Sweetbert Lukonge,
Dar es Salaam
KIKOSI cha Yanga, kesho kitashuka uwanjani kusaka ushindi wake wa kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kitakapopambana na Medeama ya Ghana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm anatarajiwa kuanzisha washambuliaji watatu ili kuhakikisha anapata ushindi utakaofufua matumaini ya timu hiyo kusonga mbele kwenye hatua nyingine ya michuano hiyo.
Washambuliaji hao ni Mzimbabwe, Donald Ngoma, Amissi Tambwe ambaye ni raia wa Burundi pamoja na Obrey Chirwa kutoka Zambia.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, Pluijm amefikia hatua hiyo ili kuhakikisha anapata ushindi katika mchezo huo ili kikosi chake hicho kiweze kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo, kwani mpaka sasa kina hali mbaya kutokana na matokeo mabaya kiliyopata dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo na MO Bejaia ya Algeria.
“Mpaka hapa tulipofikia maandalizi yetu naweza kusema yamekamilika na tunachosubiri ni mchezo huo tu ili tuweze kutimiza malengo yetu ya kuhakikisha tunashinda.
“Hata hivyo, kocha anatarajia kuwaanzisha washambuliaji wetu wote watatu wa kimataifa katika mchezo huo ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” kilisema chanzo cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Pluijm hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai: “Kila kitu kitajulikana siku hiyo ya mechi lakini maandalizi yetu yanaenda vizuri na ninashukuru kwa hilo.”
Aidha, katika mazoezi ya jana ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Yanga ilipata ugeni wa ghafla ambapo baadhi ya wanachama na viongozi wake wenye uwezo mkubwa wa kifedha walifika uwanjani hapo kushuhudia na muda mwingi wakionekana wakipanga mipango ambayo hawakuruhusu waandishi kusogea kuwasikiliza, baadhi yao ni Abdallah Bin Kleb, Ndama mtoto ya Ng’ombe, Isaac Chanji na Mustapha Ulongo.

