×

Shosti, mdomo huo ohooo!

julianadidone3

Asalam alaikum wapenzi wasomaji wa safu. Bila shaka mu wazima na mnaendelea vema na ujenzi wa taifa letu, maana ile kauli mbiu ya Mheshimiwa Magufuli inatuhusu wote.

Mashosti, leo nina mada muhimu ya kuwapa, hasa nyie ambao mpo kwenye uchumba na wenza wenu, au tayari mzee mzima ameshakuchukua na kukupeleka kwao kukutambulisha!

Kuna tatizo, wengi wenu mkishatambulishwa kwa ndugu wa mume ndiyo wanajiona wamefika, wanasahau kuwa wanaume ni kigeugeu. Wengine huwavalisha wanawake pete za uchumba au kuwatambulisha kwa ndugu zao, wakiwa na malengo tofauti.

Hufanya hivyo ili kupata urahisi wa kukupata na kukutumia kimapenzi. Wenye tabia hizo, hutumia nafasi hiyo kutafuta udhaifu wako na wakiupata, baada ya kuwa wameshatosheka na wewe, hujifanya eti wameshindwa tabia kwa sababu tu, wewe ulichonga sana baada ya kutambulishwa au kuvishwa pete.

Sasa basi sababu ya kuandika mada hii ni kuwakumbusha nyie wanawake mlio kundi hili, mnapojisahau mnakosea sana, utakuta mwanamke anaongea sana akijua ana uhakika wa kuolewa.

Wanaume ni wepesi wa kutafuta sababu, hata kama wewe unaweza kuwa unaongea suala lenye ukweli kwa kutaka haki, yeye anao uwezo wa kukugeuzia kibao na kuona kuwa unamkera kwa maneno yako.
Ni rahisi kufanya maamuzi ya kukufanya ujione mnyonge, kama si muoaji atatumia udhaifu wako huo mdogo kukubwaga kwa sababu alichokuwa akikitaka kimeshakuwa.

Wanawake wa mtindo huu wapo wengi ambao hata kabla ya kuvishwa pete au kutambulishwa kwa waume zao, hushindwa kuwasoma vizuri na kuwajua wenza wao ni watu wa namna gani.

Unaweza kuwa na mpenzi ambaye wakati wote ni mtu wa kutafuta visingizio kama unampenda au la na huwezi kwenda kwa mwingine. Punguza mdomo ili uendane na yeye na kama unahisi huwezi kuacha, bora uachane naye ili uwe huru.

Niwageukie na nyinyi wanaume mnaopenda kuwadidimiza wanawake wanaopenda kuongea ukweli, Kumbuka kumnyamazisha mpenzi wako, kunapunguza upendo maana hata akiwa na jambo muhimu, atashindwa kwa vile atakuwa anakuogopa, kitu kitakachofanya uhuru wake kwako kupungua siku hadi siku.

Sasa jiulize mpenzi wako akishindwa kuwa huru kwako atakuwa huru kwa nani? Kila anachokifanya anashindwa kukifanya kwa uhuru kwa kukuogopa. Mwisho akimpata anayempa nafasi atakimbilia huko.
La mwisho ambalo naweza kuwaambia mnaokutana na wanawake waongeaji ni kuzingatia furaha yenu tu, jiulize je tukiwa pamoja tunaenda sawa?

Kama ukiwa naye unakuwa na furaha na hajakufanyia jambo la kukuvunja moyo, basi jali hilo mengine achana nayo kwa sababu huwezi kumbadili mwanadamu mwenzako.
Mdomo ninaouzungumzia hapa naomba ueleweke ni ule wa kutaka kuongea yale unayohisi uko sahihi, simaanishi umbeya wa kutoa maneno hapa kupeleka pale!

Leave a Comment