Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
BENDI kongwe ya Muziki wa Dansi, The African Stars ‘Twanga Pepeta’, inatarajiwa kusindikiza shindano la kumsaka Miss Tabata 2016 litakalofanyika Julai 22, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Dar West Park, Tabata jijini Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, mratibu wa shindano hilo, Joseph Kapinga, alisema kuwa warembo 38 wanaendelea na mazoezi kujiandaa na shindano hilo linaloandaliwa na Keen Arts na Bob Entertainment.
“Tunatarajia kufanya mchujo kubaki na warembo 16 watakaopanda jukwaani siku hiyo ya Julai 22 wakisindikizwa na Bendi ya Twanga Pepeta chini ya Ali Chocky,” alisema Kapinga.
Naye Mkurugenzi wa shindano hilo ambaye pia ni mkuu wa kambi, Godfrey Kalinga alisema warembo watakaoshiriki kwenye fainali watatembelea mbuga za wanyama ili kupromoti utalii wa ndani.
“Washiriki watano watakaoshika nafasi za juu watashiriki kwenye shindano la Kanda ya Ilala yaani Miss Ilala na baadaye Miss Tanzania,” alisema Kalinga.
Miss Tabata inadhaminiwa na Lete Raha, DataStar College, Global Publishers, CXC Africa, Fredito Entertainment, Saluti5, Kitwe General Traders na Bob Entertainment.
