ILIPOISHIA GAZETI LA AMANI JANA:
Akakimbia kushuka chini na baada ya dakika moja tu, injini zikawaka na meli kuanza kukata maji. Kwangu sikujua kama ilikuwa kawaida au la!
“Kwani inawezekana Nurdin?” nilimuuliza.
“Kuhusu nini bwana Tolu?”
“Meli kuwakia ndani ya maji na kuanza safari?”
SASA ENDELEA NAYO…
“
Inawezekana bwana Tolu na ndiyo kama hivi sasa si unaona imewakia baharini na inaendelea na safari.”
Safari iliendelea lakini huku kila mmoja akijiuliza kwa nini meli ilizima injini? Kwa nini nahodha alikuja juu na kutupiga kisha kurudi tena kwenye chumba chake?
Nurdin alisema tukifika Mombasa tufanye mawasiliano na wamiliki wa meli maana wao walikuwa wakiishi Ubelgiji, tuwataarifu kuhusu tabia ya uvutaji wa bangi wa nahodha kwani aliamini alizima injini makusudi na ilitokana na kukolea bangi.
Wengi tulikubaliana kufanya hivyo kasoro mtu mmoja tu aliyekuwa akiitwa Johnson Kitchen, yeye alisema kuwa, nahodha wetu ni mtu safi sana kwani uvutaji wake wa bangi si kwa sababu ya kutukomoa sisi bali anajikinga na matukio ya ajabu ya majini.
Alisema: “Kila mmoja wetu humu ndani anaelewa kwamba, baharini kuna mambo mengi, ili uyazoee lazima utumie mbinu mbalimbali. Hata mimi natamani nianze kuvuta bangi.”
Mara simu ya upepo iliita kule juu. Nahodha ndiye aliyepiga maana kila alipotaka kuwasiliana na sisi ilibidi apige simu. Nurdin aliifuata ili kuipokea kwani ilikuwa inakaa kwenye kimeza pembeni kwa meli hivyo sisi wengine hatukujua alichokuwa akikizungumza zaidi ya kumwona akitumia mikono zaidi.
Nurdin aliongea huku sisi tukimwangalia kwa shauku ya kutaka kujua anaongea nini. Alipokata simu tulimwangalia na yeye alituangalia wote kila mmoja kwa zamu kisha akasema:
“Nahodha anauliza kama tumeona mwanga angani ulivyobadilika ghafla?”
Tiliangalia angani lakini hatukuona chochote. Kumbe kwa Nurdin hilo halikuwa zito wala kubwa. Ila kubwa akasema kuwa, alimuuliza nahodha kwa nini meli ilizimika? Akajibu haijazimika na wala haina tatizo la kuifanya izimike.
Hilo pia halikutosha, Nurdin akasema kuwa, nahodha anasema hajaja kule juu na wala hana ugomvi wa kuweza kumpiga mtu mangumi.
Tulihamaki wote na yule Johnson yeye akasema anavyomjua nahodha wetu, mbali na kuvuta sana bangi na kuwa mtemi lakini si mgomvi. Hilo wengi tuliliunga mkono na ndiyo maana tulijiuliza sana.
Basi, safari iliendelea mpaka tukafika mahali tukaona mji. Ikumbukwe hapo tulikuwa ndani ya giza nene au niseme totoro.
Nilimwambia Nurdin kuhusu mji kama ameuona akasema ameuona lakini akatoa angalizo kwamba, eneo lile halina mji kwa hiyo unaweza kuwa mji wa majini.
“Na kama si mji wa majini maana yake ni kwamba, meli yetu imepoteza mwelekeo,” alisema Nurdin.
Lakini aliniambia kuwa, meli kupoteza mwelekeo ni nadra sana au ni jambo la ajabu kwani inatembea kwa kufuata mwongozo wa ramani kama inavyokuwa kwa ndege ya abiria angani.
Tuliukaribia ule mji ambapo tukiwa sambamba nao tuliweza kubaini kwamba, shughuli mbalimbali za kijamii zilikuwa zikiendelea. Mfano, tuliona magari yakitembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine, watu wakiwa wanatembea kwa miguu na mambo mengine mbalimbali.
Hapo tulikuwa tunauona ule mji kwa kupitia madirisha kwani tulikuwa ndani ya meli.
“Nurdin unataka kuniambiaje kuhusu ule mji?” nilimuuliza.
“Si mji wa kawaida bwana Tolu. Kwanza angalia ukubwa wake. Si kama eneo la kujenga nyumba tano tu. Sasa magari yale ya nini wakati mtu anaweza kutembea kwa miguu?”
Nurdin akaniambia kwanba ili kuujua ule ni mji wa kawaida au wa majini nahodha atapiga honi.
“Ukisikia nahodha amepiga honi ujue ni mji wa majini. Nahodha wetu ndiyo tabia yake. Anapiga honi ili kama tumelala tuamke tuchungulie nje kuna kitu cha ajabu.
“Unajua manahodha wa meli hutangulia kuona mambo mengi ya ajabu. Hasa usiku, kama mchana hapigi honi kwani anajua tunaona wenyewe.”
Nurdin hakumaliza kusema tukasikia honi ‘poooo’. Mara moja tu akaacha.
Tuliupita ule mji na shughuli zake zote. Umbali wake mpaka kwenye meli ni kama nusu uwanja wa mpira na mji wenyewe pia ulikuwa na ukubwa wa uwanja wa mpira.
Kwa sababu ya uchovu wa safari ukichanganya na giza nene, tulilala usingizi mzito wa kibinadamu lakini katikati ya uzingizi tukaamshwa na mlio wa filimbi nyingine ndani ya meli yetu.
Milio ilikuwa mingi kiasi kwamba, isingekuwa rahisi tuendelee kulala. Nahodha akapiga honi mfululizo.
“Ni nini Nurdin? Hiyo milio inatokea wapi? Mbona kama inatokea humu ndani ya meli yetu?”
“Ni maajabu bwana Tolu. Miongoni mwa matukio ya baharini na maji yake na hili limo. Tuvumilie mpaka iishie yenyewe,” alisema Nurdin.
Nilitetemeka sana na kuogopa zaidi kwani wakati mwingine ile milio ilisikika mpaka kwenye masikio yangu kama vile anayepuliza filimbi alisimama pembeni yangu.
Nilimwangalia sana Nurdin nikiamini anaweza kuniambia lingine lolote kwani na yeye alionekana kuniangalia sana mimi.
Ilifka mahali Johnson akatangaza wote tuzibe masikio ili kuepuka ile milio lakini wakati akisema hayo, milio ilikoma ghafla kama vile wapulizaji walimsikia Johnson.
Je, kiliendelea nini? Usikose kusoma mkasa huu Alhamisi ijayo kwenye Gazeti la Amani.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com