Hebu vuta picha, walinzi wa ikulu wakiwa kwenye harakati zao za kuhakikisha ikulu ipo salama, ghafla inatokea helikopta kutoka kusikojulikana, inaanza kuzunguka kwenye anga la ikulu bila taarifa yoyote.
Rubani wake anaonesha mbwembwe za hali ya juu kisha anatua jirani kabisa na ofisi ya rais, muda mfupi baadaye anaipaisha tena bila kusema chochote! Ni jambo la hatari si ndiyo?
Basi kwa taarifa yako, tukio kama hilo limewahi kutokea nchini Marekani. Ilikuwaje? Februari 17, 1974, njemba aitwaye Robert Preston, alifanya tukio lililowashangaza wengi kwa kuiba helikopta ya kijeshi, Bell UH-1 Iroquois na kupaa nayo hadi ikulu ya Marekani, White House.
Akawa anapiga misele angani kwa zaidi ya dakika sita huku akiichezesha kwa ustadi wa hali ya juu kisha akatua mita chache kutoka ilipokuwa ofisi ya rais, alipoona maafisa usalama wanamfuata, aliipaisha tena na kutaka kutokomea lakini helikopta nyingine mbili za kijeshi, zilianza kumfukuzia.
Alipoona zinamkaribia, alianza mbwembwe za kuichezesha helikopta hiyo angani, akasababisha moja ipate hitilafu na kutua kwa dharura, ikabakia moja ambayo aliishinda ujanja, akageuza tena na kurudi ikulu, hata hivyo alipofika tu, maafisa usalama walianza kumfyatulia risasi zilizomjeruhi kidogo, akalazimika kutua ndani ya eneo la ikulu. Wakati huo, rais na mkewe hawakuwepo ikulu.
Muda mfupi baadaye, alikamatwa na ikaja kubainika kwamba aliwahi kushiriki mafunzo ya kijeshi, kitengo cha urubani ingawa baadaye alifukuzwa chuoni, jambo lililomkasirisha na kupanga kumuonesha rais, kipindi hicho akiwa ni Richard Nixon kwamba licha ya kufukuzwa chuo, alikuwa anaweza kucheza na helikopta.
Baadaye alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela pamoja na faini. Tukio hilo, linatajwa kuchochea matukio mengine kama hayo ambapo watu wenye nia ovu, mara kadhaa walijaribu kuivamia ikulu hiyo kwa kutumia usafiri wa anga lakini hawakufanikiwa.