Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpang.
Stori: Gladness Mallya, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli (JPM) kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kusoma bajeti yake kwa mwaka 2016/17 ya shilingi trilioni 29.5, mastaa mbalimbali na wasanii wa filamu na muziki Bongo, wametoa ya moyoni kuhusiana na bajeti hiyo:
“Kiukweli serikali ingeangalia vizuri kwa sababu kama ingetaka kuongeza mapato, isingeongeza kodi ya kusajili magari kwa majina binafsi mara mbili kutoka shilingi milioni tano hadi 10 kama walivyofanya. Pia kwenye usajili wa magari wasingeongeza kutoka shilingi 150,000 hadi 250,000.
“Kwa upande wangu naona bajeti haipo sawa na haijaangalia wananchi kwani ukitaka kumbadilisha mtu usimbadilishe mpaka akahisi anatoka damu.”
SINGLE MTAMBALIKE ‘RICH’ (MUIGIZAJI)
“Unajua muwamba ngoma siku zote huvutia kwake, wasanii wanaomiliki magari ni wachache sana na naona kupandishwa kwa gharama za umiliki ni kitu kidogo sana.
“Nafurahi kwa sababu bajeti imetuangalia sana wasanii kwa kutengewa bilioni tatu, ni jambo zuri kwani itatunufaisha sana wasanii. Kuhusu magari, hizo ni starehe tu cha muhimu ni sanaa yetu isonge mbele ikishaenda mbele hayo mengine yote yatakuja.”
JACOB STEPHEN ‘JB’ (MUIGIZAJI)
“Kilichonifurahisha kwenye bajeti ni suala la kudhibiti filamu za nje zinazoingia kinyemela, pia naiomba serikali itumie hizo bilioni tatu kwa ajili ya kudhibiti wezi wa kazi zetu maana ndiyo kilio kikubwa kwetu.
“Wasanii hawana tatizo la fedha za kucheza filamu bali tatizo kubwa ni wezi na soko linaloeleweka kwa jumla maana sekta ya sanaa inaajiri watu wengi kuliko sekta yoyote hivyo iangaliwe kwa makini zaidi. Kuhusu magari na vinywaji hizo ni starehe tu tena ingewezekana vingepandishwa bei zaidi ya hapo.”
SALMA JABU ‘NISHA’ (MUIGIZAJI)
“Kiukweli serikali inabidi iwatazame watu inaowatengea hiyo bajeti kwa maana inajua kabisa kilio cha kila mwananchi sasa hivi ni pesa kuwa adimu.
“Pia usafiri ni sekta muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi na mwananchi mmojammoja kwa sababu sekta hii ndiyo mahususi katika kusafirisha watu na mizigo kwa hiyo inavyopandisha gharama za umiliki na usajili itapunguza uwezekano wa watu kumiliki vyombo vya usafiri.
“Inaweza pia kuathiri pato la taifa maana kwenye usafiri huongeza pato la taifa kutokana na kodi, shughuli za walipa kodi zinazotegemea usafirishaji, bajeti hii naona ina madhara makubwa kuliko faida.”
JOKATE MWEGELO ‘KIDOTI’ (MWANAMITINDO/MUIGIZAJI)
“Yaani naunga mkono bajeti iko safi sana.”
“Bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2016/2017, kwa upande wangu naona ipo vizuri sana kwa sababu ukiangalia jinsi hizo trilioni 29.5 za bajeti zilivyogawanywa, utagundua kwamba mambo yote ya msingi yamepewa kipaumbele hasa utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo uliopewa asilimia 40 ya fedha zote.
“Hii ni dira ya kuonesha tunaelekea wapi na naamini nchi itapiga hatua kuanzia kwenye uchumi, elimu, huduma za kijamii, utalii na sanaa kwa jumla.


