Risasi Jumamosi
Mkali wa Muziki wa Dansi aliyekuwa anaunda Kundi la Mapacha Watatu, Khalid Chuma ‘Chokoraa’ anayetarajiwa kutambulishwa katika Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ Juni 4, mwaka huu amesema kuwa ingawa yeye na nguli mwenzake wa Dansi, Chaz Baba hawana maelewano mazuri lakini linapokuja suala la kupiga kazi pamoja yuko tayari.
Chokoraa aliyewahi kumshutumu Chaz ‘kuruka’ na mke wake alifungukia hilo baada ya kubanwa na gazeti hili kuwa kama Chaz akirudi Twanga Pepeta ambapo kwake ni kama nyumbani yeye atakuwa tayari kupiga naye kazi, akasema hana tatizo naye.
“Ni kweli mimi na Chaz hatuna maelewano mazuri, lakini hiyo haituzuii kupiga kazi yanapotokea mazingira yoyote ya kikazi, jambo la muhimu ni kuheshimiana na kuzingatia kile tunachotakiwa kufanya,” alisema Chokoraa.
Mkali huyo atatambulishwa kwa mara ya kwanza na Twanga leo Jumamosi katika Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni jijini Dar.
