Richard Bukos na Issa Mnally, Risasi MCHANGANYIKO
PWANI: Huu ni unyama asilimia mia! Ndivyo alivyoanza kusimulia mama wa marehemu Amina Mohamed Buyayo (28), Asha Mapande ambaye siku chache zilizopita, bintiye huyo alizikwa akiwa hai huko Njopeka-Mwarami Mketo, mkoani Pwani, Risasi Mchanganyiko lina simulizi nzito ya majonzi.
Marehemu Asha Mapande alizikwa akiwa hai Njopeka-Mwarami Mketo, mkoani Pwani.
TUJIUNGE NA MAMA MZAZI
Akizungumza na waandishi wetu mama huyo wa marehemu, alisema kabla ya tukio hilo lililobainika Agosti 20, mwaka huu, mwanaye huyo na mumewe aliyetambulika kwa jina la Yusuf Kiwingu, waliishi Bagamoyo mkoani Pwani zaidi ya miaka miwili.
SIMULIZI YA BAGAMOYO
“Wakiwa Bagamoyo inaonekana kama maisha yaliwashinda maana mwanangu alirudi hapa Njopeka kisha akaenda Kilwa kufanya biashara ya ufuta.
YUSUF AMSHTUKIZA
“Akiwa huko, Yusuf naye alitoka Bagamoyo na kumfuata Kilwa kwa kumshtukiza akijua labda alikuwa akiishi na mwanaume mwingine, lakini alimkuta akiwa peke yake.
Siku iliyofuata mwanangu alinipigia simu kuwa, kesho yake (Agosti 13) anatarajia kurudi hapa Njopeka hivyo tumsubiri kituoni ili tumpokee mizigo.
Mama wa marehemu Amina Mohamed Buyayo (28), Asha Mapande.
WAMPOKEA BINTI YAO
“Tulifanya kama alivyotuagiza lakini cha ajabu aliposhuka kituoni akatuambia tupeleke mizigo yake nyumbani yeye atakuja baadaye muda huo alikuwa anakwenda Kimanzichana kutafuta fremu ya biashara ambapo kuna mtu alishazungumza naye.
AREJEA NA YUSUF
“Akaenda alikosema lakini aliporudi alikuwa na Yusuf ambapo yeye alipoingia ndani Yusuf alibaki kule nje kama mtu aliyekuwa akijificha hakutaka tumuone. Baada ya kuona hali hiyo, baba wa marehemu aitwaye Mohammed Buyayo, alimuuliza mwanaye, yule uliyekuja naye ni nani mbona kama anajificha kule jalalani?
MAREHEMU AMTOA WASIWASI BABA’KE
“Marehemu alimwambia baba yake kuwa huyo ndiye mwanaume aliyekuwa akiishi naye Bagamoyo, hivyo baba yake akajua hakuna shaka kama ndiyo yeye.
Mumewe wa marehemu aliyetambulika kwa jina la Yusuf Kiwingu.
AMINA AONDOKA NA MWANAYE
“Baada ya kukaa kidogo, Amina akatuaga anakwenda na mwanaye mdogo aitwaye Zabibu (4) Kijiji cha Jaribu ambacho ni cha pili kutoka hapa, alisema anakwenda kuwasalimia wazazi wa mtuhumiwa. Kumbe alivyotuaga ilikuwa ndiyo anatuaga jumla,” alisema mama huyo huku akilia.
MWANAYE AREJEA PEKE YAKE
Bi mkubwa huyo alizidi kusimulia tukio hilo kwa uchungu huku machozi yakimtiririka;
“Baada ya kutuaga siku hiyo hakurudi lakini kesho yake mchana tukamuona mwanaye Zabibu akirudi peke yake na tulipomuuliza alimuacha wapi mama yake, hakuwa na jibu la kueleweka kutokana kutojua vizuri kuongea.
WAPATA WASIWASI
“Hapo tukazidi kupatwa na wasiwasi na kwenda Kijiji cha Jaribu, kumuulizia nyumbani kwa wazazi wa mtuhumiwa ambako tukamkuta Bi. Nyampapa ambaye ni mama wa mtuhumiwa yeye alisema hakumuona mwanangu, hivyo hofu ikazidi kuongezeka.
MWILI WAONEKANA
“Yaani tulimsaka mwanangu kila kona mpaka Agosti 20, mwaka huu mwili wake ulipokutwa umefukiwa, tena inasemekana alizikwa akiwa hai maana madaktari walipoufanyia mwili uchunguzi waliukuta ukiwa na mchanga ndani ya pua uliovutwa kuelekea kwenye koromeo, hivyo ni dhahiri alikuwa akipumua wakati anafukiwa,” alimaliza kusema mama huyo.
DIWANI ANENA
Akizungumzia tukio hilo, Diwani kwa Kata ya Njopeka, Mwarami Mketo, alisema kufuatia sakata hilo yeye na kamati yake ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na jeshi la polisi mwishoni mwa wiki iliyopita walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo maeneo ya Tandika Azimio, jijini Dar.
AWAPELEKA ENEO LA TUKIO
“Baada ya kumkamata alihojiwa na kuwapeleka askari kwenye chumba cha rafiki yake aitwaye Hamisi Chaurembo, kilichopo Kijiji cha Jaribu ambapo alikiri kufanyia mauaji hayo.
“Kibano kilipoendelea alitaja kuwa marehemu alimfukia hivyo alitakiwa kutaja chombo alichotumia kuchimba na kumfukia ambapo alisema alitumia chepe.
AANIKA ALIPOPATA CHEPE
“Kibano kikiendelea, alitakiwa kutaja alipolipata chepe hilo ambapo aliwapeleka askari kwenye nyumba aliyoomba chepe hilo ambapo waliompa baada ya kuhojiwa walisema alipowaomba hawakujua alichotaka kufanyia.
AWAFIKISHA ALIPOMFUKIA
“Mambo hayakuishia hapo, jamaa alitakiwa kwenda kuonesha alipomfukia mkewe huyo ambapo aliongoza mpaka Kijiji cha Malenda eneo ambalo mwili wa marehemu ulikutwa,” alisema Diwani Mketo.
KAMANDA ATHIBITISHA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Bonaventura Mushongi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kukamatwa kwa mtuhumiwa Yusuf na taratibu za kisheria zinafanyika ili kumfikisha mahakamani.
MAZISHI
Mara baada ya mwili wa Amina kufukuliwa na taratibu za kipolisi kukamilika, ulizikwa upya Agosti 20, mwaka huu kwenye Makaburi ya Serikali ya Kijiji cha Njopeka. Marehemu ameacha watoto wawili; Zabibu (4) na Asha Jumanne (9).
MAMA AOMBA MSAADA
Mama wa marehemu anaomba wasamaria wema kumsaidia kuwasomesha watoto hao kwakuwa wanaishi katika mazingira magumu kiuchumi.



