KIJANA mmoja aliyekuwa na kisu na shoka amewashambulia abiria waliokuwa kwenye treni huko Kusini mwa nchi ya Ujerumani jana usiku na kuwajeruhi watu wanne.
Kijana huyo baadaye alipigwa risasi na Polisi na kufa alipokuwa akikimbia baada ya tukio hilo.

Polisi wa mjini Wuerzburg wameeleza kwenye ukurasa wao wa Facebook kuwa abiria watatu wamejeruhiwa vibaya na wengine 14 wanapata msaada wa kitabibu kutokana na mshtuko walioupata.
Polisi wamesema bado hakuna taarifa yeyote kuhusu sababu ya kutekelezwa kwa shambulio hilo.

vyombo vya habari vya Ujerumani vimemnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya ndani mjini Bavaria kuwa mtu huyo ni mvulana wa miaka 17, mkimbizi mwenye asili ya Afghanistan.

Kabla ya kushambulia treni, kijana huyo alisikika akiongea kwa sauti ‘Allahu Akbar’ na uchunguzi uliofanywa umebaini bendera iliyochorwa kwa mkono kwenye chumba chake.

