambapo daktari angebaini matatizo yaliyokuwa katika koo, zoloto (koromeo), bomba la pumzi na njia nzima ya kupitishia hewa. Kitaalam, kipimo hicho huitwa ‘bronchoscopy’.
Kipimo cha ‘endoscopy’ kilifanywa siku hiyohiyo na cha ‘bronchoscopy’ kilifanywa Jumatatu tarehe 11. Siku ya tarehe 13, nilirejea kwa Dk. Sheaves ambaye alichukua damu zaidi kutoka kwangu na kunielekeza kwa Dk. Peters wa London Bridge Hospital ambako nilimwona tarehe 15.
Baada ya majadiliano marefu na kunifanyia vipimo vya mazoezi ya mwili, alipendekeza nimwone daktari ambaye angeondoa moja ya uvimbe ili kuufanyia utafiti. Nilirudi kwa Dk. Sheaves siku ya tarehe 18 ambako alinipa nesi mmoja wa kunipeleka kwa Dk. Satvinder Mudan, mtaalam wa upasuaji.
Yeye alinifanyia utafiti wa uvimbe mbalimbali niliokuwa nao na akaamua kuuondoa mmoja uliokuwa chini ya mfupa wa shingo (mtulinga) ambako hapakuwa na hatari ya kukata mshipa wa fahamu. Aliniambia kurejea siku ya tarehe 19. Niliporejea alinipa dawa za ganzi na kuung’oa uvimbe huo akampatia mtaalam wa magonjwa kwa ajili ya uchunguzi.
Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi ijayo.