×

Mkuki moyoni mwangu – 69

MAPENZI ndani ya nyumba yamerejea upya, Jamal na Catarina wakionekana kuwa wenye furaha muda wote, jambo hili pekee lilirudisha tumaini kwa Jamal kwamba Catarina asingeondoka na alikuwa amemsamehe kwa moyo wake wote.

Maisha yalikuwa yakiendelea Jamal akitoka na kwenda kazini na kurejea mara tatu kwa siku kumjulia hali mpenzi wake ambaye mpaka wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba na daktari ambaye alitafutiwa alifika nyumbani mara kwa mara ili kuchunguza afya ya mama na mtoto aliyekuwa ndani ya tumbo la Catarina.

Hakuna kitu kilichoumiza akili ya Jamal kama siku ambayo mke wake alitarajiwa kujifungua, alitamani siku hiyo ifike haraka ili hatimaye kukamilisha zoezi moja tu ambalo lingekuwa limebaki; Ndoa na baada ya hapo waishi maisha ya raha mustarehe kwani hakukuwa tena na kizuizi kingine mbele yao ambacho kilikuwepo kwani tayari Kevin alishakufa kwa kuliwa na wanyama wakali katika hifadhi ya mbuga ya American National Park.

Kwa huruma aliyokuwa nayo juu ya mpenzi wake huyo aliamua kumweleza nia yake ya kumtafutia msaidizi lakini Catarina alikataa na hata anapomshawishi angalau akubali aombe likizo kazini bado akaendelea kukataa. Siku moja wakiwa katika mazungumzo yao ndani ya nyumba Catarina anamwambia mpenzi wake huyo kwamba alitaka amwambie jambo ambalo aliamini lingemwondolea upweke. Je ni jambo gani hilo?SONGA NAYO…

Jasho njembamba lilitirika mwilini mwa Jamal, pamoja na kukubali kusikia jambo ambalo Catarina alitaka kumwambia bado hakuelewa lilihusu nini, mapigo yake ya moyo yakaruka mfululizo, hofu ya ajabu ikamjaa, hakuwa tayari kusikiliza jambo lolote lile ambalo lingeenda tofauti na alivyotaka.
“Mbona umebadilika ghafla hivyo?”

“Hapana, nataka tu uniambie ulichosema.”
Huku akiwa katika kutabasamu, Catarina akamsogelea Jamal kisha kuweka mkono wake juu ya kifua upande wa moyo, akayasikia mapigo yake na kushangaa.
“Umepatwa na nini mpenzi wangu?”

“Hofu, siko tayari kusikia kitu ambacho kitaumiza mtima wangu.”
“Hebu tulia, acha uwoga, kwani umenitenda ubaya?”
“Mh!”Alijibu Jamal akiachia tabasamu kwa mbali japo ndani yake alihisi mkuki moyoni mwake.
“Nakupenda.”

“Nakupenda pia unajua, je ni hilo ndilo ulitaka kuniambia?” Jamal akauliza.
“Hapana.”

“Tafadhali niambie lakini usijaribu kukumbuka yaliyopita, yataniumiza, lakini pia siko tayari kusikia kwamba unataka kuniacha Catarina.”

“Ha!Ha!Ha!Haaa!” Catarina alicheka huku akiketi vizuri juu ya kiti.
“Niambie basi nakusikiliza mpenzi wangu, niondoe kwenye hofu iliyoko ndani ya mtima wangu.”
“Hakuna kitu kibaya, nataka kukuomba uniletee televisheni tu!”
“Oooooops!” Jamal akashusha pumzi, hakutarajia kusikia neno hilo kutoka kwa Catarina.
“Pole, ni hilo tu hakuna kingine, nataka niwe naangalia mambo mbalimbali yanayoendelea duniani, lakini pia kunifanya nisiwe mpweke mpaka pale utakaporejea kutoka kazini.”

“Usijali, kesho nitakwenda mjini na nitakaporejea jioni nitakuwa nayo.”
“Ahsante mpenzi, ahsante kwa kunipenda, hakika nimegundua nilitupwa ndani ya hifadhi ili tukutane na hatimaye mimi kuwa mpenzi wako si hilo tu nikuzalie mtoto mzuri.”

“Mwaah! Mwaaah!” Yalikuwa ni mabusu mfululizo kutoka kwa Jamal kwenda kwa Catarina.
Jioni ya siku hiyo baada ya kuongea mengi hatimaye walikula chakula na kupumzika huku wakiongea mambo mbalimbali kuhusu maisha lakini pia juu ya mtoto ambaye alikuwa karibuni kuzaliwa, watakavyompokea, kumtunza mpaka kukua wote wakionekana wenye furaha kupindukia.
***
Siku iliyofuata Catarina ilionekana kwenda polepole, alitamani jioni ifike ili mpenzi wake arejee akiwa na televisheni kwani kwa muda hakuwahi kuangalia, hatimaye mbele yake zikiwa zimebaki saa mbili tu ili Jamal awasili, alijikongoja na kuingia jikoni haraka akaandaa chakula cha jioni ambacho aliamini kabisa Jamal angekula chakula hicho kwa furaha.

Hatimaye nusu saa tu baadaye ikiwa imetimu saa kumi na moja na nusu, alisikia honi ya gari nje ya nyumba na alipotupa macho yake kupitia dirishani aliliona gari alilolifahamu, lilikuwa gari la mpenzi wake Jamal, moyo wake ukajaa furaha ya ajabu, akashuhudia akishuka na kufungua mlango wa nyuma hatimaye boksi kubwa likaonekana.

“Kweli amekuja nayo!” Alitamka maneno hayo akisogea mlangoni ili kumpokea mpenzi wake. Huku akionyesha kufurahia ahadi ambayo mpenzi wake alimuahidi akamsaidia kufungua mlango na Jamal akaingia ndani kisha kuliweka boksi lililoonekana kuwa na televisheni ndani yake.
“Nimetimiza wajibu wangu.”

