×

Mchungaji Akatisha Hotuba Ya Trump

Mchungaji wa kanisa moja la watu weusi katika jimbo la Michigan, Marekani amemkatisha mgombea urais wa chama cha Republican, bwana Donald Trump wakati akitoa hotuba yake na kuanza kumshutumu mpinzani wake, mgombea urais kupitia chama cha Democratic Hillary Clinton.

Mchungaji Faith Green Timmons, alimkatisha Bwana Trump alipomshutumu mgombea huyo wa chama cha Democratic kuhusu mikataba ya kibiashara duniani.

“Bwana Trump, nilikualika hapa uje kutushukuru kwa juhudi ambazo tumefanya Flint, si kutoa hotuba ya kisiasa,” alisema mchungaji huyo wa kanisa la Bethel United Methodist.

“Aha, hilo ni jambo njema,” alijibu mgombea huyo wa chama cha Republican huku akionekana kuanza kucheza na karatasi alizokuwa nazo jukwaani.

Bw Trump baadaye aliendelea na kuzungumzia kwa kifupi kuhusu kutatua matatizo ya maji safi Flint, lakini baadhi ya watu kwenye umati wakaanza kumzomea.

Mwanamke mmoja amesema kwa sauti kwamba mgombea huyo tajiri alitumia njia za kibaguzi katika majumba yake.

Mgombea huyo amejibu:

“Haiwezekani, umekosea. Nisingeweza kufanya hivyo.”

Mchungaji alilazimika kuzungumza tena na kuwashutumu waliokuwa wanamzomea Bw Trump na kusema:

 “Yeye ni mgeni katika kanisa langu na mtamheshimu”.

Bwana Trump mwishowe amelazimika kukatiza ghafla hotuba yake, ambayo imedumu kwa dakika sita hivi.

_91204122_hi035302611Donald Trump akiwa na mchungaji Faith Green Timmons.