×

Mgonjwa afa nje ya Zahanati

Watu-4-washikiliwa-na-polisi-mkoani-MANYARA-TBC-April-16-2015DAR ES SALAAM: Mwanamke mmoja mgonjwa ambaye hakufahamika jina lake mara moja, amefariki akiwa nje ya Zahanati ya Tandale jijini Dar na kuzua balaa kubwa miongoni mwa wananchi, Amani limesheheni mkasa mzima.

Kwa mujibu wa mashuhuda, mwanamke huyo alifika katika Zahanati hiyo ili apatiwe matibabu, Jumapili jioni, lakini inadaiwa kuwa alikosa huduma hiyo kwa kuwa hakuwa na fedha. Badala ya kuondoka kwenda sehemu nyingine au kurudi nyumbani, inadaiwa mgonjwa huyo alijilaza nje huku akiugulia maumivu.

Kesho yake ilibainika kuwa mwanamke huyo alikuwa ameshapoteza maisha, hivyo wahudumu wa zahanati hiyo wakataka kuuchukua mwili wake wapate kuuhifadhi vizuri. Jambo hilo lilizua balaa kubwa baada ya baadhi ya wananchi kuwajia juu, wakiwalaumu kwa kusababisha kifo chake kwa uzembe.

“Jamani kilichotokea hapa Zahanati ya Tandale, kama polisi wasingeingilia kati sijui ingekuwaje? Kuna dada alifika hapa Jumapili jioni kwa lengo la kutibiwa lakini wakashindwa kumpa ushirikiano kwa vile hakuwa na pesa hata ile elfu mbili ya kadi, matokeo yake umauti ndo ukamkumba siku iliyofuata,” alisema shuhuda wetu.

Baada ya kupata taarifa hizo, paparazi wetu alifika kwenye zahanati hiyo, lakini katika hali ya kushangaza, wahudumu hao waligoma kutoa ushirikiano kwa madai kuwa hawawezi kuzungumzia suala hilo mpaka wapate kibali kutoka uongozi wa juu ambao haukuwepo muda huo.

Gazeti hili lilifanikiwa kuongea na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Kassim Omar ambaye alikiri kupata taarifa za mgonjwa huyo mapema kabla hajafariki na aliahidi kumsaidia.

“Asubuhi alipita dereva wa Bajaj akaniambia hapa kuna dada kalala anaumwa, alipofika hospitali Jumapili akapewa uhamisho wa kwenda kutibiwa Mwananyamala akiwa ameongozana na kijana mmoja, kwa kuwa hakuwa na pesa ya kwenda huko, yule mwenzake akamwambia amsubiri pale akachukue pesa.

“Matokeo yake hakurudi, ikabidi yule dada alale palepale zinapopaki Bajaj, aliponielezea vile nikamwambia naenda kwanza kufungua ofisi halafu nirudi kumsaidia ndipo nikakuta ameshafariki, sasa maneno ya kutopewa ushirikiano hadi watu wakaanza kufanya fujo ni ya wananchi, ila mimi nimethibitisha hapa alipokelewa vizuri,” aliongeza.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alipoulizwa kuhusu taarifa za kifo hicho, alisema; “Ninachojua mimi, huyo marehemu alitibiwa, ilipofika hatua ya kupewa dawa akawa hana pesa, ndipo akakaa eneo la Bajaj hadi alipofariki dunia. Lakini naendelea kufuatilia.”

Leave a Comment