“Ahsante mpenzi wangu! Siamini macho yangu sasa nitakuwa si mpweke tena.”
“Hakika.” Akajibu huku akiingia chumbani ambako alivua nguo zake kisha kuingia bafuni kuoga ndipo mambo mengine yote yangefuata baadaye.

Alipotoka alikaribishwa mezani na kula chakula, Catarina akiwa pembeni muda wote huku akionekana mwenye furaha kupindukia jambo lililompa faraja Jamal na alipomaliza alilisogelea boksi kisha kutoa televisheni na kuiweka juu ya meza hapo akafunga na kuhakikisha ilikuwa sawa.

“Leo tukapumzike utaangalia kesho, ninatamani kukaa na wewe tu.” Aliongea Jamal kisha akanyanyuka na kumshika mpenzi wake mkono na wote wakatokomea na kuingia chumbani.

Walilala mpaka siku iliyofuata kama kawaida Jamal aliamka na kujiandaa, kunywa chai kisha kumuaga mke wake kwamba alikuwa akielekea kazini na angerejea kumjulia hali mchana wa siku hiyo. Wakaagana na Jamal kutoka ndani ya nyumba kisha kuingia ndani ya gari kuliwasha na kuondoka nyuma akimwacha Catarina.

Siku hiyo Catarina alijtahidi kufanya kazi zake zote haraka haraka ili angalau apate muda wa kuangalia televisheni kwani kilikuwa kimepita kitambo kirefu mno bila kuangalia na alipomaliza alioga vizuri kisha kuketi juu ya kochi kubwa kisha kuwasha akitafuta sehemu mbalimbali na kuangalia chaneli ambayo ingemvutia.

Mara ghafla alikutana na kipindi ambacho kilimvutia ndani ya televisheni hiyo mzungu aitwaye Matthew Bright mtafiti wa wanyama jamii ya Tembo alikuwa akielezea namna alivyowapenda Tembo na kwa namna gani alitumia muda wake mwingi katika hifadhi mbalimbali akifanya utafiti namna walivyoishi.

“New York Televisheni kinaonekana ni kipindi kizuri ngoja niangalie kikiisha hiki nitahamia sehemu nyingine!” alisema kwa sauti akiongea peke yake kisha kusogea karibu zaidi na televisheni kuongeza sauti.

Bwana Bright alikuwa akisimulia jinsi alivyoweza kufanikiwa kufuatilia Tembo kuzaliwa mpaka kufa kwa miaka kadhaa alikuwa amefanya kazi hiyo na kuamua kurekodi kipindi ambacho kingerushwa na jamii kujionea. Wakati akieleza yote hayo pembeni yake alionekana kijana mmoja aliyevalia kofia kubwa na miwani ya rangi nyeusi muda wote alionekana kutingisha kichwa bila kusema chochote.

Wakati bwana Bright akielekea ukingoni aliamua kumwelezea kijana ambaye alimwita kama msaidizi wake ambaye alikutana naye ndani ya hifadhi ya American National Park na kuamua kumchukua ili asaidiane naye katika utafiti wake. Akamtaka asimame na kujitambulisha. Kijana akasimama, kisha kuvua kofia na miwani na kujitambulisha.

Macho ya Catarina yakahisi kudanganywa, kijana aliyesimama alikuwa ni Kevin, tena akionekana mwenye afya njema, akapikicha macho yake tena na kuangalia yalikuwa hayamdanganyi, alichokiona ndicho kilichoonekana, alikuwa ni Kevin Mdoe, mwanaume wa maisha yake furaha ya ajabu ikamshika, akaruka juu kwa furaha bila kufahamu kwamba kwake ingekuwa tatizo akajikuta akianguka na kulalia tumbo lake hapo hapo akazimia.

Kwa takribani dakika kumi nzima aliendelea kulala chini akiwa katika hali ya kutojitambua alizinduliwa na ubaridi wa sakafu na kuketi, tayari kipindi kilikuwa kimekwisha.

“Hapana, Kevin wangu yuko hai, siwezi tena kubaki hapa, ninaondoka kwenda New York kumtafuta nitampata tu.” Alijisemea akinyanyuka, huku akiwa katika maumivu makali alijikongoja na kuisogelea meza ambayo juu yake ilionekana kuwa na vitabu, hapo akatafuta karatasi ndogo pamoja na kalamu alitaka kuandika ujumbe ambao angemwachia Jamal na yeye kuondoka kwenda New York.

Jamal,
Nakuandikia barua hii nikibubujikwa na machozi, hakika halikuwa kusudio langu, najua unanipenda nami nakupenda pia, ila leo nimeshuhudia jambo la ajabu ambalo limenifanya nichukue hatua ya kuondoka; Kevin, kumbe hakufa, yuko hai.

Hivyo basi kwa sababu ni mwanaume wa maisha yangu, nimeamua kuelekea New York kumtafuta, nataka nikutane naye na kumwomba msahama kwa yote, naondoka nikiwa na ujauzito wako nakuahidi jambo moja nitailea mimba yako kama ulivyokuwa ukifanya na mtoto atakapozaliwa nitamtunza pia.

Naomba unisamehe, sikuwa na namna yoyote ile, penzi nililonalo kwa Kevin ni zito mno, siko tayari kumkosa maishani mwangu, kumbuka maisha yangu hayakuwa kamili. Baki salama, najua utaumia naomba unisamehe, ahsante kwa kuniokoa na kunitunza maisha yangu yote nitakukumbuka, wewe ni mtu wa pekee lakini si kama Kevin wangu.
Ahsante.
Ni mimi Catarina.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment