Baada ya wiki iliyopita kuwa na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum aliyefafanua mengi kuhusiana na Dini ya Kiislam hasa katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, leo tunawaletea mahojiano yaliyofanywa hivi karibuni na Wahariri Wetu Elvan Stambuli, Sifael Paul na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba yaliyofanyika ofisini kwake Kijitonyama, Dar ambayo yalikuwa kama ifuatavyo;
Kwanza kabisa tunaomba uelimishe wasomaji wetu, nini kazi ya kituo hiki cha Sheria na Haki za Binadamu?
Jibu: Kazi yake ni kukuza uelewa wa haki za binadamu na sheria mbalimbali. Watu wanatakiwa kuelewa kuwa haki haziwezi kupatikana bila kuzidai, tuna jukumu la kuwaambia watoa haki watoe haki. Pia huwa tunatoa msaada wa kisheria kwa watu wenye kuhitaji, tunajenga uwezo wa watu kujua haki zao ndiyo maana elimu hiyo tunaitoa kwa kila wilaya nchi nzima.
Je, kituo hiki kina matawi yoyote nchini? Na kama yapo ni katika mikoa au wilaya zipi?
JIBU: Tuna tawi moja tu la Arusha. Lakini karibu wilaya zote nchini tuna wasaidizi wa kisheria wanafanya kazi hizo na kuandaa mashirika au taasisi za kushughulika na sheria, hasa kusimamia haki na kwa miaka kadhaa sasa neno haki linafahamika na watu wengi, hii ni kwa sababu yetu.
Hivi sasa kuna amri ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ya kukataza mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa mujibu wake, mpaka mwaka 2020, hilo unalizungumziaje, kuna haki hapo?
JIBU: Kwanza nikitafakari naona kama rais alikuwa akitania. Nasema hivyo kwa sababu haiwezekani mtu ambaye ameapa kuilinda katiba akawa wa kwanza kuikiuka. Rais anatakiwa kufuata katiba na aelewe kwamba hivi sasa nchi ipo kwenye mfumo wa vyama vingi. Viongozi wa vyama vya siasa ni lazima watumie mikutano ya hadhara kuwashawishi watu kuingia kwenye vyama vyao. Rais lazima ajue kwamba siasa ni kazi kama kazi nyingine. Kuna watu wanategemea siasa katika maisha yao. Tuliona jinsi Kinana (Abdulrahmana Kinana ni katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi -CCM), alivyozunguka nchi nzima kuwashawishi wananchi na kufungua na kujenga mashina ya chama chake. Rais anataka watu wafanye kazi lakini asizuie wengine kufanya kazi, wapo ambapo siasa kwao ni kila kitu. Sijui anatafsiri vipi siasa ambayo ni maisha, vyama ni muhimu kwao kukutana kila mara ili kuvijenga.
Kuna hili suala la wafungwa kuhukumiwa na mahakama kunyongwa lakini hawanyongwi wala kubadilishiwa adhabu, taasisi yako inasemaje?
JIBU: Sheri hiyo ibadilishwe na adhabu ya kunyongwa hadi kufa ifutwe kwa sababu inakiuka haki za binadamu. Kwanza hapa nchini haitekelezwi na inawafanya waliohukumiwa kunyongwa kuishi kwa wasiwasi wakati wote gereza kwani hawajui watanyongwa lini. Kuna baadhi ya watu huwa hatuelewi tunaposema hivyo, lakini tunachotetea sisi ni thamani ya utu na uhai kutolewa bila kujali nani anayetoa uhai huo. Uhai wa binadamu ni lazima ulindwe ni vema badala ya mtu kuhukumiwa kunyongwa, apewe kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa watu watakaokuwa wanamuona akitumikia kifungo hicho, kumuua mkosaji ni sawa na kutenda kosa lilelile alilotenda. Kuna baadhi ya nchi mkosaji wa mauaji anahukumiwa kifungo cha maisha lakini kinakua na miaka inayotajwa, Baadhi ya nchi sheria zao zinatamka miaka ya kukaa jela kama ni miaka 20, 30 na kadhalika. Nashauri waliohukumiwa kunyongwa rais abadilishe hukumu hizo iwe kifungo cha maisha.
Kuna malalamiko kwamba baadhi ya wananchi huwa wanauawa wakiwa kwenye mikono ya polisi hivyo kuvunja haki za binadamu, je unaweza kueleza msimamo wa kituo chako kuhusiana na jambo hili?
JIBU: Ni kweli tumeona au kusikia watu wamefariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi, wanajeshi au askari wa wanyamapori. Yapo mauaji yanayotokea kutokana na askari kujikinga, au kuzuia wengine wasiuawe, au kwa kutunza mali fulani na kadhalika, hayo ni mauaji ya kisheria.
Lakini mauaji hayo ni lazima yachunguzwe na yasiishie kusema tu sababu bila kufanyika utafiti wa kutosha, watu watalalamika na ni lazima ripoti ya uchunguzi huo iwekwe hadharani. Bila ripoti ya uchunguzi watu watasema askari wameua. Na ripoti hiyo itasema wazi kama risasi zilipigwa kifuani, itaonesha na kama ni mgongoni pia zinaonesha na wachunguzi watajua.
Wiki ijayo atazungumzia kuhusu mvutano wa CCM na CUF Zanzibar, tatizo la mauaji ya albino na mengine mengi. Usikose nakala yako.

