DODOMA:
Wabunge wa vyama vya upinzani wamesusia tena kikao cha bunge na kutoka nje ya ukumbi wa bunge jioni hii baada ya Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson kukataa hoja ya wapinzani hao iliyolitaka bunge kuacha kujadili masuala ambayo yalikuwa yakiendelea kulingana na ratiba ya bunge na badala yake kujadili suala la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliotimuliwa tangu juzi kama hoja ya dharura.
Upinzani ilikitaka kiti cha Naibu Spika kuamuru kujadiliwa kwa suala la wanafunzi kama hoja ya dharura na kulichukulia uzito wa juu kwani wametimuliwa chuo, hawana pa kwenda na wanahangaika mitaani hivyo serikali itoe mwongozo namna gani itawasaidia vijana hao.
Baada ya Naibu Spika kukataa kujadiliwa kwa swala hilo kama hoja ya dharura, aliamuru shughuli za bunge ziendelee kama ilivyopangwa na badala yake suala hilo litajadiliwa baadaye jambo ambalo wapinzani hawakukubaliana nalo ndipo wakaamua kususia bunge na kutoka nje ya ukumbi.
