×

Ripoti Kamili… Ukweli Kuhusu Maiti Zinazozikwa na Manispaa-2

makaburiNa Hashim Aziz

Wiki iliyopita, tulianza kukuletea ripoti kamili ya maiti zinazozikwa na manispaa ambapo mwandishi wetu alikuwa akifanya mahojiano na Afisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Mathias Nemes Kapizo ambaye alieleza mambo mbalimbali. Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mahojiano naye.

KUHUSU UDHALILISHAJI WA MAITI

Swali: Yapo madai kwamba maiti zisizo na ndugu huzikwa zaidi ya moja kwenye kaburi moja na wakati mwingine, nyingine hukatwa miguu au mikono ili zote ziingie kwenye kaburi moja. Unalizungumziaje hili?

Kapizo: Hakuna kitu kama hicho hata kidogo. Hao wanaozusha maneno hayo, wanapaswa kupimwa akili zao. Ndugu mwandishi, mfano mwepesi tu, huko barabarani si kila siku huwa unaona mizoga ya wanyama kama mbwa na wengine? Je, umewahi kuona mzoga wa mbwa unakatwa miguu kisha ndiyo unafukiwa?

Kama huwezi kufanya hivyo kwenye mzoga wa mbwa, unawezaje kufanya kwa binadamu? Hii kazi huwa inaongozwa na ethics (miiko) na inahitaji sana mtu mwenye wito. Nakuhakikishia kwamba maneno hayo ni uzushi unaopaswa kukemewa kwa nguvu, sisi kazi yetu ni kuwasitiri na kuwahifadhi kwa upendo mkubwa maiti ambao wamekataliwa hata na ndugu zao.

Huwa maiti zinaoshwa vizuri, kuvalishwa sanda na kama tukigundua kama alikuwa ni muumini wa dini gani, anazikwa kulingana na imani yake na kama isipofahamika dini, anazikwa kawaida lakini kwa heshima zote anazopaswa kupewa.

Hao wanaoeneza maneno hayo, nani amewahi kushuhudia? Kwa sababu huwa hatuziki usiku, mazishi yanafanyika mchana na kila mtu anaona. Walete uthibitisho.

NDUGU WAKIPATIKANA BAADA YA MAZISHI, NINI HUFANYIKA?

Swali: Kwa mfano mkimzika maiti kwa kuamini kwamba hana ndugu halafu siku chache baadaye ndugu zake wakajitokeza, nini huwa kinafanyika?

Kapizo: Matukio ya namna hiyo huwa yanatokea sana. Ikitokea hivyo, wale ndugu tunawaelekeza kufuata taratibu zote za kisheria, ikiwa ni pamoja na kupitia polisi, kupata kibali, kwenda kwenye hospitali aliyokuwa amelazwa na kuthibitisha kama wanamfahamu, kwenda pia Ustawi wa Jamii kisha kwa pamoja ndiyo wanakuja kwetu wakiwa na vielelezo vyote.

Wakija kwetu, wakiwa na hao maafisa wa ngazi zote nilizozitaja hapo juu, huwa tunafuatilia taarifa za maiti wanayemzungumzia na kufananisha na zetu kisha tunagundua kwamba tulimzika kwenye makaburi gani na siku gani maana huwa tunatunza vizuri kumbukumbu.

Baada ya hapo, timu nzima huwa inakwenda mpaka kwenye kaburi alilozikwa ambapo taratibu za kisheria na kiafya za kufukua kaburi huwa zinafuatwa, maiti ikitolewa inapimwa DNA na kufananishwa na hao ndugu na ikithibitika ni kweli, huwa tunaiandaa upya na kuwawekea kwenye jeneza kwa ajili ya kwenda kufanya mazishi upya. Hata kama maiti imebaki mifupa, huwa tunafuata taratibu hizohizo.

Swali: Nani huwa anagharamia zoezi hilo la ufukuaji wa maiti iliyozikwa?

Kapizo: Kimsingi sisi kazi yetu huwa inaishi pale maiti inapozikwa kwa hiyo ikitokea ndugu wamepatikana, wao ndiyo wanaotakiwa kugharamia kufukua kaburi. Sisi huwa tunawasaidia tu.

HUWA MNAWAZIKA KWENYE MAKABURI YA WAPI?

Swali: Zipo taarifa kwamba makaburi mengi yaliyopo mijini yamejaa. Huwa mnawazika wapi maiti waliokosa ndugu?

Kapizo: Huwa napingana sana na hiyo dhana kwamba makaburi yanaweza kujaa. Maeneo ya kujenga nyumba ndiyo yanaweza kujaa lakini makaburi hayajai kwa sababu hakuna maiti anayeweza kumlalamikia mwenzake kwamba kwa nini wewe umezikwa pembeni yangu (anacheka).

Hata hivyo, ili kupunguza msongamano, huwa tunakwenda kuzika kwenye makaburi ya Kwa Kopa, Mwananyamala, Tegeta na Mabwepande ambako tuna eneo kubwa lenye nafasi ya kuzika zaidi ya watu 20,000.

TUKIO AMBALO HAWEZI KULISAHAU

Swali: Tangu uanze kazi hii ni tukio gani ambalo huwezi kulisahau?

Kapizo: Yapo mengi kwa sababu kama nilivyosema, nimefanya kazi hii kwa zaidi ya miaka 36. Tukio ambalo huwa nalikumbuka zaidi ni lile lililotokea miaka kadhaa iliyopita la watu kuzusha uvumi kwamba maiti ya Muislam iliyokuwa imezikwa kwenye makaburi ya Wakristo, imefukuliwa na mifupa yake kutupwa makaburini Wakristo wakishinikiza ikazikwe kwenye makaburi ya Waislam.

Nakumbuka taarifa hizo ziligusa hisia za watu wengi sana, ikawa zogo kubwa, Waislam wakataka kuja juu. Nikiwa safarini kuelekea Dodoma nilipigiwa simu na uongozi wa juu, nikalazimika kurudi mpaka Makaburi ya Mwananyamala lakini nilipofika, niligundua kwamba ulikuwa ni uzushi, hakukuwa na maiti iliyofukuliwa wala tukio kama hilo ndiyo watu wakatulia. Kama ingekuwa kweli ingekuwa hatari sana, watu walishapandwa na jazba.

NENO LA MWISHO

Swali: Una neno gani la mwisho la kuwaambia wasomaji?

Kapizo: Nashukuru, naomba watu waache kuzusha mambo na kujenga imani potofu kuhusu maiti, makaburi na sisi watu tunaoshughulikia maiti. Wengine wanaogopa hata kuishi jirani na makaburi, mtu akishakufa hana madhara kabisa. Pia tunaomba serikali itusaidie kupata vifaa vya kutosha na kutoa motisha kwa vijana ili wajitokeze kwa wingi kujiunga na hii kazi.

Leave a Comment