Kutoka kushoto ni Mratibu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Makame A.K , Mkurugenzi wa Haak Neel Production, Godfrey Katula (anayezungumza kati) na Msanii wa Bongo Fleva, Peter Msechu.
Kutoka kushoto ni Mratibu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Makame A.K , Mkurugenzi wa Haak Neel Production, Godfrey Katula (anayezungumza kati) na Msanii wa Bongo Fleva, Peter Msechu.
Mchekeshaji wa kuigiza sauti za baadhi ya viongozi hapa nchini, Adam Upanga ‘Mlugaluga’ (katikati) akielezea namna alivyojipanga kutoa vichekesho siku hiyo.
Msanii wa Bongo Fleva, Juma Kassim ‘Nature’ akielezea namna atakavyowapagawisha mashabiki zake.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMASHA LA SANAA (24 SEPTEMBA 2016)
UTANGULIZI
Siku ya msanii ni mradi uliobuniwa na Baraza la Sanaa la Taifa ukiwa a lengo la KUTAMBUA, KUHAMASISHA na KUTHAMINI kazi na mchango mkubwa unaotolewa na wasanii mbalimbali hapa nchini. Siku hii imeanza kuadhimishwa rasmi hapa nchini kuanzia mwaka 2014 ambapo baadhi ya wasanii waliweza kupewa tuzo na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Mh, Dr. Mohamed Gharib Bilal kutokana na umahiri wao kwenye Sanaa walizozifanya na kuliletea taifa sifa ndani na nje ya Mipaka.
Mradi huu umeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuwashirikisha wasanii na wadau wengi Zaidi wa Sanaa hapa nchini kama ambavy itaendelea kushuhudiwa mwaka huu kwenye maadhimisho ya SIKU YA MSANII 2016.
SIKU YA MSANII 2016
Siku ya Msanii mwaka 2016 imejumuisha mtiririko wa matukio ambayo yanakwenda kuakisi kaulimbiu yake ya mwaka huu yaani “NGUVU YA SANAA” Tayari maadhimisho haya yalizinduliwa mnamo tarehe 26 mwezi Mei 2016 kwenye ukumbiwa Alliance Francaise ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Moses Nnauye ambaye aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel. Uzinduzi huu ulidhihirisha kukua kwa maadhimisho haya kwani yalihusisha mjumuiko wa Sanaa kutoka nchi ya Ufaransa ambapo pia mjumuiko huu utaendelea kwenye matukio mengine yajayo hasa tukio la TAMASHA LA SANAA ambalo linakuja hapo tarehe 24 mwezi Septemba 2016 pale kwenye viwanja vya kijiji cha Makumbusho Kijitonyama Dar es salaam.
Maadhimisho ya mwaka huu kilele chake kitakuwa hapo tarehe 29 Oktoba 2016 ambapo wasanii mbalimbali watapewa tuzo ambapo baadhi ya wasanii watakaokuwa wamepitia mchujo mkali wa kitaaluma na vigezo vilivyowekwa watatunukiwa tuzo mbalimbali kuonyesha mchango wao kwenye sekta ya Sanaa na taifa kwa jumla.
TAMASHA LA SANAA
Kwa mara ya kwanza hapa nchini, SIKU YA MSANII inawakutanisha wasanii wa aina zote nneza Sanaa kwenye eneo moja yaani Sanaa za muziki, filamu, ufundi na maonyesho ili kuonyesha umahiri wao kwa hadhira. Hili ni tamasha la siku nzima yaani kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 3 usiku likiwa halina kiingilio ambapo kutakuwa na maonyesho ya kazi mbalimbali za Sanaa kama ufundi na maonyesho na baadae kuhitimishwa na burudani mbalimbali za muziki kutoka kwa wanamuziki wa mitindo mbalimbali ya muziki ikiwa na lengo la kuonyesha Nguvu waliyonayo wasanii pale wanapoungana pamoja.
SHUGHULI ZITAKAZOKUWEPO
- Tamasha hili litapambwa na shughuli mbalimbali ili kuifanya kuwa siku maalum ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake kufika na familia zao nawao pia kujionea umahiri wa wasanii wetu nchini. Shughuli zitakazokuwepo ni pamoja na;
- Maonyesho ya kazi za Sanaa za ufundi (uchongaji, ufinyanzi, ushonaji, ufinyanzi na nyingine nyingi) siku hii wale wasusi wote maarufu hapa mjini watahamia kwenye tamasha la Sanaa hili hivyo wale kina mama siku hiyo waje makumbusho kusukwa.
- Maonyesho maalum ya filamu za kitanzania ambapo pamoja na kuona wadau wa filamu watapata fursa ya kununua filamu kazi zilizotengenezwa na wasanii wetu maarufu hapa nchini.
- Burudani ya muziki wa aina zote utakuwepo huku ukisindikizwa na burudani kutoka kwa ma DJ maarufu wa enzi hizo wakishirikianana ma DJ wa sasa ili kuhakikisha wadau wanapata burudani isiyochosha kwa siku nzima.
- Kutakuwa pia na huduma ya chakula na vinywaji kuanzia asubuhi mpaka jioni ili watu watakaofika kwenye viwanja vya makumbusho waweze kupata huduma zote kusindikizia burudani zitakazokuwepo hapo.
- Kutakuwa na huduma ya uchangiaji damu
- Kutakuwa na Jukwaa la Sanaa ambalo litaongozwa na BASATA na Cosota katika kutoa elimu kwa wasanii mbalimbali.
- Kutakuwa na elimu ya mifuko ya jamii kwa wasanii na jamii ambayo itakuja katika Tamasha.
BURUDANI
Tamasha hili litashereheshwa na wasanii wa muziki mbalimbali kama ifuatavyo;
Bongo fleva; Juma Kassim Nature, Peter Msechu Misoji na wengine wengi ambao watapanda katika jukwaa.
Muziki wa Dasi; CHAMUDATA All Stars (wasanii maarufu wa zamani wataungana na wasanii wa sasa kutoa burudani).
Ifakara Band, John Kitime.
Singeli; Amsha Group na makundi mbalimbali ya singeli.
Ngoma za Asili; Mandela Group, Safari Group na sarakasi.
Taarab; Siza Segere na Super Shine.
Komedi/Mchekeshaji; Mlugaluga na wachekeshaji mbalimbali.
Ma DJ; Dj Ibony Moalim
DJ John Pantalikis
Dancer Athuman Diga Diga.
Wanamuziki mbalimbali wa nyimbo za injili pia watatoa burudani kuhamasisha Amani ya nchi yetu.
Mtiririko wote huu wa burudani utawahakikishia wadau mbalimbali wa Sanaa watakaofika kuendelea kuwepo mpaka itakapofikia tamati ya tamasha hili kubwa kabisa la Sanaa hapa nchini na ulinzi utakuwa wa uhakika kwani tumejipanga vizuri sana, wapenzi wa nyama choma zitakuwapo kwani maandalizi yake yamekamika kila kitu tulichopanga kitakuwapo bila kukosa.
MGENI RASMI
Mgeni rasmi kwenye Tamasha hili la Sanaa atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Anastacia Wambura (Mb) ambaye pia ataambatana na wageni wengine mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi yetu.
MWISHO
Imeandaliwa
Godfrey Mahendeka
Mkurungezi