×

Wewe unanukia, mwenzio kikwapa, inahuu?

Asalaam aleikumu wapenzi wasomaji wangu, naamini Mungu amewaamsha salama mnaendelea vema, Alhamdulillah ninashukuru Mungu nami pia sijambo.
Leo katika safu yetu nimeamua kuja na mada hii kwa sababu nimekutana na wanawake wengi ambao wako maridadi sana, lakini waume zao kuanzia mavazi hadi harufu inayotoka miilini mwao unajiuliza mara mbili kama kweli ni mume wake.
Kwa nini wanawake wenye wanaume wa namna hii mnalikubali hili, hivi mume akiwa mchafu, ana viharufu harufu huoni kama aibu yako?
Nikwambie tu shoga, wanaume ni kama watoto, siku zote wanatakiwa kupata muongozo kutoka kwa wake zao hasa masuala ya kuvaa vizuri, kunukia vizuri na kuwa smati kwa ujumla.

Mwanamke unalo jukumu la kuhakikisha unafua na kupiga pasi nguo za mumeo na kujua kabisa nini anatakiwa kuvaa kesho.

Utakuta mwanaume mwingine anavaa soksi zinanuka kiasi kwamba akifika sehemu hawezi kuzivua kwa kuona aibu, wengine soksi zimechanika. Baadhi ya wanaume siyo kwamba hawawezi kununua, sema wanakuwa bize kutokana na kutafuta maisha au ule utamaduni wa Kiafrika kuwa mke ndiye mwenye jukumu la kusimamia usafi wake.

Wanawake wenzangu, hii ni sehemu ya kudumisha penzi lako, mume ukimjali kila wakati hawezi kutoka nje ya ndoa yake kwa sababu ya huduma anazozipata. Akitoka na kukuta kumedorora, haraka anarudi ndani.
Mwanamke unapoamka na kujiuliza utoke vipi ili uonekane smati, kumbuka na mumeo naye anapaswa kuwa kama wewe kisha watoto wanafuata kwani haya yote ni majukumu ya mama.

Jaribu kumshawishi mume kile unachohisi akivaa ataonekana smati, kuna msemo wa baadhi ya wanawake eti wanamfulia na kumpangia nguo mumewe ili akasifiwe na wanawake wengine. Huu siyo sahihi, huwezi kujenga fikra kama hizo kwani hii inaweza kukufanya ukashindwa kumfanyia mambo mazuri mumeo kwa sababu za kijinga.

Ukimuacha akatoka nje, usije ukashangaa wenzako wakampetipeti na hata kumnunulia nguo za ndani.
Asikwambie mtu, hakuna kitu kizuri kama kumnunulia mumeo nguo za ndani, si unajua kuwa unahifadhi mali zako sasa kwa nini usijivunie hilo?
Bila shaka mmenielewa, wiki ijayo tuonane kwa makala nyingine nzuri.

Leave a Comment