MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu? Leo tunaye Mshindi wa Bongo Star Search 2015 (BSS), Kayumba Juma anayeishi Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar.
Mwanamuziki huyo ambaye ni zao la Mkubwa Fella, bado mpaka hivi sasa yuko mikononi mwake.
Aliipokea Mpaka Home kwa heshima zote hivyo fuatana nami hapa chini uweze kujua mengi kutoka kwake.
Mpaka Home: Habari Kayumba naona umejituliza nyumbani kwako, vipi hupendi kutembeatembea?
Kayumba: Napenda zaidi kutulia nyumbani.
Mpaka Home: Hapa ndipo ulikuwa ukiishi kabla hujashinda Bongo Star Search?
Kayumba: Mara nyingi sana maskani yangu yalikuwa huku lakini niliposhinda nimehamia kabisa.
Mpaka Home: Ratiba yako ya siku nzima ikoje?
Kayumba: Mara nyingi naamka mapema sana kwa ajili ya kufanya mazoezi ya sauti kisha nafungua kinywa na chai peke yake sipendi vitafunwa.
Mpaka Home: Kuna tofauti gani kabla hujawa maarufu na sasa?
Kayumba: Tofauti ni kubwa sana mwanzo nilikuwa siheshimiwi lakini sasa hivi heshima ni kubwa sana.
Mpaka Home: Ni mgeni wa aina gani unapendelea aje nyumbani kwako?
Kayumba: Sipendi ambaye hana sababu maalum ya kuja kwangu, nafurahi sana kama ulivyonitembelea kwani una kazi maalum.
Mpaka Home: Kuna siku ulishawahi kulala bila kula?
Kayumba: Sana tu, kwa vijana kama mimi hilo hutokea.
Mpaka Home: Nini ambacho hukipendi katika maisha yako?
Kayumba: Sipendi mtu anikatishe tamaa.
Mpaka Home: Ukifanikiwa kuwa na nyumba yako unapenda uweke nini?
Mpaka Home: Kupanda miti na bustani nzuri ya maua.
Mpaka Home: Asante sana Kayumba.
Kayumba: Karibu sana dada yangu.