NGOMA ya mkali wa Bongo Fleva nchini, Abedinego Damian ‘Belle 9’ iitwayo Burger Movie Selfie ni kati ya ngoma zilizomtambulisha kivingine kwenye tasnia ya Muziki wa Bongo Fleva, ambapo mbali na mshikaji huyo kuwaonesha mashabiki wa muziki nchini kuwa anaweza kudondoka katika mdundo wa aina yoyote, ngoma hiyo ilipata mafanikio kiasi cha kuchezwa kwenye vituo vya televisheni vikubwa barani Afrika.
Kuhusu ngoma hiyo Belle 9 anasema imekuwa daraja la kumfikisha kwenye levo zingine za kazi yake kwa sababu hataki kurudi nyuma, amepania kupiga hatua nyingine kutoka alipo. Katika makala haya anafunguka sababu iliyomfanya aifanyie remix ngoma hiyo na kwa nini aliamua kuwashirikisha Izzo Buzness, Mr Blue, G Nako, Jux na Maua Sama.
Uwazi Showbiz: Nini hasa kilisababisha kufanya remix ya Burger Movie Selfie?
Belle 9: Mashabiki ndiyo sababu. Tangu nimeachia ngoma hii miluzi ilikuwa mingi, mashabiki wa ndani na nje, watu wangu wa karibu na baadhi ya wasanii wenzangu waliomba niifanyie remix na kuwashirikisha wasanii wakali ili kuongeza hadhi ya ngoma yenyewe kwa sababu ni ya kimataifa.
Uwazi Showbiz: Baada ya kupewa wazo hilo na kulipitisha, ulitumia vigezo gani katika kuwashirikisha wasanii ulioimba nao?
Belle 9: Nilizingatia sana swaga. Wasanii wanaoweza ni wengi sana, lakini jambo la muhimu nilikuwa ninatazama nani mwenye swaga za kuendana na wimbo. Nikamuwaza Izzo, nikaamua kumpa nafasi kwa sababu ni mtu ambaye nina ukubali muziki wake. Mr Blue nishafanya naye kazi na ikafanya vizuri, kwa hiyo nikaona anafaa pia kuingia. Jux, swaga zake ni ameizing na wengine wote waliosikika ni kwa sababu ninawakubali.
Uwazi Showbiz: Mbali na hao kuna msanii uliyetamani awe ndani na ukamtafuta lakini hakuweza kufanya kutokana na sababu zozote zile?
Belle 9: Hapana ni hao niliowawaza na wote walifanikiwa kurekodi.
Uwazi Showbiz: Nani ulikuwa wa kwanza kumtafuta?
Belle 9: Izzo Buzness, lakini wa kwanza kuingiza sauti ni Jux.
Uwazi Showbiz: Imechukua muda gani katika maandalizi kuanzia ulipowashirikisha idea wasanii hao?
Belle 9: Kama wiki moja tu hivi.
Uwazi Showbiz: Original yake ulifanyia kwa Tiddy Hotter na kichupa ukapiga kwa GQ, lakini sasa tumeona kichupa umebadilisha kwa kugonga na Enos Orik wa Kenya, nini sababu hasa?
Belle 9: Nilikuwa siriasi na kile ninachokifanya, sikuona sababu ya kulegeza kwa kuwa nilikwishaamua kufanya kitu fulani cha tofauti.
Uwazi Showbiz: Wasanii uliowashirikisha uliwalipa?
Belle 9: Tunamakubaliano maalum ambayo sipendi kuyaweka wazi kwa sasa.
Uwazi Showbiz: Kuna changamoto yoyote ulikutana nayo katika maandalizi?
Belle 9: Hakuna, kila kitu kilienda sawa katika muda muafaka.
Uwazi Showbiz: Una lolote kwa mashabiki?
Belle 9: Waendelee kunipa sapoti.
