×

Brigedia Jenerali atoa dawa ya madiwani wakata miti hovyo!

Brigadia Jenerali  Mstaafu, Emmanuel MagangaNa Mwandishi  Wetu

Baada ya kupata kero ya wananchi kuhusu tabia ya baadhi ya madiwani na watumishi wa umma pamoja na viongozi wa kisiasa kutumia nyadhifa zao kuharibu misitu kwa kukata miti hovyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,(RC) Brigadia Jenerali  Mstaafu, Emmanuel Maganga ametoa dawa kwa kusema watakaogundulika kufanya hivyo wataadhibiwa bila kujali nyadhifa zao na majukumu yao kwa jamii.

RC Maganga alitoa kauli hiyo hivi karibuni Uvinza kwa baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Buhungwe, alisema Kigoma ni moja ya mikoa michache yenye misitu mingi ya hifadhi, mito na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini bado kuna changamoto ya uharibifu wa mazingira.

“Nimepata taarifa kuwa kuna kero hapa, wapo baadhi ya madiwani wanaharibu mazingira kwa kukata miti kiholela, hawana vibali vinavyowaruhusu kufanya hivyo. Tukikukamata hatutajali udiwani wako, tutakuburuza mahakamani ukajibu tuhuma zako,” alionya kiongozi huyo.

Mfanyabiashara wa mkaa wa mjini Kigoma, Athanasi Kabula alilalamika kuwa kumekuwa na ukataji wa miti usiozingatia sheria na kusababisha misitu mingi kuteketea kwa kasi. Wafugaji nao wametajwa kufanya uharibifu huo kwa madai kuwa wanatafuta sehemu za kulima.

Mfugaji mmoja wa Kijiji cha Mpeta, wilayani Uvinza, Idelfonce Ng’ogamado alijitetea kuwa wanakata miti ili wapate mashamba;

“Utaishije porini bila kulima? Lazima tulime na maeneo  ya kilimo yapo misituni,” alisema.

Diwani wa Viti Maalum wa Uvinza, Salome Luhingulanya aliungana na mkuu wa mkoa kwa kusema kazi yao (madiwani) ni kuhakikisha watu wanatii sheria.

Leave a Comment