×

Nilivunja Ndoa Yangu na Shetani-27

ILIPOISHIA:
Kwa kuwa nilikuwa mwenyeji wao niliwakaribisha sebuleni:
“Jamani karibuni sana wageni wangu.”
“Asante mother house,” walijibu kwa pamoja.
“Jamani nakuja,” niliwaacha na kwenda chumbani nilipokuwa nimemuacha Papaa nikamjulishe watu wake wamefika.
Nilimkuta akiwa bize na mtandao, nilipoingia aliacha na kunigeukia.
SASA ENDELEA…

“Mpenzi vipi?”
“Safi.”
“Za huko?”
“Nzuri.”
“Wanasemaje?”
“Hawana tatizo.”
“Nini kimeendelea?”
“Nimewaeleza wamenielewa kila kitu kipo poa.”
“Kwa hiyo umewaeleza nimewaitia nini?” Mmh! Swali lilikuwa la mtego kutaka kujua kama nimekwenda kinyume na maelekezo yake.
“Papaa ulinieleza nini?”
“Hujanijibu uliwaeleza wanakuja kufanya nini?”
“Nimewaeleza watajua wakikutana na wewe.”
“Si kweli, wanawake wengi hamna siri lazima kuna kitu uliwagusia, nakuuliza uliwaeleza nini,  lazima umekwenda kinyume na maagizo yangu.”
“Niliwaeleza unawaita na…na kama wataifanya vizuri, kazi ya kuuza mwili itakuwa imefika mwisho.”
“Sawa,  uliwaeleza kufanya kazi gani?”
“Papaa maswali gani hayo, kama huniamini hukutakiwa kunishirikisha naona unataka niishi maisha ya mashaka.
Nimekujibu unanilazimisha nikueleze nisichokijua. Sina jibu na kama unaona huniamini tuachane.”
“Siwezi kukuacha hivihivi.”
“Weee hunifanyi lolote sijakufuata umenifuata niache na tabu zangu,” nilijikuta nikipata ujasiri wa ajabu wa kumjibu Papaa.

“Mrembo hiyo jeuri ya kunijibu hivyo umeitoa wapi? Hata hao wanaume hawana jeuri hiyo,” alinichimba mkwala.
“Papaa hunijui siyo, sijakuficha maisha yangu hivyo siogopi kitu zaidi ya kuheshimu. Kwa hiyo suala la kutishana liondoe kabisa, kama unataka tufanye kazi basi tupige kazi siyo kutishana.”
“Mmh!” Papaa aliguna.

“Ninapoamua kufanya jambo huwa makini umenionya nisimwambie mtu nimwambie ili iweje, nimekuletea watu ulionituma sasa tufanye kazi sitaki maswali ya kijinga,” nilionesha nina msimamo.
“Mmh! Kweli nimepata mtu.”
“Katika maisha yangu naogopa kitu kimoja tu.”
“Kipi hicho?”
“Kuua tu, lakini chochote naweza kukifanya ili kupata pesa.”
“Nimekuelewa, basi mwambie dada awahudumie kila kitu kisha wapewe nguo za kitawa wanisubiri.”
“Sawa.”
Nilitoka hadi sebuleni na kumpa dada wa kazi maelekezo, aliwachukua kina Doi na kuwapeleka katika chumba cha mavazi na kubadili nguo zao za kawaida na kuvaa mavazi ya kitawa. Sekunde chache wote waligeuka watumishi wa Mungu na si machangudoa.

Walirudi sebuleni baada ya muda waliletewa glasi kubwa iliyokuwa imejaa bia kwa kila mmoja. Hawakutakiwa kunywa sana kwa vile walikuwa na kikao na Papaa kwa ajili ya kazi nzito iliyokuwa ikija mbele yetu.
Niliwatahadharisha wasinywe sana ila  baada ya mazungumzo wanywe tani yao.

Shoga zangu kila walivyojiangalia walichekea chini wengine walipiga alama ya msalaba na kujikumbatia kila mtu akiwa na tabasamu usoni kwake baada ya kujiona amebadilika.

Kwa kweli jinsi walivyobadilika ilipendeza sana, moyoni nilitamani sote tumrudie Mungu wetu kwa kuacha biashara ya kujidhalilisha ya kuuza mwili.

Lakini  moyo wangu uliingia ukungu baada ya kujua tunamcheza shele Mungu kwa kujidanganya wacha Mungu bila kujua tulikuwa tukimchokoza bila kujua adhabu yake ni kubwa.

Baada ya muda Papaa alikuwa na kikao nao na mimi kuwa chumbani kwa ajili ya kupumzika kwa vile Papaa alisema ana hamu na mimi hivyo alitaka anikute chumbani. Nilikwenda chumbani na kufanya usafi wa mwili kumsubiri mpenzi.
Baada ya kikao alirudi chumbani na kunieleza kila kitu kimekwenda vizuri nao kuanzia siku ile watahamishiwa tunapoishi ile wawe karibu yangu huku nami nikijiandaa kwa kazi ya kuihadaa dunia kwa faida ya watu wachache wanaotumia Neno la Mungu vibaya.

Baada ya kustarehe tulipumzika na jioni tulitoka na kwenda kwenda hoteli moja kubwa jijini Nairobi ambako tulikunywa na kucheza mpaka usiku wa manane tulipotudi nyumbani kulala. Lakini cha ajabu Papaa tuliyemuacha nyumbani hatukumkuta.

***
Baada ya kila kitu kwenda kama kilivyopangwa, nikiwa chini ya ulinzi mkali nilitembezwa sehemu zote nilizotakiwa kutembezwa kama kwenye jalala, sokoni na kituo cha basi.
Baada ya zoezi lile kukamilika nilirudi nyumbani na kuanza zoezi lingine la kufumua nywele na kuziacha timutimu kisha ziliwekwa vumbi la mbao na udongo kupakwa masizi usoni na kupatiwa ndala chakavu za msalani.
Nilipigwa picha huku nikitengenezwa na mtaalam wa kutengeneza sura akirekebisha sehemu zilizoonekana zina mushikeri.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave a Comment