Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.
Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.
Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta amefika kwa mzee ambaye anamwambia kwamba angemsaidia kufika Mwanza Mjini ila si kwa miguu kama aliyotaka yeye.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Dickson hakuwa na amani kabisa, kila alivyokaa ndani ya gari lile, mwili ulimsisimka, alikuwa na hofu moyoni mwake kana kwamba pale alipokuwa hakukuwa salama hata mara moja. Alibaki akiangalia huku na kule, alihisi labda kulikuwa na mtu aliyekuwa amemuona na kumgundua, ila kila alipopitisha macho yake, kila mtu alikuwa bize na mambo yake.
Hakujua sababu iliyomfanya kuwa na hofu namna ile, alijitahidi kuuletea moyo wake amani lakini haikuja kabisa. Akahisi lazima kungekuwa na kitu, hisia zake zilikuwa na maana kubwa mno, alichokifanya ni kutoka kwanza ndani ya gari.
“Ni lazima niondoke, haiwezekani hali kuwa hivi,” alisema huku akiteremka kutoka garini.
Wakati akiwa amesimama nje ya gari lile na kuangalia upande wa pili kutoka katika mgahawa ule uliokuwa kama hatua thelathini kutoka gari lilipokuwa limeegeshwa, akamuona mzee Saidi akija kule alipokuwa huku uso wake ukionesha furaha ya ajabu.
Hakutaka kujiuliza ni kitu gani kilitokea, alijua fika kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilimfanya mzee huyo kuwa katika hali hiyo, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo, tena kwa mwendo wa haraka na kwenda kujificha sehemu, katika moja ya magari yaliyokuwa yameegeshwa mahali hapo.
Macho yake yalikuwa yakimwangalia mzee Saidi kule ndani ya gari alipokuwa. Kwa muonekano tu, mzee huyo alionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha kumkosa Dickson ndani ya gari lile kilimchanganya mno, hakuamini kama kweli furaha aliyokuwa nayo ilikuwa ikienda kupotea kirahisi namna ile, hakukubali, akateremka na kuanza kumwangalia huku na kule, japo amuone na kuanza kumuitia mwizi na watu wamkamate, hakufanikiwa kumkamata kwani naye Dickson baada ya kuona hivyo, akaondoka zake.
Safari hiyo ilikuwa ni kwenda Msamvu, ilikuwa ni lazima aondoke mahali hapo, safari aliyoifikiria ni kwenda Dodoma kabla ya kuunganisha mpaka Singida, Tabora na kuanza mchakato wa kwenda jijini Mwanza.
Njiani, japokuwa watu walikuwa na hamu naye huku picha zake zikiwa zimebandikwa kila kona lakini hakukuwa na mtu aliyejua kwamba mwanaume waliyekuwa wakipishana naye alikuwa ni Dickson, waliendelea na mambo yao huku wakiwa hawana habari kabisa.
“Nataka kufika Dodoma…” alimwambia utingo mmoja, kofia na miwani vilikuwa kichwani na machoni mwake.
“Elfu saba…”
“Hakuna tatizo,” aliposema hivyo, akatoa hela, akalipia kisha kuingia ndani ya basi huku uso wake ukiwa chini. Akakifuata kiti alichoambiwa na kutulia hapo.
Wakati akiwa anafikiria maisha yake ya nyuma, ghafla macho yake yakatua kwa vijana wawili, walikuwa wakiongozana na polisi wawili waliokuwa na bunduki, walikuwa wakiwapa maelekezo yaliyompa wasiwasi.
Vijana wale wakalinyooshea vidole basi lile kisha kuanza kulifuata na polisi waliokuwa na bunduki mikononi mwao. Dickson alibaki akitetemeka, kitu kilichomjia kichwani kwa haraka zaidi ni kwamba vijana hao walimuona ndiyo maana waliwaita polisi hao kisha kuingia ndani ya basi hilo, abiria wote wakashtuka.
“Yupo wapi?” aliuliza polisi mmoja.
“Yupo kule, nimemuona kwa macho yangu,” alijibu kijana mmoja na kuanza kuelekea alipokuwa Dickson, polisi wale wakaandaa bunduki zao. Dickson akatamani kuruka kupitia dirishani, tatizo aliloliona madirisha ya basi hilo yalikuwa madogo hata kupenya kwa haraka, asingeweza.
