ASALAAM aleikum ndugu zangu Waislamu. Ni Jumamosi nyingine Mungu ametujalia uzima. Chungu cha tano leo, inshaallaah Mungu awe nanyi mmalize mfungo salama.
Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita, nilizungumza zaidi na wanawake. Nilisema kwamba, kuna vitu mwanamke anapaswa kuviacha wakati anaingia kwenye ndoa. Nilimaanisha kwamba endapo mwanamke ataendelea na desturi zilezile alizokuwa nazo kabla hajaingia kwenye ndoa ni rahisi sana kuivunja ndoa yake.
Kwa wale mliobahatika kuisoma safu hii, bila shaka mlijifunza vitu vingi. Kupitia meseji zenu, nimeona jinsi gani mmepata elimu. Nina imani hata katika mada ya leo yenye kichwa cha habari kilichopo hapo juu, mtajifunza mambo mengi ya msingi.
Nilisema mke haupaswi kuingia kwenye ndoa ukafanya vitu vya mzaha. Mfano kuruhusu marafiki zako waindeshe ndoa yako. Kuiga aina ya maisha wanayoishi. Mawasiliano yako na wanaume ambao ni marafiki zako wa kawaida yanapaswa kuwa ya staha. Ujiheshimu.
Leo nataka tujifunze kuhusu suala la mtu kumdhuru ampendaye. Kibinadamu, unaposikia mtu kamkata binadamu mwenzake panga, kamchoma kisu, kampa sumu huwa tunapata ukakasi kuliingiza akilini tukio hilo.
Katika ulimwengu wa mapenzi, matukio kama hayo yanatokea. Mtu anamdhuru mpenzi wake kwa kisu, panga au hata sumu. Unajiuliza kwa nini afanye hivyo? Utu wake unakuwa wapi? Kweli binadamu mwenzako unaweza kumfanyia tendo la kinyama kiasi hicho?
Haiingii akilini kusikia mtu amekamata kisu. Lazima uhoji, mtu anapata wapi ujasiri wa kumvaa mchumba au mkewe na kumchoma shingoni au tumboni? Tena ukizingatia kwa wewe ambaye upo katika uhusiano mzuri, ukielezwa au kushuhuduia tukio hilo, unaona ni kama sinema vile.
Huamini. Wakati huo moyo wako unaongozwa na fikra za kibinadamu. Unaamini kwamba ni vigumu sana mtu kuthubutu kufanya tukio la kinyama kama hilo. Utamlaani aliyefanya ukiamini si binadamu wa kawaida.
Utamlaani ukiamini huenda ana upungufu wa akili. Ni rahisi kumfikiria kuwa labda ana mapepo. Hapo ndipo pia zinapoibuka imani za kishirikina. Utasikia pengine kamuua mke au mchumba wake ili apate utajiri.
Mawazo hayo yanamzunguka mwanadamu kwa kuwa haingii akilini kusikia mtu anamdhuru ampendaye. Lakini ukweli ni kwamba matukio ya namna hii yapo mengi kwa sasa. Suala la msingi hapa ni kujiuliza kwa nini huwa yanatokea?
Marafiki zangu hapa yatupasa kwa pamoja tujifunze. Matukio kama haya hayatokei hivihivi tu, lazima kuwe na sababu. Kila anayefanya tukio hilo ukimuuliza kwa makini huwa anakuwa na simulizi yake.
Hafanyi tu kwa sababu ana roho ya kinyama. Anasukumwa na msongo wa mambo mengi anayopitia katika maisha yake. Anashindwa kuhimili hasira. Kuna ambao wapenzi wao wanasaliti. Si tu kusaliti, anafikia hatua ya kupata mimba na mwanaume nje ya ndoa.
Mwenzake anahoji. Haoneshi kushtushwa na habari hiyo. Haoneshi kujutia. Anamtambia mumewe. Anamfanyia kejeli. Anamuoneshea kwamba yeye si lolote si chochote. Anamdhalilisha kwa mashoga zake. Anampakazia kwamba pengine mumewe hana uwezo wa kupata mtoto.
Mwanaume anadumu na maumivu hayo kwa muda mrefu. Uvumilivu wa kibinadamu unamshinda, pasipo kujijua anajikuta ametenda unyama ambao hata yeye baadaye akitafakari anagundua hakufanya uamuzi sahihi.
Huo ni mfano mmoja lakini kuna vitu vingi vizito ambavyo vinafanana na hivyo. Kutokana na imani kuwa ndogo, mtu hujikuta amefanya tukio zito ambalo matokeo yake huwa ni majuto.
NINI CHA KUFANYA?
Tangu awali, kama humpendi mtu, usithubutu kumdanganya. Mpende mwenzako kutoka moyoni. Usiigize. Usimsaliti. Mtangulizeni Mungu katika kila jambo. Muogopeni yeye. Mumuombe awasimamie katika safari yenu. Muombeni baraka zake kila wakati.
Muwe na upendo wa dhati. Muombeni awasaidie kuwaepusha na balaa. Kwa msaada wake, mtaaminiana, mtaheshimiana na mtaishi kwa raha mustarehe.
Tukutane wiki ijayo!