Makala: Boniface Ngumije
WACHACHE sana wanaofuatilia muziki wa Bongo watakuwa hawamuelewi nini anafanya huyu jamaa, maana ni habari ya mjini. Anaitwa George Mdeme ‘G Nako,’ mmoja wa wasanii wanaotoka katika Kampuni ya Weusi ambayo pia wamo Joh Makini, Niki wa Pili na Bonta. Hivi karibuni G Nako alitambulisha ngoma yake mpya iitwayo Alosto, inayotamba kwenye media mbalimbali na katika ‘exclusive interview’ na Risasi Vibes, mkali huyu amefunguka mambo kibao kama ifuatavyo;
Risasi Vibes: Kwanza bila shaka mashabiki wako wangependa kufahamu kiundani kwa nini video ya wimbo wako wa Alosto uliifanya mara mbili.
G Nako: Oke! Naomba waelewe tu kuwa mwanzoni nilipofanya na Nisher, sikupata kile ambacho nilikuwa nakihitaji. Video haikunivutia ndiyo maana nikaamua kurudia na Hanscana tuliyetoa kichupa kikali. Lakini sababu ya pili, nilipomaliza tu kufanya ile video na Nisher hata kabla sijaitambulisha rasmi kwenye media ilivuja, so suala hilo pia halikunipendeza.
Risasi Vibes: Ilivujia wapi, mikononi kwako au kwa Nisher? Na kama ni kwa Nisher hatua gani ulimchukulia?
G Nako: Haikuvujia mikononi kwangu. Baada ya kugundua kuwa imevuja, nilimcheki Nisher nikamuuliza nini kimetokea akadai hafahamu. So sikupenda kufanya suala hilo liwe kubwa sana kwa sababu haya mambo ya ngoma kuvuja na nini mimi ninayaelewa freshi. Ndiyo maana niliamua kuchukua hatua zingine.
Risasi Vibes: Miaka ya hivi karibuni wewe na timu yako ya Weusi hasa Joh Makini mmekuwa mkifanya video zenu nje ya nchi, sababu gani zimefanya Alosto ‘uigongee’ nchini?
G Nako: Kushuti video nje inategemea mtu unakuwa unahitaji nini!
Lakini ikiwa kile unachokihitaji kwenye video yako unaweza kukipata ndani kwa nini uhangaike? Hivyo ndivyo ilivyotokea kwenye video yangu.
Risasi Vibes: Sawa, hivi nini ugumu na urahisi wa kusambaza video iliyoshutiwa nje ya nchi au ndani?
G Nako: Niwe tu muwazi, msanii anaposhutia video yake nje hasa kwa madairekta maarufu anakuwa na ‘access’ kubwa ya kuitangaza ngoma yake. Kwanza kwa kutumia ‘network’ ya huyo dairekta lakini pia ya msanii mwenyewe. Lakini ndani video inakuwa haipai sana kwa maana hata madairekta wetu wanakuwa hawana mtandao mkubwa.
Risasi Vibes: Naona mashavu yanaongezeka kwa sasa, waambie wasomaji kama kuna shavu lolote la ubalozi umekula au umewahi kula?
G Nako: Ha haaa! Ni kweli ninamshukuru Mungu mambo si mabaya. Ila sijawahi kuwa balozi wa shirika wala kampuni yoyote ile japo ninafanya kazi za matangazo na kampuni kubwa tu Bongo. Risasi Vibes: Kampuni ya Weusi inahusikaje kwa kazi za msanii mmojammoja?
G Nako: Kuna mpangilio tu, nani anafanya na kwa wakati gani! Unafika wakat wa msanii husika kampuni inasimamia mwanzo mwisho, kuanzia audio mpaka video.
Risasi Vibes: Kumekuwa na utata kwa baadhi ya watu juu ya kiongozi wa Weusi. Wapo wanaosema Joh wengine Bonta na wengine Nicki! Ukweli ni upi?
G Nako: Sitapenda kuzungumzia sana masuala ya kampuni ni vyema ayazungumzie Niki maana ndiye msemaji wa kampuni yetu. So kuna masuala ambayo pengine kampuni haitaki kuyaweka wazi au vipi, so yule ana majibu ya maswali yote kuhusu Weusi.
Risasi Vibes: Moja ya ‘technique’ ya wasanii kwa sasa ni kufanya ngoma na wasanii wakali kutoka nje ili kuishibisha ‘fun base’ yao. Kwako mipango imekaaje?
G Nako: Mipango yangu kiukweli ni ngumu kumeza. Ninamaanisha nina mipango mirefu sana ya kufanya kazi na wasanii wakubwa Afrika. Kwa sasa kuna msanii niko katika maongezi naye na mambo yakienda sawa kila kitu nitakianika. Ninafahamu itakuwa ‘suprise’ ambayo haijawahi kutokea Tanzania maana ni kitu kikubwa sana.
Risasi Vibes: Unachota kiasi gani cha pesa kupitia mauzo ya mitandaoni na kwenye miito ya simu kwa ngoma moja?
G Nako: Si rahisi kufahamu hilo maana utaratibu mauzo hukusanywa ngoma zote za msanii ambazo umeziwakilisha kwenye mtandao husika na kuuzwa.
Sasa unapofika wakati fulani unakwenda kuchota pesa za mauzo ya jumla.
Risasi Vibes: Kwa upande wa matamasha, unapokuwa na shavu nje ya kampuni utaratibu unakuaje?
G Nako: Kampuni haibani, maana tofauti na kampuni kila msanii ana kazi zake binafsi, sasa inapotokea hivyo huwa ninaweka wazi kwenye uongozi na kupewa ‘go ahead’.
Risasi Vibes: Vipi mzee, unalipa kodi?
G Nako: Ndiyo ‘why not?’ Nalipa kodi hasa ninapoandaa matamasha yangu mwenyewe lakini pia kiasi cha pesa ninachopokea kwenye miito ya simu huwa kinakatwa.
Risasi Vibes: G, tuishie hapa kwa leo, kama una lolote waachie mashabiki zako. G. Nako: Aaah, ninawashukuru kwa sapoti yao.