* * * *
Japokuwa alikuwa mpelelezi lakini kwenye suala la mamba, alikuwa na hofu kupita kawaida, aliwaona mamba wale wakiingia mtoni pamoja naye na kuhisi kwamba wangeweza kumng’ata kama walivyofanya kwa wengine, alitamani kurudi lakini kila alipotaka kufanya hivyo, mzee yule akamwambia kwamba ni lazima asonge mbele.
Hakuwa na budi zaidi ya kuiamini dawa aliyopakwa na yule mzee, akaendelea kwenda mbele zaidi, alihisi kabisa akitembea pamoja na mamba hao waliokuwa chini lakini hakutakiwa kusimama, baada ya dakika tano kutembea mtoni, akafanikiwa kufika ng’ambo ya pili, alipoyapeleka macho kwa yule mzee, akamuonesha ishara ya dole gumba.
Hakutaka kubaki hapo, alikuwa na safari kubwa, alimtafuta Dickson ambaye aliambiwa kwamba alikuwa safarini kuelekea Mwanza hivyo ilikuwa ni lazima asonge mbele ili mwisho wa siku ampate mtu huyo ambapo moyo wake ulimfariji na kumwambia kuwa hakuwa mbali kutoka alipokuwa.
Safari ilikuwa ndefu, hakutaka kusimama, aliendelea mbele mpaka alipofika katika Mbuga ya Wanyama ya Mikumi, huko hakukuwa salama kwa maisha yake lakini hiyo haikumfanya kusimama.
Alikuwa na bastola mbili alizoziweka vizuri, moja kiunoni na nyingine mguuni mwake tena huku akiwa ameificha na suruali. Aliendelea mbele mpaka alipokutana na kundi kubwa la wanyama, walikuwa nyumbu na baadhi ya wanyama wengine kama pundamilia, tembo na wengine wanaokula majani.
Hakutaka kupita karibu nao, alikwenda kwa njia nyingine upande wa Magharibi, alitaka kutoka nje ya mbuga hiyo kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, hakukuwa na amani hata kidogo.
Wakati akiendelea na safari yake hiyo, akaanza kusikia muungurumo wa helikopta ikipita angani. Kwanza akashtuka, hakujua upande ilikokuwa ikitokea helikopta hiyo, alichokifanya ni kuanza kukimbia.
Hakukuwa na mti mrefu, eneo kubwa lilikuwa na nyasi nyingi, alijua kwamba helikopta hiyo ilikuwa ikifanya doria kuzunguka mbuga hiyo kwa ajili ya majangili ambao walitishia uhai wa wanyama kipindi hicho.
Wakati akiwa kwenye kasi ya kukimbia kuelekea upande huo wa Magharibi, akaanza kusikia sauti kutoka kwa mtu aliyekuwa katika helikopta ambaye alishikilia kipaza sauti akimtaka kusimama.
“Simama hapohapo ulipo,” ilisikika sauti ya mwanaume.
Hakutaka kukaidi, akasimama na kuanza kuiangalia helikopta ile.
Hakuwa na hofu hata mara moja, helikopta hiyo ikaanza kuelekea chini.
Wakati akiisubiria ili atoe maelezo, mara kwa mbali mbele yake akawaona simba wakianza kukusanyika kuelekea kulipokuwa na helikopta hiyo.
Hiyo ilimuogopesha, hakutaka kusimama tena, tayari mbele yake kulionekana kuwa na hatari, alikuwa na bastola na kama angepiga risasi basi simba hao wangekimbia kama tu wangesikia mlio wa risasi, ila kwa sababu mlio wa helikopta ulionekana kuumeza mlio wa risasi hata kama angepiga, hakuona sababu ya kusimama akaanza kukimbia.
Watu waliokuwa wakifanya doria kwenye mbuga hiyo walipomuona akikimbia, nao wakaanza kumkimbiza kwa helikopta hiyo huku wakirusha risasi kwani waliamini mtu huyo alikuwa jangili na alikuwa akiwakimbia.
Hawakutaka kujiuliza zaidi juu ya sababu iliyomfanya Fredrick kukimbia, hawakujua kama mtu huyo aliwakimbia simba, wao walichojua ni kwamba aliwakimbia wao kwa kuwa walitaka kumkamata, hivyo wakaanza kumkimbiza huku wakijitahidi kumrushia risasi alizozikwepa kwa mtindo wa zig zag, yaani kwenda kulia na kushoto, kushoto na kulia, tena kwa kasi ya ajabu.
Je, Fredrick atakamatwa? Usikose kufuatilia hadithi hii ya kusisimua wiki ijayo.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1