Mshindi wa Kwanza wa Chemsha Bongo na Amani, Bakari Omary Omuga wa Dar es Salaam.

Mshindi wa Pili wa Chemsha Bongo na Amani, Godwin Deodath Katiali wa Kilimanjaro.
Mshindi wa tatu wa Chemsha Bongo na Amani, Jimmy Kisanga akiwa ameshikilia zawadi yake ya Sh. 500, 000 mara baada ya kukabidhiwa.
Na Mwandishi Wetu
UNAYO nafasi! Hadi sasa Chemsha Bongo ya Gazeti la Amani imeshawapa zawadi ya shilingi 500,000 washindi watatu kutoka mikoa tofauti ambao ni Bakari Omary Omuga wa Dar es Salaam, Godwin Deodath Katiali wa Kilimanjaro pamoja na Jimmy Kisanga wa Mwanza, wewe unasubiri nini?
Chemsha Bongo hiyo imekuwa ikirahisisha maisha ya washindi mbalimbali ambao wamejishindia. Bakari Omuga ambaye ni mshindi wa kwanza wa chemsha bongo hiyo tangu ianze, mara baada ya kushinda kiasi hicho cha pesa aliweka wazi kuwa ilimsaidia kumalizia deni la bodaboda alilokuwa akidaiwa.
“Nilipotangazwa mshindi kwanza sikuwa naamini. Akili na mawazo yangu kila siku ni kupata pesa na kumalizia deni la bodaboda niliokuwa nadaiwa dukani. Sasa hivi nina amani, nimeshamalizia na kuichukua bodaboda yangu kutokana na Gazeti la Amani.
“Niwaombe tu kwa wale ambao hawajalisoma, mbali na kuletewa hiyo chemsha bongo pia ni gazeti bora lililosheheni vitu vingi kama vile hadithi za kusisimua, habari za kijamii na mastaa kifupi ni gazeti lililoshiba. Sasa hivi mwenzenu bado naendelea kushiriki chemsha bongo hiyo kwani mbali na kiasi hicho cha pesa pia unaweza kujishindia safari ya kwenda Dubai na kula bata kwa siku tatu,” alisema Bakari.
Kwa upande wa mshindi wa pili, Deodath kutoka Njia Panda ya Machame, Moshi mkoani Kilimanjaro mara baada ya kushinda alisema, imekuwa ‘sapraizi’ kwake kwani siku aliyoambiwa ameshinda kidogo aanguke kutoka juu ya jukwaa.
“Ujue mimi ni fundi umeme na siku nimeambiwa nimeshinda 500,000 kidogo nianguke kutoka jukwaani nilipokuwa nikitengeneza umeme, sikuamini! Kiasi nilichoshinda kimeniokoa kwa kiasi kikubwa kumalizia fremu yangu kwani ilibaki vitu vidogo kama mabati na milango,” alisema Deodath.
Mshindi wa tatu, Jimmy kutoka Mwanza ambaye ni mfanyakazi Bodi ya Pamba kitengo cha kuendeleza zao la pamba naye aliweka wazi furaha ya ushindi wake kuwa, pesa hiyo imemuokoa ada ya mtoto wake.
“Nina mke na watoto watatu, mmoja yupo darasa la kwanza mwingine la tatu na wa mwisho hasomi. Sasa huyu wa darasa la tatu anasoma shule ya Olimpio na alikuwa akidaiwa ada, niwe mkweli zawadi hii imeniokoa ada ya mtoto,” alisema Jimmy.
Chemsha Bongo hiyo bado inaendelea katika Gazeti la Amani. Ili kushiriki ni rahisi sana, unachotakiwa kufanya ni kununua gazeti hilo kila Alhamisi na kujibu swali kiufasaha linalopatikana ukurasa wa pili. Kumbuka mshindi pia anaweza kupata safari ya kwenda kwenye jiji la maraha duniani, Dubai kula bata kwenye hoteli ya kifahari kwa siku tatu.

