Wiki hii tunaye mwanadada anayefanya poa kwenye filamu Bongo, Shamsa Ford ambaye amepigwa maswali 1O na Mwandishi Wetu Gabriel Ng’osha. Unataka kujua kaulizwa nini akajibu vipi? Fuatilia hapa chini…
Ijumaa: Unaonekana uko kimya sana, mambo ya kufyatua filamu vipi?
Shamsa: Mambo yanaenda fresh, mipango inaendelea chini kwa chini na siku si nyingi vitu vizuri vitaonekana.
Ijumaa: Soko la filamu linaonekana kuyumba kiasi cha baadhi kugeukia kazi nyingine, unadhani sababu ni nini hasa?
Shamsa: Kikubwa kuangalia wapi tunakosea na naamini bado tunaweza kurudisha heshima ya filamu zetu na kuwa kama zamani.
Ijumaa: Tangu umeachana na Nay wa Mitego, uhusiano wako wa kimapenzi umekuwa wa siri sana, umeamua kuwa singo au una-date kimyakimya?
Shamsa: Nipo na mtu ila siyo staa na wakati wa kumuweka wazi ukifika nitafanya hivyo.
Ijumaa: Au ndiyo yule Chid Mapenzi ambaye mara kwa mara mmekuwa mkionekana pamoja kimalovee?
Shamsa: Hapana, sina uhusiano na Chid Mapenzi, yule ni mshikaji wangu na tunashirikiana katika biashara.
Ijumaa: Umesema mpenzi wako wala siyo staa, kwa nini umeamua hivyo wakati uliwahi kusema kutoka na staa mwenzako kuna raha yake?
Shamsa: Nimegundua kuwa uki-date na staa ni kero, unafuatiliwa sana, kitu ambacho kinakosesha uhuru ndiyo maana nikaamua kubadilika.
Ijumaa: Kipi kilikuwa kinakukosesha amani ulipokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Nay?
Shamsa: Jinsi tulivyokuwa tunafuatiliwa maana ilikuwa hadi kero ndiyo maana hatukudumu.
Ijumaa: Kuna kipindi uliwahi kusema unavaa nguo za mitumba sana hata ‘makufuli’, huoni kwa staa kama wewe kuvaa nguo hizo ni kujishusha?
Shamsa: Noo, wala sioni tatizo maana nachagua zile zenye ubora kisha naziweka kwenye hali nzuri kabla ya kuzivaa.
Ijumaa: Unaizungumziaje serikali ya Magufuli?
Shamsa: Hakika mambo yanaenda vizuri, majipu yanatumbuliwa ila kwenye suala la mkwanja ndiyo kumebana ile mbaya.
Ijumaa: Unatofautisha vipi serikali ya sasa na ile iliyopita?
Shamsa: Tofauti ipo kwa kuwa uongozi ni wa watu wawili tofauti ila wote nawakubali, JK kafanya yake na Magufulia naye amekuja na kasi mpya.
Ijumaa: Kipi ambacho ungependa kuwaambia wasanii wenzako?
Shamsa: Kikubwa tupendane, tushirikiane, tuache majungu kwani kwa kufanya hivyo tutafika mbali na tasnia yetu itaheshimika.